Simba, Azam mechi ya pointi muhimu
Muktasari:
- Hii ndiyo mechi ya Simba kuonyesha kwamba chini ya Abelhack Benchikha si Azam wala Prince Dube anayeweza kuendeleza tambo za Mzizima. Hii ndio mechi sasa ya kuonyesha makali ya vifaa vipya baada ya kufungwa kwa dirisha dogo.
Achana matokeo ya Yanga jana, Simba leo ipo Kirumba kuvaana na Azam.Mechi hii ndiyo imebeba hatma ya mbio za ubingwa wa timu zote mbili. Yoyote atakayefungwa anampa Yanga nafasi ya kupumua na kuzidi kukaa kileleni.
Hii ndiyo mechi ya Simba kuonyesha kwamba chini ya Abelhack Benchikha si Azam wala Prince Dube anayeweza kuendeleza tambo za Mzizima. Hii ndio mechi sasa ya kuonyesha makali ya vifaa vipya baada ya kufungwa kwa dirisha dogo.
Acha tuone dabi ya kwanza ya Mzizima kupigwa kwenye mechi za ligi ikipigwa Uwanja wa CCM Kirumba inakuwa na ladha gani.
Ni nadra sana, timu hizo kukutana kwenye mechi ya ligi na kucheza nje ya Dar es Salaam. Zimekutana mara 30 kwenye ligi tangu Oktoba 4, 2008, lakini ni mara moja tu mtanange baina yao umepigwa nje ya Dar es Salaam.
Ilikuwa Septemba 11,2010, ambapo mwenyeji alikuwa Azam mechi ikapigwa Mkwakwani, Tanga na hata hivyo, ilipoteza kwa mabao 2-1. Mechi nyingine zote zilipigwa Dar es Salaam katika viwanja vya Uhuru, Mkapa na Azam Complex lakini sasa Simba imeipeleka hii CCM Kirumba Mwanza baada ya Uhuru na Mkapa kufungiwa kwa matengenezo.
Mara ya mwisho Simba kutwaa taji ilikuwa msimu wa 2020/2021, huku Azam ikilitwaa mara moja tu tena bila kupoteza mchezo msimu wa 2013/2014.
Yanga ndio imelitwaa taji hilo kwa misimu miwili iliyopita mfululizo pia imelitwaa mara nyingi zaidi (29), na msimu huu bado inalitaka lakini ushindani ni mkubwa kutoka kwa Simba na Yanga na hadi sasa haijafahamika na mechi ya leo inaweza kutoa picha halisi.
Mchezo wa leo utakuwa wa 13 kwa Simba na 14 kwa Azam. Kama Simba itashinda mechi ya leo itafikisha pointi 33 na kuzidi kuiondoa Azam kwenye mbio za ubingwa, lakini ikishinda Azam itafikisha alama 34 na kuipa ugumu Simba kuwania ubingwa.
Kufunga kawaida
Mechi inayozikutanisha timu hizi mara nyingi nyavu hazilali njaa. Katika mechi 10 za ligi zilipokutana ni mchezo mmoja tu ulimalizika bila bao (0-0), mechi nyingine zote zimetoa mabao kwani yamefungwa jumla ya mabao 24 kwenye mechi hizo 10, ambapo Simba imefunga 14 na Azam imefunga 10 huku mechi iliyozalisha mabao mengi zaidi ikiwa ile ya Machi 4, 2020 ambapo Simba ilishinda 3-2.
Licha ya kila timu kuwa na kikosi imara kwenye kila idara lakini mechi hii huenda ikaamuliwa na viungo kutokana na eneo hilo kuwa nguzo ya kila upande.
Babacar Sarr, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Said Ntibanzokiza na Clatous Chama, ni wachezaji watano wa Simba wanaopata nafasi mara kwa mara kucheza eneo la kuingo na wamekuwa imara katika kujilinda na kutengeneza mabao ikiwemo kufunga.Saido ana mabao matano, Kanoute ana mawili, Chama ana mawili, Ngoma yakiwa ni jumla ya mabao 10.
Kwa upande wa Azam eneo la kiungo wanacheza James Akaminko, Feisal Salum 'Fei Toto', Sospeter Bajana, Kipre Junior na Djibril Sylla ambapo kwa ujumla wamezalisha zaidi ya mabao 15 kwani Sylla na Bajana kila mmoja amefunga mabao matatu, Kipre akifunga manne na Fei Toto akifunga nane jumla ikiwa 18. Hapo haujaweka Asisti.
Simba kamili, Azam wanne nje
Timu zote zinatamba kuibuka na ushindi kwenye mechi ya leo ambapo kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola alisema watapanga wachezaji ambao wanaamini watashinda mechi ya leo.
“Tunajua ubora na ugumu wa Azam tunajipanga kuhakikisha tunapata pointi tatu safari ni ndefu tulilijua hilo na tumeweza kufanya wachezaji wote wako salama tunaamini tutakuwa tayari kwa mchezo na kufanya vizuri, mashabiki tunataka tuwahakikishie kwamba tutafanya kile kitu ambacho kila mwanasimba anakitarajia,” alisema Matola.
Kwa upande wa kocha wa Azam, Bruno Ferry alisema atawakosa nyota wake wanne, Sospeter Bajana, Andallah Heri, Malikou Ndoye na Allasane Diao lakini akisema wamejiandaa kushinda.
"Ni mchezo muhimu, tumejiandaa vizuri na tuko tayari kwa mchezo. Wapinzani wetu ni wazuri tunajua wana benchi zuri na wachezaji bora na tunafahamu ukiwa Simba una presha ya kushinda. Natumaini kesho mambo yatakwenda vizuri na mchezo utavutia,” alisema Ferry.