Simba, Azam zamlilia Ndugai, Singida BS nayo imo
Muktasari:
- Ndugai amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 62 na amewahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dar es Salaam. Simba, Azam na Singida Black Stars zimeungana na taasisi na watu mbalimbali kuomboleza kifo cha aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai.
Ndugai amefariki dunia leo katika Hospitali mojawapo jijini Dodoma ambako alikuwa anapatiwa matibabu.
Taarifa ya Simba imesema kuwa imepata pigo kubwa kwa vile Ndugai alikuwa shabiki wao.
“Uongozi wa klabu ya Simba umepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Spika mstaafu na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Job Yustino Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma.
“Katika kipindi cha uhai wake, Hayati Ndugai alikuwa mwanachama wa klabu yetu na hajawahi kuficha mapenzi yake kwa Simba.
“Simba inatoa pole za dhati kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson na pia inaungana na Watanzania, wananchi wa Jimbo la Kongwa, familia, ndugu,jamaa na marafiki kuomboleza msiba huu mzito kwa Taifa,” imesema taarifa ya Simba.
Taarifa ya Azam FC imesema, Tunaungana na Watanzania wote na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuomboleza kifo cha Spika Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai.
“Bwana alitoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe.”
Nayo Singida Black Stars imeonyesha kusikitishwa na kifo cha Ndugai.
“singidablackstars Tumepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai.
“Tunatoa pole kwa familia, Bunge la Tanzania na Watanzania wote. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” imesema taarifa ya Singida