Simba, Biashara hesabu tu

Thursday February 18 2021
Simba pic
By Charles Abel

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanashuka uwanjani leo kuikabili Biashara United utakaochezwa kuanzia saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Karume, mkoani Mara.

Hesabu za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu na mchezo wa raundi ya pili ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly siku sita zijazo, vinaifanya Simba ihakikishe inapata ushindi leo, vinginevyo hali haitokuwa nzuri kwa upande wao.

Ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na pointi 39, Simba ikishinda leo itafikisha jumla ya pointi 42 na itahitaji pointi tatu tu iweze kuwafikia Yanga na kuongoza msimamo kwa faida ya utofauti mzuri wa mabao.

Lakini kama itapoteza au kutoka sare, Simba itaiweka Yanga katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu kwani hata ikishinda mechi yake ya kiporo, Yanga itaendelea kubaki kileleni mwa msimamo.

Ukiondoa hilo, ushindi leo utaiweka Simba katika hali nzuri kisaikolojia kuelekea mchezo wake wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, ambao inahitaji ushindi kufikisha pointi sita zitakazoifanya kukaa kileleni mwa Kundi A.

Katika mchezo wa leo itaingia uwanjani ikiwa na pigo la kuwakosa wachezaji wake sita, ambao wamebakia nchini DR congo kutokana na kutopatiwa vyeti vya vipimo vya ugonjwa wa Covid-19, ambao ni Rally Bwalya, Erasto Nyoni, Ally Salim, Jonas Mkude na Kennedy Juma.

Advertisement

Rekodi baina ya timu hizo mbili, zinaonyesha kwamba Simba imekuwa ikitamba zaidi pindi zikutanapo katika Ligi Kuu, tangu msimu wa 2018/19, ambao Biashara United ilishiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.

Katika mechi tano ambazo zimekutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu, Simba imeibuka na ushindi mara nne na zimetoka sare mara. Mechi zote mbili ambazo Simba imecheza dhidi ya Biashar United ikiwa ugenini huko Mara, imepata ushindi bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa na imepachika mabao manne.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema licha ya kuiheshimu Simba, wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

“Tunacheza dhidi ya timu nzuri yenye wachezaji bora lakini naamini vijana wakifanyia kazi kile ambacho tumeelekezana, tunaweza kupata ushindi.

Kimsingi mechi kama hizi unatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu katika dakika zote 90 za mchezo,” alisema Baraza.

Kocha wa Simba, Didier Gomez Da Rosa alisema kuwa wanatambua ubora wa Biashara United na anaamini wana kazi kubwa ya kufanya ili kupata ushindi.

“Tumekuja hapa tukiwa na hali ya kujiamini. Tunatambua kwamba Biashara United ni timu nzuri na ndio maana sio ajabu kuona ikiwa katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

Nimewaona kwenye mechi zao na kwa maandalizi tuliyoyafanya, tunaamini tunaweza kuvuna pointi tatu ingawa mchezo utakuwa mgumu,” alisema Da Rosa.

Azam FC baada ya kutoka kupoteza dhidi ya Coastal Union watakuwa na kibarua cha kusawazisha makosa yao wakati watakapoikabili Mbeya City ambayo juzi imetoka kupata sare ya bao 1-1 na yanga.

Azam wanaingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri ya kupoteza mechi moja tu kati ya 15 ilizocheza dhidi ya Mbeya City, wakishinda tisa na kutoka sare mara moja.

Hata hivyo, mara hiyo moja ambayo Azam walipoteza, ilikuwa ni kwa pointi za mezani, ambayo Mbeya City ilipewa, lakini katika dakika 90, Azam walishinda kwa mabao 3-0.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa kuanzia saa 1 usiku katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Kwinginepo, mkoani Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri, kutakuwa na vita ya Maafande, wakati JKT Tanzania watakapoikaribisha Polisi Tanzania.

Katika mchezo wa jana, Dodoma Jiji iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Advertisement