Simba hiyoo Dubai, MO Dewji amwaga manoti

Muktasari:

  • KIKOSI cha Simba, jana kiliwasili jijini Dar es Salaam kikitokea Zanzibar ilikotolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 na fasta mchana wa leo itakwea pipa kwenda kambi ya wiki moja mjini Dubai baada ya bilionea wa klabu hiyo, Mohammed 'Mo' Dewji kumwaga noti klabuni.

KIKOSI cha Simba, jana kiliwasili jijini Dar es Salaam kikitokea Zanzibar ilikotolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 na fasta mchana wa leo itakwea pipa kwenda kambi ya wiki moja mjini Dubai baada ya bilionea wa klabu hiyo, Mohammed 'Mo' Dewji kumwaga noti klabuni.

Mo Dewji amemwaga fedha hizo na kuisafirisha timu Dubai kwa lengo la kumrahisishia kazi kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Robert Oliveira 'Robertinho' ambaye jana alianika sababu ya kumleta kocha Mtunisia ili kumsaidia kazi sambamba na kina Juma Mgunda.

Nyota wa Simba waliopo Dar baada ya kurejea kutoka Zenji na waliobaki kwa mapumziko wanaingia kambini leo asubuhi na mchana watapaa kwenda Dubai kwa kambi ya wiki moja kabla ya kurejea nchini kuendelea na mechi za Ligi Kuu Bara.

Shoo nzima ya safari hiyo inasimamiwa na MO Dewji kama Mwanaspoti lilivyodokeza Jumatatu iliyopita kwa kugharamia tiketi za ndege, hoteli, viwanja vya mazoezi, gym, usafiri, chakula na vinywaji kwa muda wote timu ikiwa huko.

Bilionea huyo ameitaka kambi iwepo Dubai ili kumpa utulivu na muda kocha Robertinho ili azoeane na wachezaji kabla ya kurejea kuvaana na Mbeya City, huku wachezaji waliokuwa nje kama Clatous Chama na Moses Phiri wanaweza kuunganisha safari yao kutoka Zambia wakati Peter Banda na Israel Mwenda watasalia Dar kusubiri kikosi kirejee kwani ni majeruhi.

Kambi hiyo itakuwa imemfurahisha Robertinho kwani alishaomba mapema juzi ili apate muda wa kuwalisha falsafa yake wachezaji wa timu hiyo, huku akiweka bayana sababu ya kumleta Oussama Sellami aliyewahi kufanya kazi katika timu ya Stade Tunisien.

Kocha huyo msaidizi anatarajiwa kuwasili nchini muda wowote baada ya kukwama kuja jana kama taarifa ya awali iliyopenyezwa kwa Mwanaspoti na Robertinho alipoulizwa jana mara baada ya kuwasili Dar kutoka Zenji alisema kwa kifupi;

"Muda mchache nipo kwenye timu masuala mengine yote ya maboresho hayo si yangu bali ya uongozi ila nimekuja Simba kuifanya timu hiyo kuwa bora kwa wachezaji, benchi la ufundi ili kuchukua mataji mengi."

Lakini taarifa zinasema Robertinho anamleta Sellami ili kumrahisishia kazi, ni mtu wanayeelewana sana, kwani wamekuwa wakifanya kazi pamoja, licha ya kuwataka wazawa aliowakuta kuendelea kubaki kikosini.