Simba ipitie hapa, itatoboa

Muktasari:

  • Klabu ya Simba inaelekea kumaliza msimu wa pili sasa bila ya taji lolote na uamuzi mgumu unapaswa kufanywa ili kuirejesha timu hiyo katika makali yake.

Dar es Salaam. Baada ya kutawala soka la nchi kwa miaka minne mfululizo, Simba inaelekea kumaliza msimu wa pili sasa bila ya taji lolote na uamuzi mgumu unapaswa kufanywa ili kuirejesha timu katika makali yake.

Juzi Simba ilifungwa mabao 2-1 na Azam FC katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports na kutolewa katika michuano hiyo ya pili kwa ukubwa nchini baada ya Ligi Kuu Bara ikiwa ni siku chache tu tangu Wekundu wa Msimbazi walipoyatupa matumaini madogo yaliyokuwapo katika kuwania ubingwa wa ligi ilipolazimishwa sare ya 1-1 na Namungo FC, pale Ruangwa.

Simba ilionekana kuyatia katika pipa la taka matumaini madogo ya kuibana Yanga hadi mwisho wa msimu katika mbio za ubingwa pale ilipopanga kikosi cha wachezaji ambao hawakuwa wakianzishwa msimu mzima, na kama ilivyotarajiwa hawakuwa na madhara mbele ya ‘The Southern Killers’.

Sare hiyo kwenye Uwanja wa Majaliwa, ilikuwa ni pigo kubwa kwa Simba, hasa baada ya vinara Yanga kushinda 2-0 mechi yao ya ugenini dhidi ya Singida Big Stars na sasa Wanajangwani wanahitaji pointi tatu tu kutoka katika mechi tatu zilizobaki ilikutwaa taji lao la pili mfululizo la Ligi Kuu na la 29 la rekodi ya kihistoria tangu ligi hiyo ilipoanzishwa mwaka 1965.


SIMBA ILE TAMU

Wakati Simba ikitwaa ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu 2018 baada ya miaka mitatu mfululizo ya utawala wa Yanga, wengi waliitabiria makubwa na haikuwaangusha mashabiki wake.

Ilitwaa kibabe ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo kuanzia 2017-18, 2018-19, 2019-20 na 2020-21.   

Simba hii ilikuwa na kikosi bora na ilikuwa inapiga soka la kumrusha roho mpinzani yeyote – sio Tanzania tu bali Afrika nzima. 

Wababe wa Afrika, wakiwamo mabingwa mara 10 wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly na wababe wengine kama Kaizer Chiefs, Orlando Pirates na wengine walikiona cha moto walipokuja Kwa Mkapa. Simba hii ilikuwa inakufunga kwa sababu imekuzidi, sio kwa kukubahatisha.

Ndio maana hamna aliyeshangaa ilipocheza robo fainali ya michuano ya Caf mara tatu katika miaka minne.

Lakini sasa mambo yamebadilika.


MSIMU MBAYA

Simba msimu huu imefika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na ukilinganisha na misimu mingine huu ndio mwaka ambao imekaribia zaidi kutinga nusu fainali pale ilipotolewa na mabingwa watetezi Wydad Casablanca kwa penalti 4-3 kule Morocco. Simba ilishinda mechi ya mkondo wa kwanza Dar es Salaam kwa bao 1-0 kabla ya kufungwa 0-1 ugenini na mechi kuamuliwa kwa ‘matuta’.

Mechi ya mkondo wa kwanza Dar es Salaam, Simba iliupiga mwingi, ikashinda bao 1-0 katika mchezo ambao ingeweza kushinda 2-0 au zaidi. Clatous Chama, ambaye ameibeba Simba msimu mzima kutokana na kufunga mabao na kutoa asisti alipoteza fursa adhimu ya kuifungia Simba bao la pili katika dakika za lala salama pale Kwa Mkapa ambalo pengine lingeimaliza mechi ile na Chama tena hakuwa na bahati kule Casablanca alipokosa moja ya penalti mbili zilizoing’oa Simba mashindanoni pamoja na Shomary Kapombe.  Chama hakuwa na siku nzuri tena alipokosa nafasi mbili za wazi dhidi ya Azam, nyingine akikosa Kibu Denis wakati wakiaga katika michuano ya Kombe la ASFC.

Baada ya Simba kupoteza nafasi ya dhahabu ya kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika mfumo wa sasa, nguvu zikawekwa katika Kombe la ASFC ambako Wekundu walikuwa wakisubiri mechi yao ya juzi ya nusu fainali dhidi ya Azam FC. Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Hatutakubali kumaliza msimu mikono mitupu… Uwanja wa Nangwanda ni wetu, Azam hawana mashabiki pale.”

Lakini baada ya mechi hiyo waliyolala 2-1, kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda alikiri: “Tumekuwa na msimu mbaya.”


TATIZO LIKO HAPA

Wakati Simba inamchukua kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ilikuwa tayari iko katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikivuka hatua za kufuzu chini ya kocha wa mpito, Juma Mgunda baada ya Pablo Franco kufutwa kazi.

Robertinho amesaidia kuiimarisha Simba, licha ya kuanza makundi kwa kusuasua kwa vipigo viwili, ilifuzu robo fainali kwa kishindo ikiwamo kutoa kipigo kikubwa zaidi katika michuano hiyo ya Caf mwaka huu cha mabao 7-0 dhidi ya Horoya na kumfunga 1-0 bingwa mtetezi Wydad Dar es Salaam huku pia ikiumaliza unyonge wa miaka miwili dhidi ya Yanga kwenye ligi kwa kuifunga 2-0 katika Dabi ya Kariakoo.

Lakini hayo siyo malengo ya Simba, malengo ilikuwa ni ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la ASFC na nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.

“Msimu mbaya” wa Simba, unaweza kuwa umechangiwa na mambo mengi yakiwamo kikosi chembamba, majeraha kwa wachezaji na baadhi ya uamuzi wa kocha Robertinho.

Baada ya kuwasili, Robetinho alieleza jinsi anavyovutiwa na uchezaji wa Kibu Denis na akampa zawadi binafsi na kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara. Kibu akajenga heshima kubwa miongoni mwa mashabiki wa Simba hasa baada ya kufunga bao lile la mshuti mkali kama anayeua nyoka katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Yanga.

Lakini bao hilo ni kati ya mambo yaliyochangia kuficha takwimu ambazo hazivutii sana kuhusu Kibu, ambaye hadi sasa msimu huu ana mabao mawili tu kwenye Ligi Kuu tofauti na msimu uliopita ambao alikuwa mfungaji bora wa Simba akiwa na mabao manane.

Kinara wa mabao wa Simba, Moses Phiri ambaye ana mabao 10 kwenye ligi alikuwa na msimu bora kabla ya kuumia. Lakini alijikuta akipoteza namba kwa Robertinho ambaye ameonekana kuvutiwa zaidi na mchango wa Kibu. Kubadili mabao 10 kwa mawili kunaweza kuwa ni kati ya vitu vilivyochangia kuikwamisha Simba.

Kuumia kwa kipa chaguo la kwanza Aishi Manula kulizaa tatizo jingine kwa Simba kuelekea mwisho wa msimu, ambako kila kitu huamuliwa katika mbio za mataji.

Kipa chaguo la pili, Beno Kakolanya alizungukwa na uvumi kwamba ameuzwa kwa Singida Big Stars ambayo itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao na hivyo Simba ikalazimika kumuamini kipa wa tatu, Ally Salim.

Licha ya kujiamini na kucheza vyema baadhi ya mechi ikiwamo dhidi ya Yanga, Salim alikosa uzoefu ambao uliigharimu Simba kutolewa katika Ligi ya Mabingwa, Kombe la ASFC na hata kuangukia mbali na mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ambako makosa ya kutema mipira yaliifanya timu yake ikose matokeo muhimu.

Simba katika ushambuliaji imekuwa ikimtegemea mchezaji ambaye yuko katika timu hiyo kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya DR Congo, Jean Baleke na haina kikosi kipana kwa sababu wachezaji ambao hawachezi mara kwa mara, wamekuwa katika wakati mgumu kila kocha anapojaribu kubadili kikosi kwa kuwapumzisha mastaa wa kikosi cha kwanza.


NINI KIFANYIKE

Msimu unaonekana umeshaisha kwa Simba, nguvu kubwa inapaswa kuwekwa sokoni katika kusaka wachezaji wa kiwango cha juu cha kushindana na miamba ya Afrika ambayo hutumia pesa nyingi kusajili wachezaji wakubwa.

Sio wakati wote wachezaji wazuri hupatikana kwa pesa nyingi, lakini ni lazima kazi kubwa ifanyike ili kuiimarisha zaidi Simba.

Kuwavimbia mabingwa wa Afrika na kuwafunga 1-0 Kwa Mkapa, kuwapasua mabingwa wa Tanzania 2-0 na kuwa timu iliyotoa vipigo vikubwa zaidi katika Ligi ya Afrika (7-0 vs Horoya) na Ligi Kuu Bara (7-1 vs Tanzania Prisons) , ni uthibitisho kwamba Simba sio timu mbovu kama baadhi wanavyodhani, inahitaji marekebisho machache ili kurejesha utawala wake.