Simba yafafanua sakata la FCC

Monday January 18 2021
fcc PIC
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Siku chache tangu Tume ya Ushindani (FCC) kutangaza kuanza kufanya uchunguzi wa mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu ya Simba, inayowahusu wadaawa watano Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo imesema hakuna kitakachoharibika kwani kila kitu kipo sawa.

Katika tangazo lao, FCC walibainisha kwamba uchunguzi huo utaanza kufanywa kwa wadaawa watano ambao ni Simba Sports Club Holding Company Ltd, Simba Sports Club Company Ltd, Simba Sports Club, Mo Simba Company Ltd na Mohammed Gulamabbas Hassanali Dewji.

Tume hiyo pia ilitangaza kuwa ndani ya siku 21 inaruhusu kupokea pingamizi kwa mtu yoyote kuhusiana na mchakato huo wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.

Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kuwa hawana shaka na hatua za mchakato wao hata kama FCC wameamua kufanya uchunguzi kwao walipeleka mchakato huo kwa ajili ya kuomba ushauri tu.

“Sioni kama kuna tatizo lolote lililofanywa kinyume na taratibu za mfumo wa mabadiliko, kikubwa wanachama tulikubaliana kuingia kwenye mfumo huu na kwao tulienda kuomba ushauri tu,

“Hivyo tunaamini kila kitu kitakwenda sawa kwani hatujakiuka taratibu zozote za mfumo huu,” alieleza Try Again.

Advertisement

Simba ilianza mchakato wa mabadiliko kwa muda sasa, jambo ambalo halikuwa limekamilika kwa mujibu wa FCC, wakiwataka kurekebisha baadhi ya mambo kabla ya kuendele.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ alinukuliwa mara kadhaa akisema mchakato huo upo katika hatua nzuri kabla ya kauli yake ya mwisho juu ya suala hilo.

Mo alidai kuwa upande wao ulikuwa umekamilisha kila kitu, hivyio swali juu ya kukwama kwa mchakato huo linatakiwa kuelekezwa kwa FCC.

Lakini hivi karibuni, FCC ilitoa taarifa ya kushitua juu ya kutaka kuichunguza Simba juu ya mabadiliko waliyoanza kuyafanya katika uongozi.

Taarifa ya tume iliyotolewa wiki iliyopita ilidai kuwa mdaawa wa tatu kwa kushirikiana na mdaawa wa kwanza, pili na tano walichukua mali na biashara za mdaawa wanne Tanzania Bara bila kuitaarifa tume hiyo kinyume na sheria ya ushindani kifungu cha 11 (2), 11 (6) (cha mwaka 2018) na kizingiti cha muunganiko wa makampuni cha mwaka 2017.

Kwa upande wake, mwanasheria wa klabu ya Simba, Mhina Mhina alikiri kupokea taarifa hiyo kutoka FCC na kudai kuwa klabu hiyo itakaa na kutoa taarifa rasmi, lakini tayari Try Again amelimaliza jana.

Advertisement