Simba yaipiga Azam, Fei akosa penalti

Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wameendeleza moto wao wakiwa chini ya kaimu kocha mkuu, Juma Mgunda kufuatia kuibuka na ushindi wa tatu mfululizo katika mchezo wa vita ya nafasi dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mabao ya Saido Kanoute dakika ya 63,  Fabrice Ngoma dakika ya 77  na David Kameta 'Duchu' dakika ya 89, yametosha kwa vijana hao wa Mgunda kuvuna ponti tatu ambazo zinawafanya sasa wawe na matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Kabla ya mchezo huo, Simba ambayo ipo nafasi ya tatu ilikuwa nyuma ya Azam FC kwa tofauti ya pointi nne hivyo ushindi huo umewafanya kuwa na pointi 56 wapo nyuma kwa pointi moja tu huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Simba na Azam ni kama waligawana vipindi katika mchezo huo. Azam ilikuwa bora  katika kipindi cha kwanza kwa kufanya mashambulizi mfululizo kupitia maeneo yake ya pembeni ambako walicheza Gibril Sillah na Idd Seleman 'Nado'.

Wakati katika kiwango bora katika dakika ya 35, Azam ilipata penalti baada ya Sillah kuangushwa na Che Malone katika eneo la hatari hata hivyo, walishindwa kuitumia.

Mkwaju wa Feisal Salum Fei Toto uligonga nguzo na kuufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa suluhu kabla ya kibao kugeuka katika kipindi cha pili kwa vijana wa Mgunda kutandaza kandanda la kuvutia zaidi.

Katika kipindi hicho cha pili ubora wa eneo la kati la Simba uliibeba timu hiyo, Ngoma, Kanoute na Mzamiru walifanya kazi kubwa kwenye eneo hili.

Kipigo cha Azam kina maana kuwa Yanga imerahisishiwa kazi Simba katika mbio za ubingwa kwani kwa sasa wanahitaji pointi nne tu badala ya tano kutwaa ubingwa huo.


VIKOSI

Azam FC; Mohammed Mustafa, Nathaniel Chilambo, Pascal Msindo, Yannick Bangala, Yeison Fuentes, James Akaminko, Gibril Sillah, Yahya Zayd, Kipre Junior, Feisal Salum 'Fei Toto', Idd Seleman 'Nado'.