Simba yalaani Mangungu kufanyiwa vurugu Benjamin Mkapa
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Simba imeaga Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani na Esperance ya Tunisia.
Dar es Salaam. Uongozi wa Simba umelaani vitendo vya vurugu alivyofanyiwa Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Murtaza Mangungu baada ya kumalizika kwa mchezo baina yao na Esperance ya Tunisia, jana Jumapili, Februari Mosi, 2026 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mara baada ya mchezo huo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo walimvamia Mangungu wakati anatoka jukwaa kuu kuelekea katika gari lake lililokuwa limepakiwa katika maegesho ya Uwanja huo.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Bosi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori imeeleza kuwa klabu hiyo imelaani tukio hilo na kutaka wahusika wachukuliwe hatua.
“Bodi ya Wakurugenzi ya Simba imesikitishwa na vitendo vya baadhi ya watu kumvamia na kumfanyia fujo Mwenyekiti wa Klabu na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Murtaza Mangungu baada ya mchezo wetu dhidi ya Esperance de Tunis kumalizika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. “Vitendo hivyo sivyo vya kiungwana, havikubaliki na havitafumbiwa macho.
Uongozi wa Klabu unatoa pole kwa Mwenyekiti Mangungu kwa kadhia hiyo.
“Aidha Uongozi wa Klabu umeliandikia Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kisheria kwa wote waliohusika katika vurugu hizo au kula njama ili kuwafikisha katika Vyombo vya Sheria. Bodi inasisitiza kuwa haitabariki wala kuvumilia mtu yoyote atakayeharibu taswira ya Klabu kwa namna yoyote,” imesema taarifa hiyo ya Simba.
Sare hiyo ya mabao 2-2 ambayo Simba imepata jana, imeifanya iwe timu ya kwanza kuaga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ikiwa na pointi moja.
Hii ni mara ya pili kwa Simba kuishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2003.
Kundi lao D linaongozwa na Stade Malien yenye pointi nane ikifuatiwa na Esperance yenye pointi sita huku Petro Luanda ikiwa na pointi tano na Simba ina pointi moja.