Simba yamtumia straika mkataba

MEZANI kwa mabosi wa Simba kuna majina ya wachezaji wapya wanne kati ya hao watatu watasajili kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Januari 15, licha ya kubaki siku mbili kutokea leo, huku ikimtumia straika mkataba.
Taarifa kutoka ndani ya Simba ambazo Mwanaspoti imejiridhisha nazo kuna washambuliaji wawili wote ni raia wa DR Congo, Jean-Marc Makusu Mundele aliyekuwa mchezaji huru baada ya kuachwa na FC Lupopo Januari 7 mwaka huu ila kwa sasa yupo na kikosi cha timu ya taifa hilo kwenye mashindano ya CHAN.
Straika mwingine raia wa nchini hiyo, Jean Baleke mchezaji wa TP Mazembe ila yupo kwa mkopo Nejmeh SC, iliyopo kwenye nchi za falme za Kiarabu.
Majina mengine mawili ya mshambuliaji mmoja mzawa na kiungo mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya ukabaji na ushambuliaji aliyewahi kucheza Ligi Kuu ya Morocco, Simba imeendelea kuyaweka mafichoni ingawa Mwanaspoti linafahamu mchakato wa kuwanasa unaendelea.
Inaelezwa kama mambo yasipokwenda tofauti leo (jana), Simba ilimtumia mkataba Makus usiku ili asaini akiwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani baada pia ya mwenyewe kuomba ashiriki kwanza mashindano hayo ndiyo aje nchini.
Tayari Simba imekubaliana kila kitu na Makusu kwa maana hiyo ikimtumia huo mkataba atausaini kisha ataurudisha kwa njia ya mtandao kama ilivyofanywa na mabosi zake wapya na unaweza kuingia kwenye mfumo bila shida ingawa pia inaelezwa kama kutakuwa na kusuasua Simba wanaweza kutazama mshambuliaji mwingine haraka kwa kuwa muda hautoshi.
Simba imeamua kufanya hivyo, ili mkataba wa Makusu uweze kuingiza kwenye mfumo na kutambulika kama mchezaji mpya wa timu, kisha atawasili nchini kuitumikia timu hiyo.
Kama mambo yasipobadilika maana yake Makusu atakuwa mchezaji mpya wa Simba na atawasili hapa nchini baada ya CHAN, kumalizika mwanzoni mwa mwezi ujao kwani kwa sasa ni mchezaji huru tangu mkataba wake na FC Lupopo kuvunjwa.
Wakati huohuo, Mwanaspoti linafahamu straika mwingine Mkongomani Baleke juzi Jumanne mchana aliwasili Kinshasa DR Congo akisubiri tu tiketi ya ndege ili aweze kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha dili lake na Simba.
Inaelezwa Simba imekuwa ikihitaji kumnunua Baleke kutokea TP Mazembe ila tajiri wa timu hiyo, Moise Katumbi amegoma na kuwaeleza yupo tayari kuwapatia kwa mkopo si moja kwa moja.
Kulikuwa na mvutano Simba ilihitaji kumchukua moja kwa moja kwani inaogopa Baleke anaweza kufanya vizuri akarudi TP Mazembe na ikapata kazi ya kutafuta straika mwingine kwa wakati huo.
Alipotafutwa na Mwanaspoti Baleke alisema :"Nimewasili Kinshasa Jumanne kwa ajili ya mchakato wa suala langu la kusajili wa Simba kwani wenyewe kuninunua ila TP Mazembe inataka kunitoa kwa mkopo."
"Kama watakubaliana viongozi wa pande hizo mbili muda wowote kuanza wakati huu nitakuja huko Tanzania kwa ajili ya kujiunga na Simba ili kuanza kazi kwenye majukumu yangu mapya, ila binafsi nimewaeleza natamani mno kucheza Simba."
Kutokana na hali hiyo ilivyo straika mmoja wapo kati ya Makusu au Baleke muda wowote kabla ya dirisha la usajili kufungwa Januari 15, atambulishwa kama nyota mpya wa kikosi hicho.
Uongozi wa Simba unapambana kutafuta straika na kiungo kwani hayo ni mapendekezo ya kocha wao mpya, Robert Olveiera 'Robertinho' mara baada ya kuanza kazi ya kikinoa kikosi hicho na juzi alihakikishiwa na mabosi wa timu hiyo kuwa ataletewa mshambuliaji mpya kama alivyopendekeza.