Simba, Yanga zinavyokabana koo
Muktasari:
- Timu hizo kongwe katika soka la Bongo, mpaka sasa haijatokea kipindi cha kwanza zimeongoza kisha mwisho wa mchezo zikapoteza mechi.
Takwimu zinabainisha kwamba, Simba na Yanga ndiyo timu zilizofanya vizuri zaidi hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara. Hata ukiangalia msimamo wa ligi utakubaliana na hilo kutokana na namna nafasi wanazoshika zikitofautiana pointi moja pekee.
Msimamo wa ligi unaonyesha kinara kwa sasa ni Simba iliyokusanya pointi 25, ikifuatiwa na Yanga yenye 24, timu hizo zimecheza mechi 10. Chini yao kuna Singida Black Stars (23), Azam (21), kisha Fountain Gate na Tabora United ambazo zimekusanya pointi 17 kila moja. KenGold inaburuza mkia na pointi zake tano, juu yake kuna Pamba Jiji (8) na Kagera Sugar (8).
Waswahili wanasema biashara asubuhi, jioni mahesabu. Kutokana na takwimu za ligi hiyo baada ya kuchezwa mechi za raundi ya 11, Simba na Yanga zinakabana koo katika suala zima la kusaka matokeo mazuri ambapo rekodi zinaonyesha timu hizo zimefanya vizuri zaidi mechi zake sita kati ya kumi kulinganisha na zingine ndani ya ligi hiyo.
Katika mechi hizo sita, Simba na Yanga zimeonekana kukusanya pointi nyingi (18) zilizotokana na ushindi baada ya kuongoza kipindi cha kwanza, muda ambao makocha wengi wanakiangalia kipindi hicho na mwelekeo wa ushindi. Mbali na timu hizo, hakuna zingine zilizofanikiwa kupata ushindi mara nyingi kwa kuongoza kipindi cha kwanza.
Timu hizo kongwe katika soka la Bongo, mpaka sasa haijatokea kipindi cha kwanza zimeongoza kisha mwisho wa mchezo zikapoteza mechi.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Simba haijapoteza mechi ambayo kipindi cha kwanza iliongoza bali iliwatokea mara moja wameongoza kipindi cha kwanza dhidi ya Coastal Union (2-0), kisha mwisho wa mchezo matokeo yakawa sare ya 2-2.
Pia Simba ni mara moja imeshuhudiwa ikienda mapumziko matokeo yakiwa sare kisha kipindi cha pili ikapoteza. Ilikuwa dhidi ya Yanga ilipofungwa bao 1-0 dakika ya 86 ambapo Kelvin Kijili alijifunga.
Simba pia imewatokea mara mbili wakienda mapumziko matokeo yakiwa sare kisha ikashinda kipindi cha pili. Ilikuwa dhidi ya Mashujaa (1-0) na Dodoma Jiji (1-0).
Kwa upande wa Yanga, kati ya mechi kumi ilizocheza na sita kufanya vizuri zaidi kwa kuongoza kipindi cha kwanza na mwisho wa mchezo kupata ushindi, ni mara mbili pekee imetokea kwao kipindi cha kwanza sare, lakini wakaja kuondoka na ushindi kipindi cha pili. Hiyo ilikuwa dhidi ya Simba na Singida Black Stars ambapo mechi zote hizo ilishinda 1-0 kipindi cha pili. Mara zote ambazo Yanga imeongoza kipindi cha kwanza, haijapoteza wala kupata sare.
Lakini pia, Yanga katika mechi mbili tofauti wamejikuta wakiwa nyuma kipindi cha kwanza na kupoteza mchezo, ilikuwa dhidi ya Azam (1-0) na Tabora United (3-1) zote ikicheza uwanja wa nyumbani.
Ukiziweka kando Simba na Yanga, Azam inafuatia kwa kufanya vizuri zaidi kutokana na kuongoza kipindi cha kwanza mara tano na kuondoka na ushindi mwisho wa mchezo. Fountain Gate inafuatia kwa kufanya hivyo mara 4, huku Singida Black Stars, Tabora United, KMC na Mashujaa nazo zikifanya hivyo mara tatu kila moja.
Timu ambazo hazijafanikiwa kuongoza kipindi cha kwanza na kuondoka na ushindi mwisho wa mechi ni Tanzania Prisons na KenGold pekee ambazo hizo zote maskani yao jijini Mbeya zikiutumia Uwanja wa Sokoine kwa mechi zao za nyumbani.
KenGold pia inaongoza kwa kuwa timu iliyopoteza mechi nyingi (6) ambazo zote imemaliza kipindi cha kwanza ikiwa nyuma, huku jumla ikipoteza nane kati ya 11 ilizocheza hadi sasa.
Kwa sasa ligi imesimama kupisha mechi za kufuzu Afcon 2025 ambapo Timu ya Taifa ya Tanzania ina kibarua cha kucheza mechi mbili dhidi ya Ethiopia na Guinea.
Baada ya kumalizika kwa mechi hizo za kimataifa, Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuendelea Novemba 21 mwaka huu ikiwa ni raundi ya 12 kuelekea kumaliza mzunguko wa kwanza wenye raundi 15.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Almas Kasongo, amezungumzia namna ambavyo ligi inavyokwenda na ushindani unaoonyeshwa na timu shiriki 16.
“Ligi imekuwa na ushindani mkubwa kulinganisha na msimu uliopita, tulipofika hapa unaweza kuona timu zote angalau zimepoteza mechi moja. Kile ambacho Watanzania walikuwa wakikitarajia kukiona katika ligi yao ushindani ndio huu.
“Matarajio yetu ni kuona mzunguko wa pili ushindani utakuwa mkubwa hasa mwezi Machi, Aprili na Mei kwa sababu ndiyo kipindi ambacho timu zinapigia hesabu ubingwa, zingine hazitaki kushuka daraja wala kuwepo katika play off,” alisema Kasongo.