Kipingu atoboa siri ya Kaseja, Mgosi na msitu wa Lugalo
"Haikuwa rahisi kuwaingiza kwenye mfumo, wakati, walimu wangu waliniambia kwa hawa hapana," ndivyo anaanza kusimulia Kanali Mstaafu, Iddi Kipingu.
Kipingu ambaye ameacha historia kubwa si tu kwa wanamichezo wengi, pia waigizaji na wanamuziki katika sehemu ya pili ya mahojiano na gazeti hili ameeleza siri ambayo wengi hawaifahamu kuhusu mandhari ya msitu wa Lugalo, Dar es Salaam sanjari na nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Juma Kaseja na Mussa Hassan Mgosi.
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika wiki iliyopita nyumbani kwake, Makonde jijini Dar es Salaam, Kipingu ameeleza safari yake ya michezo hadi kuwa mkuu wa shule ya Sekondari Makongo.
"Wakati ule iliitwa Lugalo kabla haijabadilishwa jina kuitwa Makongo, mimi nilikuwa mwalimu msaidizi wa Michezo Shule ya Jitegemee na aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya shule Jenerali Mboma akawambia Jitegemee mimi niende Makongo,".
Kipingu ambaye aliongoza Makongo kwa miaka 12, tangu 1995 anasema alipoingia pale kulikuwa na wanafunzi 3500.
"Niliona sitaweza kuwa-meneji kama sitawapa kitu cha kufanya, wakati ule waziri wa elimu alikuwa profesa Phillimon Sarungi, alitutembelea shuleni, nikamwambia nataka kutengeneza bustani za timu ya taifa."
Anasema eneo lote lile lilikuwa na ukame mkubwa, hivyo mbali na kutaka shule iwe bustani ya timu za taifa, alianzisha mpango wa kupunguza ukame eneo la Lugalo.
"Shule ilichangia sana kutengeza mazingira yale, hata msitu wa Lugalo ile miti niliipanda mimi na wanafunzi wangu," anasema.
Anasema mbali na utunzaji mazingira, alitoa fursa kila mwanafunzi kuonyesha kipaji chake.
"Haikuwa kwenye michezo tu, hadi muziki na maigizo, ndipo kina Seki, Bambo, Daz Nundaz, Jose Mara, Kalala Junior wakaibuliwa, niliwakuta pale hadi kina Angela Damas.
"Baada ya kuwapa fursa kila mmoja akawa mfalme kwenye kipaji chake."
Akiwa na miaka miwili Makongo, Kipingu anasema ndipo aliwaibua Mussa Hassan Mgosi na Juma Kaseja.
"Ilikuwa kwenye Umitashumta (Mashindano ya Shule za Msingi Tanzania) ya 1997, ndipo niliwaona na kuwaleta Makongo.
"Walimu waliniambia sijawatendea haki, Kaseja akitoke timu ya Mkoa wa Kigoma na Mgosi Kilimanjaro, walikuwa wadogo, nikawaambia walimu wangu hawa ni wachezaji.
Anasema kwenye timu ya Kigoma, Kaseja alikuwa ni kipa namba tatu, hivyo akawa anaingizwa dakika chache chache.
"Timu yao iliingia fainali na Dar es Salaam, kipa namba moja wa Kigoma na namba mbili walikuwa wagonjwa, ikabidi Kaseja aanze, siku hiyo nilipata muda mzuri wa kumtazama.
"Hii ya kudaka penalti hakuanza leo, siku hiyo alidaka penalti mbili, Mgosi yeye alikuwa ana control sana ya mpira, alikuwa winga machachari wa timu ya Kilimanjaro, mashindano yalipokwisha nikawachukua kuwapeleka Makongo," anasema.
Anasema kuna mwalimu alimpa jukumu baada ya mazoezi ya timu, wao walikuwa na nusu saa zaidi ya mazoezi binafsi hadi wakawa mastaa.
Wachezaji wengine baadhi waliopitia mikononi mwa Kipingu, ni Haruna Moshi Boban ambaye anasema alimpeleka Makongo akiwa kidato cha pili.
"Hata Awadh huyu kocha wa Mtibwa alipitia kwangu, kwa kweli wale niliowa-pick wote walikuja kuwa tishio kwenye timu za taifa.
"Kina Boniface Pawasa, hata Nicodemus Njohole na Ally Mayay niliwahamishia Makongo wakitokea Tabora, walipohitimu kidato cha nne na kwa kuwa kwenye Umisseta tulihiwahitaji, ndipo nikawapeleka Jitegemee.
"Kidau (Wilfred ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania) naye alikuja alikuwa anajua mpira, sio kwenye soka hata wanariadha na wachezaji kikapu.
"Huyu Hasheem Thabeet, nilikwenda kutizama mechi ya UDSM Outsider, nikaona jitu refu linazunguka zunguka, lakini hachezi, nikamuuliza kama anasoma akasema ndio shule moja ya Sinza, nikamwambia kesho njoo Makongo.
Anasema alipokwenda alimueleza kuhamia Makongo, akamwambia anakwenda kwanza kuzungumza na mama yake ambaye alikubali na kijana wake huyo akahamia shuleni hapo akiwa kidato cha pili.
"Wakati yupo kidato cha nne, kulikuwa na mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya Sekondari, nikaomba shule yetu ishiriki kwa kuwa Tanzania hatukuwa tunashiriki kama nchi, nilikubaliwa na kwenye timu ya kikapu ya wachezaji 13, kocha hakunjumuisha Hasheem.
"Si kama alimuonea, katika wale 13 waliochaguliwa hakuwa na uwezo wa kushindana, ila nikamshauri kocha amchukue kwa faida ya kuwatisha wapinzani
Anasema kwenye mashindano hayo yaliyofanyika Kenya, Hasheem alipewa dakika 10 za kucheza na moja ya shule nchini humo ikampenda.
"Waliniandikia barua, nikawambia lazima wamgharamia akiwa huko na nauli yake wakati wa likizo, walikubali ndipo akaenda kuanza maisha mapya kule hadi anafika levo ya kucheza NBA (Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani).