Simba yatua Bukoba, akili yote kulipa kisasi kwa Kagera Sugar

Muktasari:

  • Mastaa wa Simba hawataki kuendelea na rekodi ya kufungwa na Kagera Sugar kama ilivyokuwa msimu uliopita kufungwa nyumbani na ugenini.

Dar es Salaam.Kikosi cha Simba kimewasili Kagera asubuhi na wachezaji wake wameapa kuvunja mwiko wa kufungwa na Kagera Sugar katika mechi yao ya kesho itakayopigwa Uwanja wa Kaitaba.

Simba imewasili kwenye uwanja wa Ndege mjini Bukoba leo tayari kwa mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 msimu uliopita kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Akizungumzia mchezo huo beki wa Simba, Haruna Shamte amejiunga na mabingwa hao msimu huu akitokea Lipuli ya Iringa amesema wanataka kufuta rekodi yao mbaya kwa Kagera Sugar.

Shamte alisema mpinzani wao anapojiamini kupitiliza kwao ni faida kujituma na kupata matokeo akisisitiza kwamba licha ya kuheshimu uwezo wa Kagera Sugar hautawazuia malengo yao.

"Timu ambazo zinakaa na wachezaji kwa muda mrefu ni nzuri kwani wanakuwa wanajuana kama ilivyokuwa kwa Kagera Sugar, lakini kwa sasa kikosi chao kimebadilika."

"Tunajua siyo mechi ya kupata mtelemko ndio maana tumefanya mazoezi ya nguvu kuhakikisha tunakuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo, mechi itakuwa ngumu ila tutapambana," alisema Shamte.

Naye kiungo Jonas Mkude alisema kwa ufupi mechi hiyo kwamba dakika 90 ndio mwamuzi wa mchezo huo na kwamba ya msimu uliopita hayana nafasi kwao.

"Mchezaji yoyote anapocheza akili yake unakuwa inawaza ushindi tunaangalia mechi ya kesho na sio nini kilitokea msimu ulioisha hapo tutakuwa hatufiki kwenye malengo yetu"alisema.

Wakati mastaa wa Simba wanawaza kuvunja mwiko kwa upande wa beki wa Kagera Sugar, David Luhende alisema mchezo wa kesho utawashangaza wengi.

"Simba wanafungwa kwa sababu saikolojia zao zinakuwa zinatuwazia tofauti hilo halitufanyi tuone mchezo rahisi, Kuna wachezaji wapo vizuri kiufundi ila tutapambana nao," alisema Luhende.