Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simbu azindua kampeni ya kuibua mabingwa wapya wa riadha

Mwanariadha, Alphonce Simbu (wa kwanza kulia) akizungumza wakati wa Alphonce Simbu Foundation jijini Arusha.

Arusha. Akiwa ameendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania katika majukwaa makubwa ya riadha duniani, bingwa wa marathon, Alphonce Simbu, ameanzisha kampeni ya “Kimbia na Simbu” yenye lengo la kukusanya zaidi ya Sh600 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha michezo kitakachotumika kuibua na kukuza vipaji vya wanariadha chipukizi, sambamba na kumuandaa kwa mashindano makubwa ya kimataifa yanayokuja.

Kampeni hiyo ilizinduliwa jana Juni 10, 2026 jijini Arusha kupitia Alphonce Simbu Foundation na imeungwa mkono na viongozi wa riadha, wadau wa michezo pamoja na sekta binafsi, ikiwemo ya utalii.

Uzinduzi huo unafanyika wakati Simbu akiendelea kung’ara katika riadha ya dunia baada ya kuwa mwanariadha wa kwanza kutoka Tanzania kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya marathon mwaka 2025 jijini Tokyo, Japan.

Mbali na ubingwa huo, Simbu ameendelea kuonyesha ubora wake katika mbio za masafa marefu baada ya kumaliza katika nafasi za juu kwenye mashindano ya Boston Marathon kwa miaka miwili mfululizo, hatua iliyomuweka miongoni mwa wanariadha wanaoheshimika duniani.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Ntua Communications Ltd, Moses Ntua, alisema kampeni hiyo imeanzishwa kutokana na mafanikio makubwa ya Simbu pamoja na umuhimu wa kuhakikisha anapata maandalizi bora kuelekea mashindano yajayo.

Alisema Simbu ameendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuwa chanzo cha hamasa kwa vijana wengi wanaotamani kufanikiwa katika riadha.

“Tunataka Watanzania wote wawe sehemu ya safari hii. Kila mchango una thamani kubwa katika kufanikisha malengo ya Simbu na maendeleo ya riadha nchini. Kauli mbiu yetu ni ‘Kila Hatua ni Ushindi’,” alisema Ntua.

Kwa mujibu wa waandaaji, fedha zitakazokusanywa kupitia kampeni hiyo zitatumika kujenga kituo cha kisasa cha michezo katika eneo la Ngateu, Arusha.

Kituo hicho kinatarajiwa kuwa kitovu cha mafunzo, makazi na maendeleo ya wanariadha chipukizi kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Ntua alisema kampeni hiyo pia itahusisha matukio mbalimbali ya kukimbia na Simbu katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam, yatakayowapa mashabiki na wanachama wa klabu za mazoezi fursa ya kushiriki mbio pamoja na mwanariadha huyo.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Alfredo Shahanga, alisema kampeni hiyo imekuja wakati muafaka kwa kuwa itasaidia si tu maandalizi ya Simbu bali pia maendeleo ya muda mrefu ya riadha nchini.

“Tanzania inahitaji kuwekeza zaidi katika vijana wenye vipaji ili kuhakikisha mafanikio tunayoyaona leo yanaendelea hata baada ya wanariadha wa kizazi cha sasa kumaliza ushindani. Tunamuunga mkono Simbu kwa asilimia 100. Kituo hiki kitasaidia kuibua vipaji vipya na kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na wanariadha wa kiwango cha dunia,” alisema Shahanga.

Naye Mkurugenzi wa Kilifair Promotion Company Limited, Dominic Shoo, alisema sekta binafsi imeanza kutambua umuhimu wa kuwekeza kwa wanamichezo wanaolitangaza taifa kimataifa.

“Alphonce Simbu si mwanariadha tu, bali ni balozi wa Tanzania. Kila anaposhiriki mashindano nje ya nchi anaitangaza Tanzania na vivutio vyetu vya utalii. Ndiyo maana tumeamua kumuunga mkono katika safari hii,” alisema Shoo.

Kwa upande wake, mwanariadha nyota wa Tanzania, Gabriel Geay, alisema kampeni hiyo ni mfano bora wa namna wanamichezo wanavyoweza kutumia mafanikio yao kusaidia kizazi kijacho.

Geay alisema mafanikio ya Simbu yamefungua milango kwa wanariadha wengi wa Tanzania kupata kutambulika kimataifa, hivyo juhudi zake za kuwekeza katika maendeleo ya vipaji zinastahili kuungwa mkono.

Akizungumza kwa hisia, Simbu alisema lengo la kampeni hiyo si kuongeza mafanikio yake binafsi pekee, bali kuhakikisha Tanzania inaendelea kuzalisha wanariadha wa kiwango cha juu kwa miaka mingi ijayo.

Alisema yeye na wanariadha wenzake wamekuwa wakitafakari namna ya kuandaa kizazi kitakachokuja baada yao ili kuepusha pengo la uwakilishi wa Tanzania katika mashindano makubwa ya kimataifa.

“Tunaposhinda medali na kuiwakilisha Tanzania, tunawaza pia nani atakuja kuchukua nafasi zetu baadaye. Kulikuwa na kipindi taifa halikuwa na wawakilishi wengi katika mashindano makubwa ya kimataifa. Hatutaki hali hiyo ijirudie,” alisema Simbu.

Alisema kupitia Alphonce Simbu Foundation tayari wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kutambua vipaji vya vijana, hususan maeneo ya vijijini, lakini changamoto imekuwa ukosefu wa miundombinu bora ya mazoezi.

“Tumegundua kuna vipaji vingi sana. Ndiyo maana tunataka kujenga kituo hiki kitakachokuwa kama sports centre kwa ajili ya vijana wenye vipaji vya riadha,” alisema.

Simbu aliwataka Watanzania, mashabiki wa michezo, taasisi na wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono kampeni hiyo ili kufanikisha ndoto ya kujenga kituo hicho na kuendelea kuiweka Tanzania kwenye ramani ya riadha duniani.

“Ndoto yangu ni kuona vijana wengi zaidi wakipata nafasi ya kufikia mafanikio makubwa kuliko hata tuliyoyapata sisi. Huo ndiyo ushindi mkubwa zaidi,” alisema Simbu.