Sowah aipa jeuri Simba, watoa onyo
Muktasari:
- Sowah alimaliza katika nafasi ya Pili katika chati ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu msimu uliopita akifunga mabao 13.
Dar es Salaam. Baada ya Simba kunasa saini ya Jonathan Sowah kutoka Singida Black Stars, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally amewapa tahadhari wapinzani wao mapema, huku mshambuliaji huyo akifunguka mipango yake ndani ya Wekundu wa Msimbazi.
Mghana huyo ambaye alitua Singida Black Stars katika dirisha dogo la usajili akitokea Al Nasr ya Libya, alimaliza msimu wa 2024/2025 akiwa na mabao 13 akipishana matatu na mfungaji bora kJean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga mabao 16.
Ahmed Ally amesema, miongoni mwa timu kubwa hapa Afrika, Simba ni miongoni mwao ndio maana wanapata heshima hata ya kudhaminiwa na makampuni makubwa kutoka nje ya nchi.
"Simba mnaweza kuiona tu ni timu ya kawaida kwa sababu mmeizoea lakini kwenye ramani ya soka sisi tuko juu na tunaweza kununua kitu chenye thamani yoyote kutokana na utajiri tulionao.
Amshukuru Mwigulu kwa Sowah
Ahmed amesema kuwa kama watampata Sowah litakuwa ni jambo jema na atamshukuru Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ambaye ni mlezi wa Singida Black Stars.
“Sina taarifa rasmi kama ni kweli ni mchezaji wetu mpaka pale nitakapopewa habari na viongozi wangu na kama itakuwa hivyo basi namshukuru mlezi wa klabu hiyo Mwigulu Nchemba kwa kutupa mchezaji bora sana.
"Wanaozungumza kwamba sisi tumepewa mchezaji bure hawaelewi. 2018 walipewa Feisal Salum, Duke Abuya, Nickson Kibabage na Israel Mwenda pia walipewa bure, kwa hiyo nani mtaalamu hapo wa kuomba?” amehoji Ahmed.
Awapa dongo wapinzani
Ahmed alisema sababu zinazowatesa wapinzani wao ni mbili.
"Kwanza ni wivu. Wanaogopa kwa sababu Sowah ni mchezaji hatari ni mashine kweli kweli, hakuna staa anayemfikia katika ligi kwa miaka ya hivi karibuni. Wapo tulioanza nao msimu na hawajafikia rekodi yake, wanawaza kama Singida alifunga vile je, huku itakuaje?
"Sababu ya pili ni uonga, kwamba sisi tunakata mfereji wa kuchukua wachezaji Singida sasa kumuona Simba kavamia kichaka chao inawapa shida. Pia wanahisi ushindani wa kugombea mastaa utazidi kuongezeka na wanajua kwenye ushindani lazima tushinde kumpata,” amesema Ally.
Aliongeza kuwa,” wachezaji ambao wao wanawachukua hawakuwa vipaumbele vya Simba na wanachoweza ni kuchukua mastaa ambao sisi tumewaacha."
Sowah atamba
Kwa upande wake Sowah amesema kuwa Ame hips ha kuisaidia Simba.
Amesema akili yake imetulia na anapojiunga na Simba ana hesabu nyingi lakini kubwa ni kupata mafanikio ndani ya timu hiyo.
"Nataka kuisaidia Simba kurudisha heshima yake na kuhakikisha inapata mafanikio binafsi kwa kuwa mfungaji bora. Nitajituma katika nafasi yangu kupata mabao mengi kwa kuwa najiunga na timu yenye viungo wengi wazuri,” amesema Sowah.
Sowah anakwenda kucheza nafasi moja na Steven Mukwala na Leonal Ateba ambao walianza na kikosi cha Simba msimu uliopita,huku wote wakipewa nafasi kwa vipindi tofauti tofauti na kocha Fadlu Davids.
REKODI ZAO
Steven Mukwala
Mechi:26
Dakika:1094
Mabao:13
Asisti:03
Leonel Ateba
Mechi:24
Dakika:1,497
Mabao:13
Asisti:04