Spika Ndugai awaita mashabiki kwa Mkapa

Spika Ndugai awaita mashabiki kwa Mkapa

Muktasari:

  • Spika Job Ndugai amewaita Watanzania kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa Septemba 19, 2021 ili kuishangilia Timu ya Simba ya itakapomenyana na timu ngumu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Dodoma. Spika Job Ndugai amewaita Watanzania kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa Septemba 19, 2021 ili kuishangilia Timu ya Simba ya itakapomenyana na timu ngumu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya hoja ya kuahirisha bunge iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambapo amewatakia ushindi timu zinazotarajia kucheza michezo ya Kimataifa kutoka Tanzania mwisho mwa wiki hii.

Simba itakuwa na tamasha la Simba Day ikiwa na lengo la kuwatambulisha wachezaji wake wapya na shughuli mbalimbali ambazo Simba watazifanya.

“Nataka kuwaambia kuwa Spika wenu nitakuwepo siku hiyo, kuna mambo makubwa ambayo tutayafanya siku hiyo njooni muone uhondo maana wale wengine walitusumbua pale alipokuwa Makamu wa Pili wa Rais, tutaonyesha mambo yetu,” amesema Spika Ndugai.

Kiongozi huyo amesema Simba ni moja ya timu ambazo zinaonyesha kandanda lenye mvuto kwa hiyo anaamini kuwa watu watafurahi siku hiyo bila kuwa na shaka ukilinganisha na mechi zilizochezwa na timu zingine.

Awali Waziri Mkuu amezungumzia furaha yake na Watanzania kwa timu ya Taifa na mabondia wa Tanzania kutokana na ushindi walioonyesha hivi karibuni huku akisifia uwekezaji katika timu za Simba, Azam na Yanga kuwa unaleta mafanikio ya kulipeleka mbele soka la nchi hii.

Kwenye hoja ya kuahirisha bunge, Majaliwa amemtaja Rais Samia Suluhu Hassan kwamba amekuwa mfano mwema wa kuigwa katika mipango yake ya uwekezaji wa michezo kwa timu za wanawake akitaka watu wengine kumuunga mkono.