Stand United yanasa kifaa cha Burundi

Muktasari:

Timu hiyo ya mkoani Shinyanga ilionyesha ushindani na kufika nusu fainali ya Kombe la FA licha ya kumaliza nafasi ya 11 kwa pointi 32 kwenye Ligi Kuu msimu uliopita.

Mwanza. Klabu ya Stand United imepania kufanya vyema katika Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kunasa saini za wachezaji wawili wapya akiwemo raia wa Burundi.

Timu hiyo ya mkoani Shinyanga ilionyesha ushindani na kufika nusu fainali ya Kombe la FA licha ya kumaliza nafasi ya 11 kwa pointi 32 kwenye Ligi Kuu msimu uliopita.

Akizungumza mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Stand United Elyson Maheja alimtaja mshambuliaji Mrundi Alex Kitenge, ametia saini mkataba wa miaka miwili kutoka klabu ya Lydia.

Pia Stand United imenasa saini ya kiungo Hafith Mussa ambaye pia alikuwa mchezaji wa Lydia ingawa ni raia wa Tanzania.

Alisema katika kuimarisha kikosi hicho klabu hiyo imeongeza mkataba kwa kipa Mohammed Makaka na beki Erick Murilo ambao wamejifunga mwaka mmoja kila mmoja.

“Tuna amini ni vijana wazuri ambao watakuwa na mchango mkubwa katika kikosi chetu,”alisema Maheja.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa malengo yao msimu ujao ni kufanya vizuri na wamejipanga vyema kurekebisha kasoro zilizojitokeza msimu uliopita.

Mwenyekiti huyo alisema wanaendelea na mchakato wa kufanya usajili lengo ni kupata kikosi kipana ambacho kitatoa ushindani katika Ligi Kuu msimu ujao.

Ratiba ya awali ya Ligi Kuu inatarajiwa kutangazwa wiki hii na itajumuisha timu 20 msimu ujao baada ya klabu sita kupanda daraja.

Klabu zilizopanda Ligi Kuu ni JKT Tanzania, KMC, African Lyon, Alliance Mwanza, Biashara United (Mara) na Coastal Union ya Tanga.