Stand Utd, Yanga warushiana makonde

Muktasari:

  • Mbali na kurushiana makonde, makomandoo hao walimiminiana mvua ya mawe hatua iliyohatarisha maisha ya wachezaji wa timu hizo kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.

Huwezi amini, hata kabla ya mchezo leo, makomandoo wa Stand United na Yanga, wamezitwanga kavukavu.

Mbali na kurushiana makonde, makomandoo hao walimiminiana mvua ya mawe hatua iliyohatarisha maisha ya wachezaji wa timu hizo kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.

Tukio hilo lilitoa jana asubuhi zikiwa zimebaki saa chache kabla ya Stand United na Yanga kuteremka uwanjani kuwania pointi tatu muhimu katika mchezo wa Ligi Kuu.

Tukio lenyewe lilianza hivi, wakati timu ya Yanga inaingia uwanjani kufanya mazoezi ya asubuhi wachezaji wa Stand United walikuwa wakiendelea kujifua.

Kimsingi Yanga ndiyo ilikuwa na haki ya kufanya mazoezi kwenye uwanja huo kwa mujibu wa kanuni za soka kwa timu mwenyeji kupisha wageni kujifua siku moja kabla ya mchezo.

Mbali na Stand United kufanya mazoezi, lakini makomandoo wa klabu hiyo waliweka ulinzi mkali kuanzia juzi jioni kwa kile kinachodaiwa kuogopa ‘ndumba’ kutoka kwa wapinzani wao.

Baada ya Yanga kuwasili uwanjani ikiwa na mashabiki, makomandoo wake waliwataka wenyeji wao kutoka nje ili kuwapa fursa ya kufanya mazoezi kitendo ambacho kilipingwa vikali na wenyeji wao.

Baada ya mabishano ya dakika takribani tatu vurugu ilianza makomandoo wa Yanga waliamua kutumia ubabe na kufanikiwa kuwatoa wenzao wa Stand, lakini baadhi yao walibaki ndani ya uwanja na muda mfupi baadaye mvua ya mawe ilianza.

Kocha wa Yanga George Lwandamina, alilazimika kusitisha kwa muda mazoezi akihofia wachezaji wake kuumia kabla ya polisi kufika eneo la tukio na kuwakamata baadhi ya mashabiki wa Stand United na kuwapeleka kituoni.

Baada ya vurugu kutulia Yanga ilifanya mazoezi vyema na iliondoka kwa usalama uwanjani hapo ingawa tukio hilo limekuwa gumzo kwa mashabiki wa soka mkoani hapa.

Mchezo wa leo unavuta hisia za mashabiki wa soka nchini kutokana na tambo za klabu zote mbili kwa kila moja ikijinasibu kupata ushindi dhidi ya mpinzani wake.