Stars yainyoosha Malawi kwa Mkapa, Kibu balaa

KWENYE uwanja wa Benjamin Mkapa, mchezo wa Kirafiki wa kimataifa kati ya Tanzania 'Taifa Stars’ na Malawi umemalizika kwa Stars kuibuka na ushindi wa bao 2-0.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu zote kwenda mapumziko bila kupata bao (0-0).

Kipindi cha pili kilianza kwa Stars kufanya mabadiko manne kwa kuwatoa Shomari Kapombe, Yusuph Mhilu, Nickson Kibabage na Mudathir Yahya ambao namba zao zimechukuliwa na Israel Mwenda, Abdul Suleiman, Ayoub Lyanga na Mzamiru Yassin mabadiliko yaliyoongeza kasi ya Stars.

Dakika ya 53, Malawi nao walifanya mabadiliko kwa kumtoa Myaba Ike na nafasi yake kuchukuliwa na Chester Yamikani.

Feisal Salum alioneshwa kadi ya njano dakika ya 58 baada ya kumchezea faulo moja ya washambuliaji wa Malawi nje ya boksi la 18, alipokuwa akijaribu kupenya.

Dakika moja baadae Stars walifanya mabadiliko tena kwa kumtoa kiungo Salum Abubakar na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Kibu Denis ambaye alibadilisha kasi ya eneo la mashambulizi.

Lyanga dakika ya 65 kidogo aipatie Stars bao la kuongoza baada ya kupiga kiki kali langoni kwa Malawi akipokea pasi kutoka kwa John Bocco na mpira kupanguliwa na kipa wa Malawi Munthali Brighton.

Dakika ya 68, Stars ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Bocco aliyemalizia pasi safi ya Kibu aliyopiga baada ya kuwatoka mabeki wa Malawi na kufanya ubao wa matangazo usomeke 1-0.

Baada ya bao hilo, Stars walifanya mabadiliko mengine kwenye eneo la ulinzi kwa kumtoa Erasto Nyoni na nafasi yake kuingia Kennedy Juma.

Israel Mwenda dakika ya 75 aliipatia Stars bao la pili kwa mpira wa faulo alioupiga baada ya Kibu kuangushwa nje ya boksi la 18 na kuzama moja kwa moja wavuni kwa kwa Malawi.

Malawi walifanya mabadiliko dakika ya 82 kwa  Chimodzi Tawonga na Nyangulu Vicent waliingia kuchukua nafasi za Mhango Hellings na Namweda Rafiki mabadiliko ambayo hayakubadili matokeo.

Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika Tanzania 2-0 Malawi.