Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sura mbili za machozi ya Ochoa akiaga Mexico

Ni Jumatano saa 3 kasoro usiku kwa muda wa Mexico sawa na Alhamisi saa 12 kasoro asubuhi kwa muda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mashabiki 80,824 waliojitokeza katika Uwanja wa Azteca jijini Mexico City, Mexico kutazama mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Dunia ambao wenyeji wameibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Jamhuri ya Czech, wanasimama na kupiga makofi huku macho yote yakiwa uwanjani.

Timu ya Taifa ya Mexico ilikuwa imejihakikishia kutinga hatua ya 32 ikiwa kinara wa kundi A lakini makofi hayo ya umati wa mashabiki waliojitokeza katika Uwanja huo hayakuwa kwa ajili ya hilo bali kwa kipa mkongwe wa Mexico, Guillermo Ochoa.

Wachezaji wa Mexico wakifurahia na kipa wao mkongwe, Guillermo Ochoa baada ya mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Czech wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Ilikuwa ni heshima maalum kwa Ochoa ambaye alitumia mchezo huo dhidi ya Jamhuri ya Czech ambao aliingia uwanjani katika dakika ya 78, kuchukua nafasi ya Raul Ranger, kwa ajili ya kuaga rasmi mashabiki wa soka nchini humo na duniani kiujumla kwa vile atastaafu rasmi soka la ushindani baada ya kumalizika kwa Fainali za Kombe la Dunia.

Tukio hilo la mashabiki linamfanya Ochoa amwage machozi huku akiwashukuru mashabiki kwa heshima waliyompa.

Mexico itacheza tena uwanjani hapo katika mechi ya hatua ya 32 bora lakini kuna uwezekano finyu kwa Ochoa kucheza kwa vile sio kipa namba moja wa timu hiyo.

Kwa Ochoa machozi hayo yanamaanisha mambo mawili.


Huzuni ya kuachana na soka

Pengine asingeamua kuwa mwanasoka, Ochoa asingeweza kuwa mtu maarufu duniani leo hii lakini imekuwa kinyume.

Imempa umaarufu, heshima, fedha na marafiki nje na ndani ya Mexico.

Kipa mkongwe wa Mexico, Guillermo Ochoa. Picha na Mtandao

Dunia imemfahamu kupitia soka hasa akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Mexico kwenye fainali za Kombe la Dunia ambazo ameshiriki kwa awamu sita tofauti kuanzia 2006.


Heshima ya kuagwa nyumbani

Uwanja wa Azteca umebeba historia kubwa kwa Ochoa mwenye umri wa miaka 40.

Mahali hapo ndipo alipoanzia rasmi kucheza soka la ushindani kwani ndipo alipocheza mechi yake ya kwanza ya kulipwa akiwa na Club America mwaka 2004.

“Mechi yangu ya kwanza Azteca. Mechi yangu ya mwisho Azteca. Imekuwa ni ukurasa wangu wa mwisho mzuri wa kazi yangu. Asante kwa kila mmoja,” amesema Ochoa baada ya mechi hiyo.


Hana deni Mexico

Ochoa anaondoka akiwa ameweka rekodi ya kuwa miongoni mwa wachezaji watatu walioshiriki fainali sita tofauti za Kombe la Dunia.

Kipa wa Mexico, Guillermo Ochoa akiwa na familia yake uwajani baada ya mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Czech wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Amecheza idadi ya mechi 154 za timu ya taifa ya Mexico na kati ya hizo, hajaruhusu bao katika michezo 64.

Katika miaka yake 22 aliyocheza soka la kulipwa, amezitumikia klabu tisa tofauti na sasa anaitumikia AEL Limassol ya Cyprus.

“Ni mfano bora kwetu. Amekuwa wa kwanza kuingia gym na wa mwisho kutoka,” amesema nyota wa Mexico, Mateo Chavez.