Tanzania yang’aa tuzo CAF, Rais Samia, Mzize wakitwaa
Muktasari:
- Mchezaji Bora Afrika Mwaka 2025 kwa Wanaume ni Achraf Hakimi na kwa Wanawake ni Ghizlane Chebbak wote wakiwa ni raia wa Morocco.
Tanzania imepata tuzo mbili katika Hafla ya Tuzo za Mwaka za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambayo imefanyika leo, Jumatano, Novemba 19, 2025, Rabat, Morocco.
Tuzo ya kwanza imeenda kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imetolewa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya soka nchini.
Motsepe pia amewapa tuzo hiyo, Rais wa Uganda, Yoweri Museven na Rais wa Kenya, William Ruto.
Kwa niaba ya Rais Samia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokea tuzo hiyo na kusema kuwa serikali ya Tanzania inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano na CAF na FIFA katika kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua.
Tuzo nyingine imeenda kwa nyota wa Yanga, Clement Mzize ambaye ameshinda tuzo ya Goli Bora la Mwaka.
Goli hilo ni lile alilofunga dhidi ya TP Mazembe katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Januari 4 mwaka huu ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Tuzo kubwa ambayo ilifunga tukio lenyewe ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2025 Afrika ilienda kwa nyota wa Morocco anayeichezea PSG, Achraf Hakimi.
Hakimi ameshinda tuzo hiyo akiwapiku Mohamed Salah (Liverpool/Misri) na Victor Osimhen (Galatasaray/Nigeria).
Nyota wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa anachezea Pyramids FC, Fiston Mayele ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ndani ya Afrika.
Pyramids FC imeshinda Tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka kwa Wanaume huku timu ya Taifa ya vijana ya Morocco chini ya Umri wa miaka 20 ikishinda tuzo ya Timu bora ya Taifa ya Wanaume.
Orodha ya Washindi wengine
Timu Bora ya Taifa Wanawake- Nigeria
Kipa Bora Wanaume
-Yassine Bonou (Morocco)
Kipa Bora Wanawake
-Chiamaka Nnadozie (Nigeria)
Mchezaji Bora Mdogo Wanawake
-Doha El Madani (Morocco)
Mchezaji Bora Mdogo Wanaume
-Othmane Maamma (Morocco)
Kocha Bora wa Mwaka Wanaume
-Bubista
Refa Bora Wanaume
-Omar Artan (Somalia)
Refa Bora Wanawake
-Shamirah Nabaddah