Tanzania yashuka FIFA

Muktasari:

  • Kidunia vinara ni Brazil wakifuatiwa na Ubelgiji, Argentina, nafasi ya nne wako Ufaransa na inayoshika nafasi ya tano ni England

Tanzania imeanguka kwa nafasi moja katika viwango vya ubora wa soka vilivyotolewa leo Juni 23 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Kutofanya vizuri kwa Taifa Stars katika mechi mbili za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 dhidi ya Niger na Algeria kunaonekana kuiponza Tanzania ikijikuta imeanguka kutoka nafasi ya 130 hadi ya 131.

Anguko kwenye viwango hivyo vya ubora halijaikuta Tanzania pekee bali hata nchi jirani zikiwemo zile ambazo ni wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Uganda licha ya kuendelea kuongoza kwa upande wa nchi zilizo chini ya Cecafa, imeporomoka kwa nafasi nne, kutoka ile ya 86 ambayo walikuwepo katika orodha ya mwisho iliyotolewa Machi hadi nafasi ya 90.

Kama ilivyo kwa Uganda, majirani wengine wa Tanzania ambao wameporomoka katika viwango hivyo vya ubora ni Malawi, Zambia na Burundi.

Maajabu ya viwango hivyo ni Kenya ambayo licha ya timu yao ya taifa 'Harambee Stars' kutocheza mechi yoyote ya kimataifa hivi karibuni baada ya kufungiwa na FIFA, wamepanda kwa nafasi mbili kutoka ya 104 hadi ya 102.

Senegal wameendelea kuongoza kwa upande wa Afrika wakifuatiwa na Morocco, Tunisia, Nigeria na Cameroon.

Kidunia vinara ni Brazil wakifuatiwa na Ubelgiji, Argentina, nafasi ya nne wako Ufaransa na inayoshika nafasi ya tano ni England