TFF ya Karia hatari tupu

Tuesday April 13 2021
karia pic
By Mwanahiba Richard

WAKATI Serikali ikitoa siku nne za kukaa na kumaliza tofauti kati ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) na klabu ya Yanga ambazo zinamalizika leo Jumatatu, moto pia uliwaka bungeni ukilalamikia sheria zinazotumika na shirikisho hilo kutoa adhabu kwa wadau wao.

Hivi karibu Kamati ya Maadili ya TFF lilimfungia kujihusisha na soka Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela kwa miaka mitano pamoja na kulipa faini ya Sh 5 milioni.

Makosa yaliyosababisha Mwakalebela kuingia kwenye jela hiyo ya soka ni baada ya kudaiwa kutoa maneno ya uchochezi kwa nia ya kuchochea washabiki, wanachama na wapenzi wa Yanga dhidi ya vyombo vinavyosimamia mpira wa miguu nchini.

Februari 19 mwaka huu, Mwakalebela aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kudai kuwa TFF, Bodi ya Ligi Kuu Tazania Bara (TPLB) na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa ligi hiyo zinaihujumu Yanga, madai ambayo ilidaiwa alishindwa kuthibitisha mbele ya kamati.

Mwakalebela alilalamikiwa kwa kutoa taarifa za uongo ambapo Oktoba 1, 2020 aliitisha mkutano na kudai kuwa anao mkataba kati ya mchezaji Bernard Morrison na Simba na kuuonyesha kwa waandishi wa habari huku akijua ni uongo na kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Kamati hiyo ilimtia hatiani katika shtaka hilo na kumpa onyo la kutotenda kosa hilo tena kwa muda wa miaka mitano sambamba na kutozwa faini ya Sh 2 milioni, adhabu hizo ni kwa mujibu wa kifungu cha 6(1) (b) na 6(1) (c) cha kanuni za TFF toleo la 2013.

Advertisement

Adhabu ya Mwakalebela imeonekana kuwagusa wengi ikidaiwa kwamba ni adhabu kubwa ukilinganisha na kosa lake huku suala hilo likienda mbali zaidi hadi bungeni ambako lilielezwa kuwa TFF inatoa adhabu kubwa kuliko hata adhabu za kesi za ubakaji.

Mbunge wa Kasuku vijijini Agustino Holle alionyesha kukerwa na adhabu hizo na kuiomba Serikali kuliangalia suala hilo hasa kwenye sheria za TFF kwani adhabu wanazotoa kwa wadau wao ni kubwa mno ambapo hurudisha nyuma maendeleo ya mchezo husika.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wadau wa TFF ambao wamefungiwa maisha ama miaka kadhaa na shirikisho hilo ambalo mwaka huu viongozi wake wanamaliza miaka minne ya kukaa madarakani.


MICHAEL WAMBURA

MACHI 2018, Wambura alifungiwa kujihusisha na masuala ya soka katika maisha yake yote na Kamati ya Maadili ya TFF.

Wambura alishitakiwa kwenye kamati hiyo kutokana na makosa matatu, kupokea/kuchukua fedha za shirikisho za malipo ambayo hayakuwa halali kutoka Chama cha Miguu Tanzania (FAT na baadaye TFF) ikiwa ni marejesho ya mkopo ambao FAT ilikopeshwa dola la 30,000 na kampuni ya Jekc Systems Limted.

Pesa hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 2002, ambapo Sekretarieti elieleza kuwasilisha ushahidi kwa nyakati tofauti kuwa Wambura alipokea jumla ya Sh84 milioni kutoka FAT/TFF kama marejesho ya mkopo kwa niaba ya kampuni hiyo.

Pili, ilielezwa kwamba Wambura amehukumiwa kwa kosa la kughushi barua kuelekeza alipwe malipo na kampuni hiyo huku akijua malipo hayo si halali.

Mdau huyo alipigiliwa msumari wa mwisho kwa kufanya vitendo vya kuishushia hadhi TFF. Hivyo kwa makosa hayo yote alifungiwa maisha kujihusisha na masuala ya soka pamoja na faini ya Sh 10 milioni.


MBASHA MATUTU

Huyu alikuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo na msimamizi wa kituo cha Shinyanga, alifungiwa kujihusisha na soka maisha.

Agosti 2018, Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo ilimfungia kiongozi huyo baada ya kumkuta na hatia ya ubadhirifu, kughushi na kuiba kinyume na kanuni za maadili ya Ligi Kuu Bara.


DUSTAN MKUNDI

Huyu alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, alifungiwa kujihusisha na masuala ya soka maisha kwa wakituhumiwa kughushi na kufanya udanganyifu katika mapato ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Ndanda FC na Simba uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Dustan na wenzake watatu walihojiwa na kuthibitisha kuwa mapato halisi yalikuwa ni Sh 37,780,000 na siyo Shilingi 34,070,000 kama alivyowasilisha msimamizi huyo wa kituo cha Mtwara.

Mbali na huyo, kamati hiyo pia ilimhukumu kifungo cha miaka mitano Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara, Kizito Mbano.


JULIUS LEO

Alikuwa ni Katibu Mkuu wa Lipuli FC ya Iringa, alifungiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa miaka mitatu na faini ya Sh 3 milioni kwa mujibu wa kifungu cha 73(4) cha Mwongozo wa Maadili wa TFF, Toleo la 2013.

Julius alitiwa hatiani kwa makosa mawili, kutoa taarifa ya uongo kuhusu kiasi ambacho klabu yake ilikuwa inaidai TFF ikiwa ni zawadi ya mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho la Azam wakati kosa la pili ni kukosa umakini katika kutunza nyaraka na siri za kiofisi, hivyo kusababisha barua rasmi ya TFF kupelekwa kwenye mitandao.


HASSAN BUMBULI

Alifungiwa kujihusisha na soka kwa miaka mitatu kwa kutotii uamuzi wa Kamati ya Maadili dhidi yake ambapo alitakiwa kulipa faini ya Sh 5 milioni na kamati hiyo na kutorudia kufanya kosa la kimaadili ndani ya miaka miwili.

Hata hivyo, Bumbuli alipangua kifungo hicho kwani alilipa pesa hizo mapema tofauti na ilivyoelezwa awali kwamba alikata rufaa na kushinda.

Mbali na vifungo hivyo, pia kuna waamuzi ambao wamefungiwa kuchezesha baadhi ya mechi pamoja na kufungiwa akiwemo Shomary Lawi alifungiwa mwaka mmoja kwa kushindwa kutafsiri sheria za soka katika mechi ya Prisons na Simba iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Rukwa.

Advertisement