UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kwa nini Simba msianzishe Hans rafiki pale Simba?

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kwa nini Simba msianzishe Hans rafiki pale Simba?

Muktasari:

  • Nimeona wamepewa jina la Mo Rafiki. Sidhani kama ni jambo baya, lakini ingeweza kuwa Simba Rafiki. Kumekuwa na mambo mengi ya Simba ambayo yamekuwa yakitumiwa kama binafsi.


Dar es Salaam. Siku  chache kabla ya Simba Day, Klabu ya Simba ilizindua vikaragosi wake. Ni jambo jema sana.

Arsenal pale nchini England wana kikaragosi wao anayeitwa Gunnersaurus. Hapo ndani ya hilo jina kuna jina la utani la Arsenal la The Gunners.

Pale Manchester United kuna kikaragosi wao anayeitwa Fred the Red. Hiyo ‘red’ hapo ni kuashiria jina lao la utani, yaani Mashetani Wekundu. Karibu kila timu hasa barani Ulaya kumekuwa na vikaragosi. Hawapewi majina ya watu binafsi, bali wanapewa majina ya utani ya timu zao.

Vikaragosi waliozinduliwa na Simba wanaitwa Mo Rafiki. Hawa ni marafiki wa bilionea na mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji maarufu kama Mo. Sio jambo baya, lakini Simba wanatakiwa kuifikiria klabu kwanza kuliko mtu. Wale vikaragosi ni njia nzuri sana ya klabu kuweza kujitangaza. Ni moja kati ya majukwaa makubwa sana kwa Simba kujiweka sokoni. Sidhani kama ni jambo baya kwa Mo kujitangaza hapo, lakini nadhani lingekuwa ni jambo zuri kama Simba ndiyo ingejitangaza.

Hakuna ubishi wowote kuwa ukubwa wa Simba hii ya sasa umetokana na nguvu za Mo Dewji. Hakuna ubishi wowote kuwa kufanya vizuri kwa Simba Afrika kwa sasa ni mkono wa Mo, lakini Simba inapaswa kutangulizwa mbele kabla ya mtu yeyote.

Wale vikaragosi wanapaswa kuitangaza zaidi klabu kuliko mtu binafsi. Wale vikaragosi wanapaswa kubeba taswira ya klabu na sio mtu.

Nimeona wamepewa jina la Mo Rafiki. Sidhani kama ni jambo baya, lakini ingeweza kuwa Simba Rafiki. Kumekuwa na mambo mengi ya Simba ambayo yamekuwa yakitumiwa kama binafsi.

Kuna Uwanja wa Simba wa mazoezi ambao unajulikana kama Mo Simba Arena. Kumekuwa na tuzo za Simba ambazo kwa sasa zinajulikana kama Mo Simba Awards. Sidhani kama ni jambo baya kumuenzi mwekezaji wa Simba, lakini nadhani klabu inapaswa kutangulizwa mbele. Naheshimu sana mchango wa Mo. Nathamini sana mchango wa Mo, lakini ikitangulizwa Simba mbele itakuwa imekaa vizuri sana.

Kama ikitokea Simba inataka kuwaenzi watu wake, basi isiwe pia mtu mmoja. Wapo watu wengi sana walioacha alama ndani ya mabingwa hao mara 22 wa Tanzania.

Wapo wachezaji wakubwa. Wapo viongozi wakubwa. Sio vibaya kama nao watawekwa kwenye vitu mbalimbali vya klabu.

Kwa mfano, hivi karibuni Simba imempoteza mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Zacharia Hans Poppe. Huyu ni mojawapo wa watu walioipenda na kuitumikia klabu maisha yake yote.

Ametoa mchango mkubwa sana kwa Simba tunayoiona leo. Kwanini wale Mo Rafiki wasingeitwa Hans Rafiki kwa heshima yake? Sina tatizo na Mo kupewa heshima hiyo, lakini nadhani wapo watu wengine pia ambao wameifanyia Simba makubwa.

Lipo kundi kubwa la wachezaji. Lipo kundi kubwa la mashabiki na lipo pia kundi kubwa la viongozi.

Mpira wetu bado unawahitaji watu wenye pesa kama Mo. Ndiyo wenye nguvu za kutuvusha kwenda nchi ya ahadi, lakini twende nao vizuri.

Lazima tuwatengenezee mazingira mazuri ya wao kufanya kazi bila kuharibu utamaduni wa klabu zetu. Simba ni kubwa kuliko mtu yeyote. Hizi ni miongoni mwa nukuu alizowahi kuzisema Mo Dewji.

Nakubaliana naye kwa Asilimia 100. Juzi kwenye Tamasha la Simba Day nilifurahi kumuona mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Emmanuel Okwi akialikwa.

Ni jambo zuri sana lakini isiishie kwa Okwi tu, Simba ni kubwa kuliko mtu mwingine yeyote. Simba Day ya mwakani panapo uzima tuone mwaliko mmoja wa wachezaji wakubwa wazawa waliowahi kuiletea heshima.

Tuone wakipata thamani ileile au zaidi ya aliyopewa Okwi. Simba ni ya kila mtu. Simba ni kubwa sana. Vikaragosi ni jambo jema, lakini kama vingepewa jina la klabu ingekuwa nzuri sana.

Vikaragosi ni jambo jema, lakini kama vingepewa jina hata la Hans Rafiki kwa heshima ya Hans Poppe ambaye ametangulia mbele za haki ingekuwa nzuri sana.

Simba ni klabu kubwa nchini. Inapaswa kumfikia kila mtu. Kitendo cha mtu mmoja kutajwa kwenye kila kitu si kosa, lakini wakitajwa na wengine inakuwa nzuri zaidi.

Simba haikufikia ukubwa huo kwa juhudi za mtu mmoja. Ni ushirikiano wa watu wengi.

Ni kama ujenzi wa nyumba huyu akileta tofali, mwingine analeta theruji. Watu kama kina Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Evans Aveva, Hassan Dalali na wengine wengi wana mchango mkubwa kwenye kukua kwa Simba.

Kama klabu itaamua kuwaenzi watu wa aina hii litakuwa ni jambo zuri. Itakuwa ni heshima kubwa kwa Simba na mpira wetu kwa ujumla.

Natambua sana mchango wa Mo Dewji ndani ya Simba. Nguvu na pesa anazoweka haziishii tu kuwanufaisha Simba, bali mpira wetu kwa ujumla, lakini nadhani kuna haja kubwa ya kuitanguliza kwanza Simba kisha wengine ndiyo wafuatie.

Nawapongeza kwa kuzindua vikaragosi. Ni sehemu ya kudumisha utamaduni wa soka. Sina tatizo na vikaragosi kuitwa Mo Rafiki, lakini kama mngevipa jina la Hans Rafiki mngemuezi vizuri Hans Poppe wetu.