UCHAMBUZI: Kaze keshaijua ramani, hawezi kupotea kizembe

HUENDA mechi tatu ambazo Yanga ilipata sare mfululizo, zilitosha kumnyoosha Cedric Kaze. Ndio, mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Tanzania Prisons kabla ya Ligi Kuu Bara.

Hii haikufuatiliwa sana, lakini ligi iliporejea tena na Yanga ililazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City.

Mechi hii iliwashtua wanayanga. Naweza kusema hapa mambo yalitibuka Jangwani. Lakini wanayanga walichefukwa zaidi, pale walipoishuhudia timu yao ikitoka sare ya mabao 3-3 na Kagera Sugar.

Tena ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Katika mechi ambayo walipotea mno hasa kipindi cha kwanza. Kitendo cha Kaze kumuanzisha benchi Mukoko Tonombe na kusababisha timu kupwaya iliwakata stimu mashabiki wa klabu hiyo. Sura zao zilionyesha hivyo mbele ya kamera za Azam TV.

Hawakujua nini kinaenda kutoka kwa timu yao. Bahati nzuri kipindi cha pili, Kaze alimrejesha kikosini Mukoko. Kiungo huyo fundi, aliirejesha Yanga mchezoni na kupata sare hiyo ya 3-3.

Utabisha nini hizo ni mechi ambazo zilimnyima raha Kaze? Hii ni kutokama na masimango kutoka kila kona ya nchi. Wananchi walichefukwa. Kama utakuwa unabisha kwa hiki ninachokisema, angalia tu namna alivyoshangilia bao la Carlinhos walipoinyoa Mtibwa Sugar katika mchezo uliofuta. Kama hiyo unaikataa basi isikilize upya kauli alizotoa kwenye mkutano wake na wanahabari baada ya mechi dhidi yas Mtibwa. Alishindwa kuficha hisia zake, namna alivyoumizwa na maneno yaliyokuwa yakielekezwa kwake na hata kwa timu yake. Aliumizwa na watu aliowaita wachambuzi. Uzuri tu, kocha huyo Mrundi hakuvuka mipaka katika kueleza alivyoumizwa na masimango hayo, ila ilitosha kuonyesha amepata somo. Hata mwenyewe alikiri, ameelewa tamaduni za wadau wa soka nchini. Amewajua kiundani Wanayanga walivyo, hasa timu yao inapopata matokeo ya ovyo. Wahenga wanasema fimbo ikuchapato ndiyo ikufunzayo! Kajifunza!

Huenda Kaze kwa sasa, ameiona rangi halisi ya soka la Tanzania. Ameishaijua ramani nzima ilivyo na katu msitarajie apotee tena njia. Kabla ya hapo alikuwa akila shushu. Hakujua kama mashabiki wa soka nchini ni vigeugeu. Wale waliokuwa wakimuimba, ghafla wamemchenjia. Yaani ni kama vinyonga. Leo wanakuwa na rangi hii, ghafla kesho wanakuwa na rangi nyingine. Mashabiki burudani yao ni kutaka kuona timu inashinda, hawataki kujua kujua timu zao zinashindaje!

Hawajui kama hii ni ligi na kila timu iliyopo kwenye inahitaji matokeo mazuri. Hakuna timu inayoshiriki ligi kwa lengo la kupoteza tu mechi zake. Ndio maana Ruvu inapigwa leo, kesho inashinda na keshokutwa inabanwa kwa sare. Kwa nini isiwe kwa Simba na Yanga maadamu zipo ndani ya ligi hiyo ambayo wachezaji wanajua nje ndani?

Hakuna ligi hivyo ya timu zisizofungika, lakini mashabiki wa Yanga na wenzao wa Simba, wanaishi dunia ya pekee yao. Wanaziamini sana timu zao. Wanaaminisha timu zao ni bora zaidi kuliko nyingine.

Wanaamini timu zao hazifungiki kirahisi au kutoka sare, ndio maana zikipata matokeo hayo mfululizo unaona wanavyowaka. Wanapagawa na kudhani zinahujumiwa. Wanavurugwa na kuhisi labda timu zao zinaonewa.

Utabisha nini? Si mliona Msimbazi kulipotibuka wakati chama lao lilipopoteza mechi mbili mfululizo? Vipigo kutoka kwa Tanzania Prisons kisha Ruvu Shooting iliwavuruga Simba.

Sio mashabiki na wanachama tu, bali hadi viongozi wake. Lilipitishwa fagio kwa baadhi ya viongozi kwa tuhuma wanaifanyia hujuma timu. Baadhi ya viongozi walifikia hatua ya kuwashutumua waamuzi.

Waliamini timu yao ilikuwa inahujumiwa nao. Haya ndio maisha ya Simba na Yanga ndani ya soka la Tanzania. Miaka nenda, rudi hazijawahi kubadilisha mfumo wa maisha haya. Sven Vandenbroeck alipokuwa Simba alishayajua maisha haya.

Alikuwa akisikia na kuona namna watu wanavyomjadili kulingana na aina ya matokeo kwa timu yake. Hakujali sana, kwani naye alikuwa na misimamo yake. Lakini alishaijua rangi za watu anaofanya nao kazi, ndio maana aliwashtukiza kwa kutimka zake Morocco.

Hakutaka CV yake iharibike kwa kitu kidogo. Aliingiza timu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya presha kubwa na kuona ni wasaa wa mtu mwingine kuendeleza alipoishia.

Kaze ni kama hakujua jambo hili, lakini kashkash alizozipata katika matokeo ya mechi hizo chache, zimemwamsha usingizini. Kuanzia sasa ataishi kwa akili zaidi kuliko mwanzo. Atalazimika kufanya kama alivyofanya Sven pale Msimbazi kabla hajatimka zake. Kuna wakati makocha wenyewe wanajichanganya. Maamuzi ya kutaka kufanya mzunguko wa nyota wake kwa kila mechi inawagharimu. Kikosi kinachoipa timu matokeo mazuri huwa hakibadilishwi ovyo labda itokee dharura ya majeruhi, adhabu ya kadi na matatizo mengine yanatoweza kumfanya mchezaji asiwepo kikosini.

Ni nadra kumwona Pep Guardiola ama makocha wa klabu nyingine kubwa duniani wanabadilisha wachezaji ovyo katika ligi au mashindano muhimu.

Kaze alishambuliwa sana katika mechi ya Kagera kwa kuamua kumweka benchi, Mukoko Tonombe! Sitaki kuamini kama kocha huyo atafanya jambo hilo tena, kama kiungo huyo ama nyota wake yeyote wa kikosi cha kwanza atakuwa hana dharura yoyote, kwani chamoto amekiona!

Lakini, licha ya hayo yote, bado itapendeza kama mashabiki wa hizi klabu za Kariakoo, zijue kuwa katika soka huwa lina matokeo matatu. Kushinda, kufungwa ama kutoka sare.

Kadhalika ni lazima wabadili mitazamo yao na wasijiaminishe kwamba timu zao ni bora kiasi kwamba hazifungiki, kwani soka halipo hivyo.

Hivyo pale timu zao zinapopata matokeo maadamu yapo ndani ya mfumo wa kawaida wa soka, wavumilie na kuwaunga mkono makocha na wachezaji wao badala ya kuwasakama.

Waache kuwapa presha makocha na hata wachezaji wa timu zao, kwani wakati mwingine presha hizo huwa zinawapotezea dira zaidi.

Ni kweli hakuna mdau yeyote wa klabu anayependa kuona timu yake ikipata matokeo mabaya, lakini kuna wakati lazima wayakubali. Kama Barcelona, Atletico Madrid na Real Madrid kama sio Bayern Munich, PSG, Man City, Liverpool na Man United zinachapika, Simba na Yanga zina nini cha ajabu kinachozuia timu zao zisifungwe katika ligi ama michuano mingine?

Imeandikwa na BADRU KIMWAGA