Uganda ‘The Cranes’ ilivyoanzia mguu mbaya CHAN 2024
Muktasari:
- Uganda haijawahi kuvuka zaidi ya hatua ya makundi kwenye Fainali za CHAN ambazo imeshiriki mara saba tofauti.
TIMU ya Taifa ya Uganda 'The Cranes', imeanza vibaya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN), baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Algeria katika pambano la kwanza la ufunguzi la kikosi hicho.
Katika mechi hiyo ya kundi C iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Algeria ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 36, lililofungwa na nahodha Ayoub Ghezala aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Abderrahmane Meziane.
Licha ya wenyeji kucheza soka safi na kutengeneza mashambulizi mbalimbali, wageni Algeria waliongeza bao la pili katika dakika ya 76, kupitia kwa Abderrahmane Meziane, aliyepiga shuti kali na kumshinda kipa wa Uganda, Jude Ssemugabi.
Bao la tatu la Algeria lililopoteza matumaini kwa wenyeji kuchomoa, limefungwa na Soufiane Bayazid katika dakika ya 79, ikiwa ni muda mchache tu tangu nyota huyo aingie dakika ya 69, akichukua nafasi ya mshambuliaji wa timu hiyo, Aimen Mahious.
Kwa matokeo hayo, Algeria inaongoza kundi C ikiwa na pointi tatu sawa na Guinea iliyo nafasi ya pili baada ya kuanza vyema kwa kuichapa Niger bao 1-0 huku Afrika ya Kusini ikishika nafasi ya tatu, wakati Uganda inaburuza mkia wa kundi hilo.
Matokeo haya, yanaifanya Uganda kuwa timu pekee ambayo ni mwenyeji wa CHAN 2024 kuanza kwa kichapo, baada ya Taifa Stars kushinda mechi ya kwanza kwa ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 2, 2025.
Wenyeji wengine wa michuano hiyo, timu ya Taifa ya Kenya 'Harambee Stars', iliyo kundi A ilianza vyema pia jana baada ya kuifunga DR Congo kwa bao 1-0, lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Austine Odhiambo aliyepokea pasi safi ya David Sakwa.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Uganda ndio taifa lililofanikiwa zaidi kutoka ukanda wa CECAFA likiwa na mataji 40, huku ikishiriki CHAN mara ya saba, baada ya kufanya hivyo, mwaka 2011, 2014, 2016, 2018, 2020, 2022 na 2024.
Uganda imeendeleza rekodi mbovu kwa Algeria kwani kabla ya pambano la leo, mara ya mwisho zilikutana kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambapo zilipangwa tena kundi F na kikosi hicho cha The Cranes kikachapwa mechi zote.
Katika mechi ya kwanza, Algeria ilishinda nyumbani mabao 2-0, Juni 4, 2022, huku ile pia ya marudiano iliyopigwa Uganda kikosi hicho kikashindwa kutamba mbele ya mashabiki zake, baada ya kukubali kupoteza tena kwa mabao 2-1, Juni 18, 2023.
Kwenye kundi hilo, Algeria ilikuwa vinara na pointi 16, ikifuatiwa na Tanzania iliyomaliza ya pili na pointi nane, huku Uganda ikiwa ya tatu na pointi saba, wakati Niger iliburuza mkiani, baada ya timu hiyo kuambulia kukusanya pointi mbili.
Hata hivyo, katika fainali za CHAN zilizofanyika Sudan mwaka 2011, timu hizo zilipangwa kundi moja la A, ambapo Uganda ilichapwa tena mabao 2-0, yaliyofungwa na Abdelmoumene Djabou na Hillal Soudani, mechi iliyopigwa Februari 5, 2011.
Katika fainali hizo zilizoshuhudia Tunisia ikitwaa ubingwa, wenyeji Sudan ilimaliza kinara wa kundi A na pointi saba, Algeria ikishika ya pili na pointi tano, huku Gabon ikimaliza ya tatu na pointi nne, wakati Uganda ilichapwa mechi zote.