Vita ya CHAN sasa imehamia Uganda
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Uganda ndio taifa lililofanikiwa zaidi kutoka ukanda wa CECAFA likiwa na mataji 40, huku ikishiriki CHAN kwa mara ya saba, baada ya kufanya hivyo, mwaka 2011, 2014, 2016, 2018, 2020 na 2022.
Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN), inaendelea tena leo kurindima kwa mechi za kundi C, ambapo Niger itaikaribisha Guinea saa 11:00 jioni, huku wenyeji, Uganda 'The Cranes', ikipambanaa na Algeria.
Niger inashuka kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, uliopo huko Uganda kupambana naa Guinea huku timu hizo zikiwa na rekodi ya kukutana katika michuano hiyo mwaka 2016 iliyofanyika Rwanda na DR Congo kutwaa ubingwa huo, ukiwa ni wa pili kwake.
Baada ya DR Congo kuchukua ubingwa mwaka 2009 kule Ivory Coast, kikosi hicho kikatwaa tena taji la mwaka 2016, likiwa ni la pili kwake katika michuano hiyo iliyofanyika Rwanda, kufuatia kuifunga Mali kwa mabao 3-0, kwenye mechi ya fainali.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa Februari 7, 2016, kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Amahoro, mabao hayo ya DR Congo yalifungwa na Meschak Elia aliyefunga mawili dakika ya 29 na 61, huku lingine likifungwa na Jonathan Bolingi dakika ya 73.
Kikosi hicho kilitwaa ubingwa huo kikiwa chini ya Kocha, Florent Ibenge anayeiongoza Azam FC msimu wa 2025-2026, huku Meschak Elia anayeichezea BSC Young Boys ya Uswisi akiibuka kidedea na tuzo ya mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP).
Mbali na tuzo ya MVP, Meschak Elia aliibuka mfungaji bora sawa na Ahmed Akaichi (Tunisia) na Chisom Chikatara (Nigeria), ambao kila mmoja alifunga mabao manne, huku aliyekuwa nyota wa Coastal Union, Ley Matampi akishinda tuzo ya kipa bora.
Katika fainali za mwaka 2016, timu hizo zilipangwa pia kundi C kama ilivyo mwaka huu, ambapo zilitoka sare ya mabao 2-2, katika mechi iliyopigwa Januari 22, 2016 na kushuhudia Niger ikiburuza mkiani, baada ya kukusanya pointi yake moja tu.
Kwenye kundi hilo, Tunisia iliongoza kwa kukusanya pointi tano, sawa na Guinea iliyomaliza ya pili ila, zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, huku Nigeria ikimaliza nafasi ya tatu, baada ya kikosi hicho kujikusanyia pointi nne.
Kwa upande wa Uganda ambayo inashirikiana na Tanzania na Kenya kuandaa michuano hiyo, itashuka kwenye Uwanja wa Nelson Mandela kucheza na Algeria kuanzia saa 2:00 usiku, huku The Cranes ikipambana kuondokana na jinamizi la kufanya vibaya.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Uganda ndio taifa lililofanikiwa zaidi kutoka ukanda wa CECAFA likiwa na mataji 40, huku ikishiriki CHAN kwa mara ya saba, baada ya kufanya hivyo, mwaka 2011, 2014, 2016, 2018, 2020 na 2022.
Uganda haina rekodi nzuri kwa Algeria kwani mara ya mwisho timu hiyo zilikutana kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambapo zilipangwa katika kundi F na kushuhudia kikosi hicho cha The Cranes kikichapwa mechi zote mbili.
Katika mechi ya kwanza, Algeria ilishinda nyumbani mabao 2-0, Juni 4, 2022, huku ile pia ya marudiano iliyopigwa Uganda kikosi hicho kikashindwa kutamba mbele ya mashabiki zake, baada ya kukubali kupoteza tena kwa mabao 2-1, Juni 18, 2023.
Kwenye kundi hilo, Algeria ilikuwa vinara na pointi 16, ikifuatiwa na Tanzania iliyomaliza ya pili na pointi nane, huku Uganda ikiwa ya tatu na pointi saba, wakati Niger iliburuza mkiani, baada ya timu hiyo kuambulia kukusanya pointi mbili.
Hata hivyo, katika fainali za CHAN zilizofanyika Sudan mwaka 2011, timu hizo zilipangwa kundi moja la A, ambapo Uganda ilichapwa tena mabao 2-0, yaliyofungwa na Abdelmoumene Djabou na Hillal Soudani, mechi iliyopigwa Februari 5, 2011.
Katika fainali hizo zilizoshuhudia Tunisia ikitwaa ubingwa, wenyeji Sudan ilimaliza kinara wa kundi A na pointi saba, Algeria ikishika ya pili na pointi tano, huku Gabon ikimaliza ya tatu na pointi nne, wakati Uganda ilichapwa mechi zote.