Ujio mpya wa Kim Poulsen gumzo

Muktasari:

  • Urejeo wa aliyekuwa kocha wa timu za vijana Tanzania na timu kubwa ya Taifa, Kim Poulsen umeibua hoja kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka nchini.

Urejeo wa aliyekuwa kocha wa timu za vijana Tanzania na timu kubwa ya Taifa, Kim Poulsen umeibua hoja kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka nchini.

Kurejea kwa kocha huyo kulithibitishwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alipozungumza na gazeti Mama (Mwanaspoti) akisema kocha huyo anarudi kuwa mshauri wa ufundi kwenye soka la vijana.

Baada ya kauli hiyo, jana TFF walitoa barua ambayo inaonyesha kumpa kocha Kim mkataba wa miaka mitatu kwa ajili ya kuinoatimu ya Taifa,

Taifa Stars.

Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alihoji uhakika wa viongozi wa sasa wa TFF kama kocha Poulsen bado alikuwa anaendelea kufanya kazi za soka hadi sasa.

Mwaisabula alisema kwa ufahamu wake, Kim aliondoka nchini muda mrefu, hivyo hana uhakika kama viongozi wamekuwa wakifuatilia kwa ukaribu nini ambacho kocha huyo anakifanya.

“Namfahamu vizuri Kim kwamba ni kocha mzuri sana hasa katika soka la vijana, viongozi wa sasa (TFF) wengi hawakuwepo wakati wa Kim, lakini waliona kazi yake, ndiyo maana wamemrejesha, wasiwasi wangu ni uhakika wa ubora wake wa sasa,” alisema Mwaisabula.

Saad Kawemba, ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, alihoji Kim anakuja kuwa mshauri wa soka la vijana kwa mfumo upi.

Kawemba alisema ni mfumo upi uliotengenezwa kwa ajili ya kuletwa Kim, kwani wanaomleta bado wana maswali ya kujibu. Lakini taarifa ya sasa inaweza kuwa na majibu kutokana na kuja kama kocha wa Stars.

“Kama klabu tu zinashindwa kuwa na timu za vijana kama kanuni zinavyotaka sijajua kama tunaweza kuwa na timu za vijana angalau moja kwa kila mkoa, tena zikiwa na makocha wa kuwafundisha vijana.

“Kwangu, Kim ni kocha mzuri kwa vijana, hata mimi nilipokuwa pale TFF nakiri kwamba tulifanya kosa kumtoa timu ya vijana na kwenda timu kubwa baada ya kutamani mafanikio ya haraka.

“Lakini Kim baada ya kurejea aliondoka vipi, aliondoka kutokana na uwezo kuwa mdogo au mahitaji yake yalikuwa makubwa?” alihoji Kawemba.

Mchezaji Ibrahim Twaha ‘Messi’ ambaye alipitia katika mikono ya Kim alisema kama kocha huyo anarejea kwa upande wa soka la vijana itakuwa ni vizuri zaidi, lakini kama ni timu ya Taifa pekee inaweza kuwa changamoto.

“Kim ni kocha ambaye anajua namna gani ya kuishi na vijana na kumfanya kijana afurahie mpira, ukiangalia hilo limefanya wachezaji wake wengi ambao aliwafundisha sasa hivi ndiyo wapo kwenye ligi.

“Unajua timu za taifa kwa vijana hapa Tanzania ndio akademi zetu ila watu hawajaelewa tu, wanakula muda sahihi, wanafanya mazoezi muda sahihi na wanapata posho, kijana anajiona amethaminika na kutamani kufika juu.”

Kim alikuja nchini Mei 2011 akiwa kama kocha wa timu za vijana na Mei 2012 aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa Tanzania, lakini alitimuliwa.

Kocha huyo alirejea tena nchini 2016 akiwa mshauri wa timu za vijana akiwa na kocha Bakari Shime na kuiwezesha Tanzania kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza nchini Gabon, 2017.