Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ujirani wa Tanzania, Uganda ulivyohamia AFCON, Msuva aandika rekodi

Muktasari:

  • Tanzania na Uganda wamebakisha mchezo mmoja kwa kila timu ambao ndio utaamua hatima yao kwenye Fainali za AFCON 2025.

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni ujirani unaendelezwa hadi AFCON baada ya sare ya bao 1-1 baina ya Uganda na Tanzania ambapo wote wanatokea Afrika Mashariki.

Sare hiyo imeendelea kuwaweka njiapanda majirani hao katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 wakijikusanyia pointi moja katika michezo miwili kila mmoja.

Mabao ya mchezo huo yamefungwa na Simon Msuva kwa mkwaju wa penalti kwa upande wa Tanzania huku Uche Ikpeazu akiisawazishia Uganda.

Kinda wa Uganda, Allan Okelo alishindwa kuihakikishia timu yake pointi tatu baada ya kupoteza mkwaju wa penalti dakika ya 90 ya mchezo huo.

Msimamo wa Kundi C baada ya mechi mbili Stars ipo nafasi ya tatu na pointi 1, sawa Uganda inayoshikilia mkia na Nigeria akiongoza kundi akifuatiwa na Tunisia.

Stars imebakiza mechi dhidi ya Tunisia ikamilishe mzunguko wa kundi huku Uganda akibakisha dhidi ya Nigeria.

Aidha, Msuva amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mchezo 'Man of the Match' katika mchezo huo akicheza dakika zote 90.


Rekodi ya Msuva

Bao la mkwaju wa penalti katika mchezo wa dhidi ya Uganda limempa rekodi tatu tamu Msuva.

Kwanza amefikia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Mrisho Ngassa kwa muda mrefu.

Ngassa ameifungia Taifa Stars mabao 25, idadi ambayo leo imefikiwa baada ya Msuva kufunga bao hilo.

Msuva ameendeleza pia rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyeifungia Taifa Stars mabao katika awamu nyingi tofauti za AFCON ambapo hii ni mara ya tatu.

Alifunga katika fainali za 2019 zilizofanyika Misri na kisha akafanya hivyo katika AFCON ya 2023 ilizofanyika Ivory Coast.

Rekodi ya tatu ambayo Msuva ameiweka ni ya kuwa mchezaji aliyefunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika kikosi cha Taifa Stars kwenye Fainali za AFCON.

Awali rekodi hiyo ilikuwa inashikiliwa kwa pamoja na yeye na Thuweni Ally ambao walikuwa kila mmoja amefunga mabao mawili na sasa Msuva amefikisha mabao matatu.