Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

United yamuongezea dau Mbeumo

Muktasari:

  • Iwapo dili hilo litakamilika, Mbeumo atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na United katika dirisha hili la usajili baada ya Cunha na beki kinda Diego Leon.

Manchester, England. Manchester United imewasilisha ofa mpya ya jumla ya pauni 70 milioni kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji wa Brentford, Bryan Mbeumo, katika jitihada za kuendeleza mazungumzo kati ya timu hizo kuhusu usajili huo.

Awali, United ilikataliwa ofa yao ya pili ya pauni  62.5 milioni kiasi sawa na walicholipa kwa Wolves kumsajili Matheus Cunha.

Hata hivyo, Mashetani Wekundu sasa wana matumaini kuwa ofa yao mpya ya pauni milioni 65 pamoja na nyongeza ya pauni milioni 5 kwa masharti maalumu itawashawishi Brentford kumuachia Mbeumo, ambaye tayari ameonyesha nia ya kutaka kuhamia Old Trafford.

Iwapo timu hizo mbili zitafikia makubaliano, nyota huyo wa kimataifa wa Cameroon atapaswa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kukamilisha usajili wake, hali inayoashiria kuwa huenda asiwahi kucheza katika mechi za kwanza za United za kirafiki .

Hata hivyo, inawezekana akajumuishwa kwenye kikosi cha United kitakachosafiri kwenda Marekani kwa ziara ya maandalizi ya msimu mpya wiki ijayo, endapo ofa hii ya tatu itakubaliwa na Brentford na kufanikisha uhamisho huo ambao umekuwa moja ya vuguvugu kubwa la usajili msimu huu wa kiangazi.

Iwapo dili hilo litakamilika, Mbeumo atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na United katika dirisha hili la usajili baada ya Cunha na beki kinda Diego Leon.

Kocha mkuu Ruben Amorim pia ataonekana kufanikisha usajili wa wachezaji wake wawili anaowapendelea kwa nafasi ya namba 10 kwenye mfumo wake wa 3-4-2-1, akitumia zaidi ya pauni milioni 130 kwa Cunha na Mbeumo.

Mbeumo, mwenye umri wa miaka 25, alifunga mabao 20 kwenye Premier League msimu uliopita akiwa na Brentford. Pia amekuwa akiwindwa na vilabu vingine vikubwa vya EPL kama Arsenal, Newcastle na Tottenham inayofundishwa na kocha wake wa zamani, Thomas Frank.

Tatizo la upachikaji mabao ndilo lililowakosesha United mafanikio msimu uliopita, wakifunga jumla ya mabao 44 pekee kwenye EPL idadi ya pili ya chini zaidi kwa timu isiyoshuka daraja, na rekodi mbaya zaidi tangu ligi hiyo ilipobadilishwa jina mwaka 1992.

Tangu alipowasili Brentford mwaka 2019 kwa dau la pauni milioni 5.8, Mbeumo amefunga jumla ya mabao 70 katika mechi 242, yakiwemo 42 kwenye mechi 136 za Premier League, akijizolea sifa kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi kwenye ligi hiyo.

Mchezaji wa zamani wa United Rio Ferdinand, ameonya kuwa United itajipatia aibu iwapo dili hilo halitakamilika. “United wanapaswa kufikia kiwango cha thamani kilichoainishwa na Brentford,” alisema Rio. “Wameonyesha wazi kuwa wanamtaka, na sasa wanapaswa kuhakikisha wanamaliza dili hili.”

Wakati huo huo, Brentford wiki hii ilitoa video ya wachezaji wao wakirejea mazoezini, ambapo Mbeumo alionekana akiwa mwenye furaha, akifika peke yake na kuwasalimia wafanyakazi akiwa mchezaji wa mwisho kuingia kwenye kituo cha mazoezi.

Ikiwa dili hili litakamilika, Mbeumo anaweza kuwa suluhisho muhimu kwa tatizo la mabao lililowakumba United msimu uliopita, huku mashabiki wakingoja kwa hamu kuona iwapo ataungana rasmi na kikosi cha Amorim.