Prime
Vita ya usajili Simba, Yanga

Muktasari:
- Kwa upande wa Simba, Fadlu anaamini kikosi chake kinahitaji kuboreshwa kwa maeneo manne muhimu ambayo ni kiungo wa kuzuia, kiungo wa kushambulia, mshambuliaji wa kati, na beki wa kati mwenye kasi na uamuzi wa haraka.
Simba na Yanga ni washindani wakubwa katika soka la Bongo, kuanzia ndani ya uwanja hadi nje. Hali hiyo tumeishuhudia tena msimu uliomalizika hivi karibuni.
Vigogo hao wa soka hapa nchini baada ya vita yao ndani ya uwanja kumalizika na Yanga kuwa bingwa, sasa wamehamishia nje ya uwanja, wanasuka vikosi vyao kuelekea msimu ujao.
Si vigogo hao pekee, bali klabu zote 16 zitakazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao zimeanza kujipanga mapema huku kelele za usajili zikishika kasi. Hakuna anayetaka kupitwa. Kila mmoja anataka kufikia malengo. Waliojikwaa msimu uliomalizika, wana hasira zaidi, huku wale waliofanikiwa, wanataka kuendeleza ubabe wao.
Sababu kubwa ya kuanza mapema kwa harakati hizi za usajili hata kabla ya dirisha kufunguliwa rasmi ni dhamira ya kuonesha namna ya kujipanga kikamilifu na kufuta makosa. Si JKT Tanzania, KMC, Tanzania Prisons wala Namungo, kila mmoja yupo bize kujiimarisha.
Kwa Simba na Yanga, kutokana na kujihakikishia nafasi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, inatajwa kuwa ndiyo sababu ya kuingia sokoni mapema. Hata Singida Black Stars na Azam ambazo nazo zitashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids na Miloud Hamdi aliyekuwa Yanga kabla ya kuondoka hivi karibuni, walishawasilisha ripoti kamili kuhusu maeneo ya kuboreshwa. Wameomba wachezaji wa viwango vya juu, wakiwa na sifa za kiuchezaji lakini pia tabia zinazolingana na maono ya klabu.
Azam nayo imemshusha Florent Ibenge, huku ikitangaza usajili wa wachezaji watatu wazawa, Lameck Lawi, Aishi Manula na Muhsin Malima.
Singida Black Stars nayo imeanzia kwenye benchi la ufundi, imemrudisha Miguel Gamondi aliyewahi kuinoa Yanga, huku suala la usajili likianza mdogomdogo.
Ramani ya Simba
Kwa upande wa Simba, Fadlu anaamini kikosi chake kinahitaji kuboreshwa kwa maeneo manne muhimu ambayo ni kiungo wa kuzuia, kiungo wa kushambulia, mshambuliaji wa kati, na beki wa kati mwenye kasi na uamuzi wa haraka.
Mapungufu haya yalijitokeza zaidi kwenye mashindano ya kimataifa, ambapo Simba ilionekana kukosa uimara wa kimkakati hasa ilipokutana na timu za Afrika Magharibi na Kaskazini.
Ripoti ya Fadlu inaeleza kuwa Simba inahitaji mchezaji wa kusimama mbele ya walinzi, kuwasoma wapinzani na kupoza presha kabla haijafika langoni. Aidha, ameomba mchezaji namba 10 mwenye ubunifu wa hali ya juu si wa kusambaza pasi tu, bali wa kuamua matokeo ya mechi kwa ubora wa uamuzi wake katika sekunde chache.
Hali hiyo inakwenda sambamba na ombi la mshambuliaji mpya. Licha ya uwepo wa Leonel Ateba na Steven Mukwala na nyota chipukizi kama Valentino Mashaka, Simba inahitaji straika mwenye uzoefu, aliyekutana na presha za soka la Afrika, anayefunga bila kupewa nafasi nyingi.
Lakini anahitaji kipa mpya mzawa wa kumpa changamoto Moussa Camara kama ataendelea kusalia kikosini kutokana na kuondoka kwa Aishi Manula ambaye msimu mzima aliwekwa benchi, huku Ally Salim na Hussein Abel wakishindwa kutoboa.
Pia kuna kiungo mshambuliaji mkali zaidi ya Jean Charles Ahoua anayetakiwa kuongeza nguvu eneo hilo kwa wachezaji walioonekana wangeweza kumsumbua kama Awesu Awesu na wenzake kikosini kwa sasa ni kama vile wamechemka na kumfanya Fadlu kupiga hesabu mpya.
Yanga katika ukurasa mpya
Baada ya kuwa na mafanikio makubwa msimu uliomalizika kwa kubeba mataji matano, Yanga inakabiliwa na changamoto msimu ujao kutokana na kuondokewa na kiungo tegemeo, Stephane Aziz Ki aliyetua Wydad Casablanca.
Kuondoka kwake ni pengo ambalo haliwezi kuzibwa na mchezaji wa kawaida, anahitajika mtu mwenye maono na ukomavu kama wake.
Kocha Hamdi aliomba mbadala wa Aziz KI mapema kabla ya kutimkia. Lakini si Aziz Ki tu, Yanga inahitaji mshambuliaji mwingine wa kati kutokana na uwepo wa taarifa za Clement Mzize kuhusishwa na klabu kadhaa za nje.
Vilevile, kutokana na kutokuwepo kwa uhakika kwenye beki ya kulia kufuatia majeraha ya muda mrefu aliyonayo Kouassi Attohoula Yao, Hamdi alitaka mchezaji wa nafasi hiyo asajiliwe mapema.
Yanga pia inahitaji mbadala wa Khalid Aucho ambaye mkataba wake uliisha na tayari ameongezwa mwaka mmoja. Katika mechi za kimataifa, uzoefu na uimara wake umetegemewa sana. Kwa kuongezewa mkataba, basi mbadala wake lazima awe tayari kuanza kusoma ramani mapema wakati Mganda huyo akielekea ukingoni kuishi Jangwani.
Soko lilivyo
Majina mengi yamekuwa yakitajwa. Baadhi yao ni Feisal Salum 'Fei Toto', kiungo wa Azam FC anayewaniwa kwa nguvu na timu zote mbili. Simba imeshatuma ofa yao, lakini Yanga iko tayari kufunguka zaidi. Tayari kuna taarifa kuwa ofa ya mshahara wa Sh. milioni 40 kwa mwezi imewekwa mezani.
Imourane Hassane ni kiungo mkabaji kutoka Loto Popo ya Benin, aliyewahi kupita Uswizi. Simba inamtazama kama nyongeza bora kwa safu ya kiungo wa ulinzi.
Damaro Camara ni kiungo wa Singida Black Stars ambaye ametajwa kuwa na utulivu mkubwa na uelewa wa mchezo. Yanga inamuona kama suluhisho la namba 6 au 8.
Koimizo Abdul Abass Maïga anayecheza ASEC Mimosas, analengwa na Yanga kama mbadala wa Aucho.
Gibril Sillah, winga mahiri aliyemaliza mkataba Azam FC, anatajwa kupewa mkataba na Yanga.
Jonathan Sowah ni mshambuliaji wa Singida Black Stars. Simba inamtaka, lakini Yanga na Kaizer Chiefs pia zinamuhitaji.
Henock Inonga, beki wa kati wa FAR Rabat aliyewahi kung’ara Simba. Anatajwa kuwindwa na Yanga.
Mofosse Karidioula, winga anayetajwa kumalizana na Simba kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast ni kati ya wachezaji waliokuwa wakipigiwa hesabu. Kocha Fadlu alimtaka winga huyu na kama ameshatua kazi imemalizika kwa eneo hilo na kulichobaki ni kwa maeneo mengine.
Ushindani, mahitaji mapya
Katika kipindi cha nyuma, Simba na Yanga zilifanya usajili wa majina makubwa lakini bila muunganiko wa kiufundi. Sasa zinabadilika. Zinafuata hesabu za kisayansi kwa kufanya 'scouting', data, umri, matumizi ya GPS tracker na psychology za wachezaji kabla ya kusaini mikataba.
Hii ndiyo sababu ripoti za makocha zimepewa uzito mkubwa. Hakuna tena usajili kwa presha za mitandaoni. Falsafa imebadilika usajili wa kimkakati wa kusaidia kocha kutimiza malengo yake.