Vodacom wavunja mkataba Ligi Kuu

Tuesday June 08 2021
vodacompic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Kampuni ya Vodacom Tanzania imesema haina nia ya kuendelea kuidhamini Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na mwenendo mbovu wa biashara usioridhisha na kuiandikia TFF kuvunja mkataba.

Kwa mujibu wa ripoti ya fedha ya awali ya kampuni hiyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 Vodacom imepata hasara ya Sh30 bilioni tofauti na mwaka uliopita walipata faida ya Sh45.76 bilioni.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kampuni hiyo ambayo imekuwa ikidhamini Ligi Kuu kwa miaka 10 ilipata hasara kutokana na wateja wake zaidi ya milioni 2.9 kufungiwa laini zao kwa kushindwa kukamilisha usajili wa alama za vidole pamoja na sababu nyingine za kikodi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu jana, Ofisa mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi alisema imekuwa ni fahari kubwa kwa kudhamini Ligi Kuu Tanzania ikiitwa jina lao kwa zaidi ya miaka 10, lakini kutokana mwenendo wa ufanisi wa kampuni hawataendelea.

“Tunafurahia ubia na tunaupenda, ligi imekuwa ikiitwa jina letu, lakini kwa kampuni ambayo inatengeneza hasara, leo usipoweza kuinuka juu lazima uangalie gharama zako na katika mazingira magumu lazima uchukue uamuzi mgumu.

“Kila msimu tunatumia zaidi ya Sh3 bilioni, lakini pengine tunaweza kuwa na majadiliano na TFF kwa baadaye, lakini kwa sasa tunapaswa kuchukua uamuzi mgumu na si kwa udhamini wa ligi pekee bali na mambo mengine ya kupunguza gharama,” alisema Hendi.

Advertisement

Wakati mkurugenzi huyo akisema hayo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo alisema anachofahamu ni kwamba udhamini wa kampuni hiyo utamalizika msimu ujao.

Kasongo alisema mkataba wa miaka mitatu uliosainiwa 2019 unatakiwa kumalizika mwakani kama walivyosainishana na hana taarifa ya barua ya kuvunjwa.

“Ninachofahamu ni kwamba mkataba wetu unamalizika 2022, sina taarifa za kutosha juu ya kuondoka kwa mdhamini katika mwaka huu,” alisema kwa kifupi.

Vodacom Tanzania imetoa taarifa ya kimaandishi kwa TFF, na Hendi alithibitisha kutuma barua TFF, ambayo hadi jana haikuwa imejibiwa.

“Tuliwaandikia wenzetu wa TFF kuwaambia kile tunachokikusudia lakini hadi sasa hawajatujibu, ila hatuna nia ya kuendelea,” aliongeza Hendi.

Advertisement