VPL SPESHO: Yanga SC ilipotea hapa

Monday July 19 2021
vpl spesho pic
By Khatimu Naheka

WAKATI msimu wa Ligi Kuu Bara 2020/21 ukimalizika jana Jumapili na kutarajiwa kuanza, moja ya timu iliyohesabiwa kwamba ingeweza kuwapa shida Simba katika kutetea taji lao, Yanga ilikuwemo.

Hesabu hizo zilikolea zaidi kwani Yanga hadi inamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ilikuwa inaongoza msimamo wa ligi lakini sio tu hapo hawakuwa wamepoteza mchezo wowote kisha baadaye kushtua zaidi wakienda kuchukua taji la Kombe la Mapinduzi tena mbele ya Wekundu hao.

Ghafla mambo yalibadilika, Yanga ilianza kuporomoka hadi kufikia hatua ya kupoteza matumaini ya kuwa mabingwa wakiiacha Simba ikichukua taji lao la nne mfululizo msimu huu, na hizi ni baadhi ya sababu zilizowaangusha Yanga.


Changamoto

za kiungozi

Advertisement

Uongozi wa Yanga uliiangusha timu yao ndani yao hawakuonekana kutulia kulikuwa na changamoto nyingi wakianza msimu kwa kufukuzana na hata baadhi ya watendaji katika sekretarieti kutimuliwa makosa yakawa mengi zaidi baadaye kiasi cha kufikia baadhi ya mambo mengi kufanywa na hata viongozi wa wadhamini wao.

Hebu angalia jinsi Yanga ilivyompoteza aliyekuwa mchezaji wao Bernard Morrison katika mazingira rahisi tena akienda kutua kwa watani zao Simba.


Usajili

uliwaangusha

Usajili wa Yanga nao uliwaangusha kuna baadhi ya wachezaji waliiangusha timu wakionekana mapema kuwa na ubora mdogo tofauti na watu walivyotarajia, angalia ingizo jipya kama la mshambuliaji Michael Sarpong licha ya kuanza vizuri lakini baadaye kadiri ya muda ulivyosogea alipotea.

Kiungo Carlos Carmo ‘Carlinhos’ licha ya kuwa na kipaji kikubwa lakini muda aliokaa nje ulikuwa mwingi kuliko kucheza uwanjani hatimaye ubora huu uliangusha timu yao na kujikuta wanateseka na majina waliyoyasajili wakiwa na imani nayo makubwa kwamba wangewakomboa, mfano mwingine ni usajili wa mshambuliaji Fiston Abdulrazack uliongeza shida katika timu yao.

Angalau usajili wa wachezaji kama Mukoko Tonombe,Tuisila Kisinda, Said Ntibazonkiza walikuja na nguvu ya kuirudishia thamani timu hiyo.


Mabadiliko

ya makocha

Msimu huu Yanga imeongozwa na makocha wanne tofauti wakianza na mzawa Juma Mwambusi ambaye alianza na maandalizi ya msimu na kikosi hicho kisha kabla ya kuanza ligi akapokewa na Zlatko Krmpotic ambaye aliiongoza timu hiyo kwa mechi tano pekee kisha akapoteza kazi waliomuajiri wakiona timu yao haikuwa inashinda kwa soka lenye afya kwao.

Baada ya kutimuliwa kwa Krmpotic, iliruidi tena kwa kocha waliotaka kumchukua mwanzo wa msimu Mrundi Cedric Kaze ambaye naye aliongoza mechi 22 ukiongeza na zile mechi za Kombe la Mapinduzi.

Nuksi ikaja baada ya kupoteza mechi yao ya kwanza ya ligi dhidi ya Coastal na baadaye kupata tena sare akapoteza kazi na ajira hiyo kurejea tena kwa Mwambusi ambaye naye baada ya mechi mbili tu akaondolewa na akaletwa kocha mpya wa sasa Nesreddine Nabi.

Mabadiliko haya yalionekana wazi kuisumbua Yanga katika kukosa utulivu wa kikosi chao wachezaji walionekana kupoteza ubora wakishindwa kung’amua kwa haraka washike kipi.


Kipigo, sare mbili ziliwatibulia

Kuna matokeo fulani ya mfululizo yaliwaumiza Yanga na kuwaondoa haraka katika mbio za ubingwa, kumbuka pale ilipopoteza mechi yake ya kwanza dhidi ya Coastal Union ugenini na baadaye kupata sare mbili mfululizo dhidi ya Polisi ugenini na KMC nyumbani, matokeo haya yaliwaondoa zaidi kwenye mbio za ubingwa wakimuacha Simba kujitanua.

Nidhamu kwa wachezaji

Yanga pia ilikumbwa na jinamizi la ukosefu wa nidhamu kwa wachezaji wake nahodha wao mkuu Lamine Moro, Sarpong na hata kipa Metacha Mnata kwa nyakati tofauti walilazimika kukaa nje ya kikosi hicho kutokana na shida ya nidhamu ingawa sasa inaelezwa wamerudishwa, ndani ya kikosi chao kulikuwa na makundi mengi ya wachezaji hili nalo liliwabomoa zaidi.


Makosa binafsi

kwa wachezaji

Kuna maeneo pia tunaweza kusema Yanga ilikosa bahati hebu kumbuka matokeo ya sare ya dakika za mwisho dhidi ya Mbeya City wakati Yanga wakiamini wanashinda ghafla matokeo yanabadilika.

Matokeo mengine ni katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Yanga inaruhusu mabao yaliyomfanya kipa, Metacha Mnata kulaumiwa na kutofautiana na mashabiki wa timu hiyo akionekana kuruhusu mabao ya kizembe.

Ukiachana na hapo kuna mchezo wa ugenini dhidi ya Namungo Yanga inafunga bao safi lakini mwamuzi namba moja analikataa ingawa baadaye alifungiwa kwa makosa hayo na kuilazimisha Yanga kuangusha pointi mbili.


Kipi kifanyike

Yanga inatakiwa sasa kujifunza na changamoto hizi hatua nzuri kwao sasa wanaonekana kutulia katika uongozi wakionekana kuwa wamoja hali hii inatakiwa kudumishwa pia wanatakiwa kutulia katika hesabu zao za kuendelea kuijenga timu yao kwa tathimini nzuri ya wachezaji ambao wanahitajika kuja kuongeza nguvu kama hakutakuwa na utulivu katika usajili wanaweza kuja kuanguka tena.

Advertisement