Wababe wanne Ligi ya Mabingwa Ulaya
Muktasari:
Usiku huo ulishuhudia timu za Real Madrid ya Hispania, ambayo iliitupa nje Manchester City kwa mikwaju ya penalti ikitinga hatua ya nusu sawa na Bayern Munich ya Ujerumani ambayo iliitupa nje Arsenal iliyokuwa inapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.
Ligi ya Mabingwa Ulaya ilimaliza hatua ya robo fainali juzi baada ya vigogo wa England Manchester City na Arsenal kuondolewa kwenye michuano hiyo kwa usiku mmoja.
Usiku huo ulishuhudia timu za Real Madrid ya Hispania, ambayo iliitupa nje Manchester City kwa mikwaju ya penalti ikitinga hatua ya nusu sawa na Bayern Munich ya Ujerumani ambayo iliitupa nje Arsenal iliyokuwa inapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.
Sasa ni rasmi wababe wanne kutoka mataifa matatu ndiyo wanakwenda kuvaana kwenye hatua ya nusu fainali, huku kila mmoja akionekana kuwa na nafasi kubwa ya kwenda fainali itakayopigwa kwenye Uwanja wa Wembley, mwezi ujao.
Ujerumani inaonekana kuwa na faida ya kuigiza timu mbili kwenye hatua ya nusu fainali, likiwa ndiyo taifa pekee ambalo limeweza kufanya hivyo baada ya Bayern na Dortmund kupenya, lakini zinatakiwa kufanya kazi kubwa kwa kuwa zinacheza na wapinzani tofauti.
Huu hapa ndiyo ubora, wachezaji pamoja na viwango vya timu hizo zilizokwenda nusu fainali itakayopigwa Aprili 30-Mei 1 na Mei 8-7.
Bayern München (Ujerumani)
Hii ni timu ambayo haiwezi kuwa imeingia hapa bahati mbaya ikiwa inashika nafasi ya pili kwenye ubora wa UEFA, imepangwa kuvaana na Real Madrid kwenye nusu fainali.
Msimu uliopita ilitolewa robo fainali na Manchester City ambayo baadaye ilitwaa ubingwa.
Pamoja na mafanikio ya msimu huu, Bayern ina rekodi nzuri kwenye michuano ya Ulaya ikiwa imetwaa ubingwa mara sita msimu wa 1973/74, 1974/75, 1975/76, 2000/01, 2012/13, 2019/20, sasa inamtegemea zaidi mshambuliaji wake Harry Kane.
Kocha wa timu hiyo, Thomas Tuchel ana rekodi nzuri kwenye michuano hii akiwa ameshatwaa ubingwa huu mwaka 2021 akiwa na Chelsea, sasa anatafuta ubingwa wa kwanza wa Ulaya na Bayern.
Dortmund (Ujerumani)
Hii ndiyo timu ya chini zaidi ambayo imefanikiwa kufika hatua ya nusu fainali kwenye michuano hii msimu huu, ikiwa inashika nafasi ya 13 kwenye ubora wa UEFA.
Ilifika hapa baada ya kuitupa nje Atletico Madrid kwenye hatua ya robo fainali ambapo msimu uliopita ilitolewa kwenye hatua ya 16 bora na Chelsea, mafanikio yao makubwa kwenye michuano hii ni ubingwa wa msimu wa 1996/1997.
Dortmund inakutana na PSG ambayo ilikuwa nayo kwenye hatua ya makundi hivyo ni timu zinazofahamiana na sasa zinakutana tena kwenye hatua muhimu ya michuano hiyo mikubwa.
Dortmund imetinga hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2012/13, ikiwa na kocha mtata Jürgen Klopp.
Edin Terzić amekuwa akipewa heshima kubwa nchini Ujerumani, lakini hana mafanikio kwenye Uefa na sasa anataka kuweka rekodi mpya huku akimtegemea mkongwe Julian Brandt, ambaye ameshacheza zaidi ya michezo 40 ya michuano hiyo.
Paris Saint-Germain (Ufaransa)
Hii ni timu ambayo mara nyingi inapewa nafasi kubwa ya kufanya mambo makubwa lakini mwishoni inashindwa kufurukuta baada ya kuishia njiani mara kadhaa.
PSG ikiwa na Kylian Mbappe imefanikiwa kuingia nusu fainali kwa kuwatupa vigogo Barcelona nje, ikiwa inashika nafasi ya nne kwa ubora wa Uefa.
Msimu uliopita ikiwa na timu bora ilitupwa nje hatua ya 16 Bora na Bayern Munich na msimu huu inarudi palepale Ujerumani.
PSG imefuzu hatua ya nusu fainali kwa mara ya tatu ndani ya misimu mitano na itakuwa hamu kubwa kwa Mbappe kutwaa ubingwa huu kabla hajaondoka kwenye timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Luis Enrique ndiye kocha wa PSG akiwa na uzoefu mkubwa kwenye michuano hiyo lakini akiwa ameshatwaa ubingwa mara moja sasa wanakwenda kuvaana na Borrusia Dortmund hatua ya nusu fainali.
Real Madrid (Hispania)
Real Madrid pamoja na ubora wake wa nyuma msimu huu ilikuwa haipewi nafasi kubwa ya kufika hapa ilipo, lakini ubora wa wachezaji wake na mafanikio ya kocha wao Carlo Ancelotti yamesaidia kuitupa nje Manchester City.
Madrid kwenye viwango vya Uefa inashika nafasi ya tatu na ilifika hapa baada ya kuitupa timu inayoshika nafasi ya kwanza Manchester City kwenye hatua ya robo fainali ikiwa inalipa kisasi baada ya City kuitupa nje msimu uliopita kwenye nusu fainali.
Ikiwa na kijana mdogo Jude Bellingham, Madrid ambayo imetwaa ubingwa huu mara 14 inakwenda kwenye mechi hii ikiwa inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na kuwa na kikosi chenye mchanganyiko, wakongwe na damu changa na sasa anakwenda kuvaana na Bayern yenye njaa ya mafanikio. Hawa ndiyo wapinzani wakubwa kwenye michuano hii.