Wachezaji Gambia wanasurika kifo wakienda Afcon
Ndege ya Air Cote d'Ivoire iliyokuwa imewabeba wachezaji wa timu ya Taifa ya Gambia
Muktasari:
- Kikosi cha wachezaji wa timu ya Taifa ya Gambia kikijumuisha viongozi wa timu hiyo, kimenusurika kifo baada ya ndege waliokuwa wakisafiria Ivory Coast kushikiri michuano ya Afcon kukosa hewa ya oksijeni muda mchache baada ya kuruka angani
Banjul. Msafara wa wachezaji na viongozi wa timu ya Taifa ya Gambia uliokuwa ukielekea Ivory Coast kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023; umenusurika na vifo baada ya kukosa hewa ya oksijeni kwenye ndege yao.
Kocha wa timu hiyo, Tom Saintfiet aliyewahi pia kufundisha klabu mbalimbali katika Bara la Afrika ikiwamo Yanga ya Tanzania ameiambia BBC kuwa ndege ya Air Cote d'Ivoire iligeuka dakika tisa tu baada ya kuondoka katika Mji Mkuu wa Gambia, Banjul.
Kwa mujibu wa tovuti ya BBC iliyoweka habari hiyo leo Alhamisi Januari 11, 2024, ukosefu wa oksijeni ndani ya ndege hiyo, ulisababisha wajumbe wengi wa msafara huo kusinzia.
Hata hivyo, Saintfiet alisifu hatua za haraka za usalama zilizochukuliwa na rubani wa Air Cote d'Ivoire.
“Wahudumu wa eneo hilo walisema kulikuwa na tatizo la kiyoyozi kabla hatujaondoka lakini kila kitu kitakuwa sawa tutakapoondoka,” amesema Saintfiet akizungumza na BBC michezo Afrika.
Saintfiet ameongeza kuwa, “baada ya dakika chache, kulikuwa na joto kali ndani ya ndege, sote tulilala kwa sababu ya ukosefu wa oksijeni, baadhi ya wachezaji hawakuweza kuamshwa, rubani alifanya uamuzi wa busara kutoendelea na safari.
Kocha huyo amesema watu walipata maumivu ya kichwa na endapo ndege hiyo ingeendelea na safari kwa dakika 30, timu nzima ingekufa.
“Jambo la kushangaza ni kwamba barakoa za oksijeni hazikutoka, tunamshukuru rubani aligundua kuwa hii ilikuwa hali mbaya na kuamua kuirejesha katika uwanja wa ndege, lakini bado tuko kwenye mshtuko,” amesema Saintfiet.
Timu ya Taifa ya Gambia ilifika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika miaka miwili iliyopita nchini Cameroon licha ya kuwa timu hiyo haikupewa nafasi kubwa na sasa inatarajiwa kumenyana na majirani zao Senegal siku ya Jumatatu katika mchezo wao wa ufunguzi.
Aprili 27 mwaka 1993 ndege ya kijeshi iliyokuwa inawasafirisha wachezaji, kocha na maofisa wengine wa timu ya Zambia wapatao 25, ilianguka katika Bahari ya Atlantic pwani ya Jiji la Libreville nchini Gabon na kuua abiria wote waliokuwamo.
Wachezaji hao walikuwa wakienda Senegal mjini Dakar kucheza mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 1994.