Wanne Dodoma kuikosa Simba

DODOMA Jiji ikiwa na furaha ya kupata ushindi wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara kwa kuifunga Geita Gold kwa bao 1-0, tayari ipo Dar es Salaam kwa pambano lao la leo dhidi ya Simba huku ikiwakosa wachezaji wanne ambao benchi la ufundi limesema mbadala wao upo. Simba itakuwa wenyeji wa Dodoma kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku kila moja ikiwa na matokeo matamu kwenye ligi hiyo.

Msimu uliopita Dodoma ilipoteza mechi zote mbili kwa Simba, ikifungwa nyumbani kwa bao 1-0 na kulala 2-0 ugenini na kujiandaa na mchezo huo kikosi hicho cha Kocha Djuma Masoud kitawakosa wachezaji wanne.

Daktari wa timu hiyo, Baraka Mipango aliwataja wachezaji watakaokosa mchezo huo wa kesho kuwa ni Augustino Nsata, Joram Mgeveke na Salumu Ngadu walio majeruhi, huku Rajabu Mgalula akiukosa kutokana na kufungiwa michezo mitatu.

“Salim Kihimbwa amepona ni jukumu la kocha kumpanga ama la,” alisema Dk Mpango huku Mgeveke alisema bado hajapona vizuri nyama za paja kutokana na kujitonesha katika michezo ya mwanzo wa msimu.