Watatu Simba kuikosa dabi ya Kariakoo
Muktasari:
- Simba ndiyo kinara wa Ngao ya Jamii, ikiwa imetwaa taji hilo mara kumi wakati Yanga ikitwaa mara nane.
Dar es Saalam. Simba imepata pigo kuelekea fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, baada ya kuthibitishwa kwamba nyota wake watatu muhimu, Jonathan Sowah, Alassane Kanté na Mohamed Bajaber, hawatakuwepo kwenye mchezo huo.
Upungufu huu unaweza kuathiri safu ya ushambuliaji na mipango ya kocha, hasa ikizingatiwa ukubwa wa pambano hilo la watani wa jadi linalotarajiwa kupigwa leo saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mshambuliaji mpya Jonathan Sowah, ataikosa mechi hiyo kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu uliopita wakati akiwa na Singida Black Stars.
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, mchezaji anapopata kadi nyekundu katika michezo ya FA anatakiwa kutumikia adhabu hiyo kwenye mechi zinazofuata za mashindano ya ndani, ikiwemo Ligi Kuu Bara, na pia Ngao ya Jamii.
Hii inamaanisha kwamba Sowah hataruhusiwa kushiriki mchezo huo wa ufunguzi wa msimu mpya.
Kukosekana kwake kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ni pigo kwa Wekundu wa Msimbazi ambao walihitaji nguvu ya kikosi chao kipya kuonyesha ubora dhidi ya watani wao wa jadi.
Wengine ni Bajaber na Kante ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kwa sababu ya majeraha waliyopata kwenye mechi za maandalizi ya msimu.
Katika mechi 20 zilizochezwa, miamba hii imekutana mara tisa. Simba imeibuka kidedea mara tano, huku Yanga ikipata ushindi mara nne.
Kwa ujumla, Simba ndiyo kinara wa Ngao ya Jamii, ikiwa imetwaa taji hilo mara kumi wakati Yanga ikitwaa mara nane.