Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wikiendi ya moto, burudani zimerejea

Muktasari:

  • Kwenye Ligi Kuu Bara kuna mechi moja tu kati ya Pamba Jiji iliyopanda daraja kutoka Ligi ya Championship ambayo itapambana na maafande wa Tanzania Prisons

Dar es Salaam. Moto utawaka: Ndivyo hali ilivyo wakati mwanzo mpya wa michuano mbalimbali ukianza rasmi leo Ijumaa.

Baada ya mapumziko marefu hatimaye leo timu kadhaa kubwa zinaanza kutafuta makombe ya ligi na mashindano mbalimbali zinazoshiriki.

Kwenye Ligi Kuu Bara kuna mechi moja tu kati ya Pamba Jiji iliyopanda daraja kutoka Ligi ya Championship ambayo itapambana na maafande wa Tanzania Prisons.

Mechi hiyo ya ufunguzi wa ligi hiyo kwa msimu wa 2024-2025, itapigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya kesho Jumamosi na keshokutwa Jumapili kupigwa michezo mingine minne ukiwamo wa Mnyama, Simba itakayoanza nyumbani dhidi ya Tabora United.

Pamba na Prisons zilizowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Muungano, zinafungua mwanzo wa karibu miezi 10 ya msimu mpya kwa timu 16 kuanza vita ya kusaka ubingwa unaoshikiliwa na Yanga kwa misimu mitatu mfululizo, sambamba na kusaka tiketi za kucheza michuano ya kimataifa kwa mwaka 2025-2026.

Mechi hiyo inazikutanisha timu zilizowahi kutamba katika soka la Tanzania miaka ya 1990.

Pamba imepanda daraja msimu huu itawaalika Prisons ambao kwa pamoja mastaa wao watakuwa wakisaka rekodi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mchezaji atakayefunga bao la kwanza la msimu endapo timu hizo zitafungana.

Msimu uliopita Elius Maguri ndiye alikuwa mchezaji wa kwanza kupachika bao akifunga dakika ya tano na rekodi hiyo ilimfanya amalize msimu na bao hilo moja.

Pamba licha ya ugeni wao kwenye ligi msimu huu wamefanya usajili mkubwa ambao unatoa picha kwa Tanzania Prisons kujiandaa kwenda kukabiliana na mastaa kama George Mpole ambaye msimu wake wa mwisho kucheza Ligi Kuu Bara 2021-2022 alifunga mabao 17 na kuibuka mfungaji bora akiwa na Geita Gold kabla ya kushuka daraja.

Kwa upande wa Prisons ambayo ilimaliza nafasi ya tisa kwenye msimamo ikikusanya pointi 34 wao wana faida ya Ismail Ally, Haruna Chanongo wote viungo ambao walicheza Pamba msimu ulioisha wakiipandisha baada ya kuwasajili wakiwa wachezaji huru.

Pamba watatakiwa kuwachunga wachezaji hao kutokana na kuifahamu timu hiyo na msimu huu watakutana na Pamba wakiwa Tanzania Prisons ambayo imewasajili dirisha lililoisha jana.


Wikiendi ya moto

Baada ya mchezo huu, Ligi Kuu Bara itaendelea tena kesho Jumamosi ambapo timu ya Mashujaa ya Kigoma itaingia kwenye msimu wake wa pili mfululizo ikivaana na Dodoma Jiji.

Mashujaa inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na mastaa wengi wapya kama Ally Nassoro 'Ufudu', Yusuph Dunia, Robert Mackidala, Ismail Mgunda, Jaffary Kibaya na Mohamed Mussa ambaye alijiunga akitokea Simba.

Lakini watakutana na moto wa Dodoma Jiji ambayo ipo chini ya kocha mkongwe Mecky Maxime lakini ikiwa na mastaa wapya ambayo itawatengemea kesho Alain Ngeleka, Waziri Junior, Dickson Mhilu na Reliants Lusajo ambao wanapewa nafasi kubwa ya kufanya mambo mazuri msimu huu.

Hata hivyo, mashabiki wanasubiri kama Wazir Junior ambaye alimaliza msimu uliopita na mabao 12 akiwa na KMC ataendeleza kasi yake ndani ya timu mpya ya Dodoma.

Mechi nyingine ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa wenyeji Namungo watavaana na Fountain Gate ikiwa ni mechi ya kwanza ya ufunguzi kupigwa usiku ambapo itaanza saa 1:00.

Namungo ambayo haikufanya vizuri msimu uliopita itaingia ikiwa na sura ngeni kama kipa Beno Kakolanya, Djuma Shabani, Raphael Daud, Lenny Kisu, Amade Momade, Erick Molongi na Moubarack Amza.

Mashabiki wamekuwa wakiisubiri kwa hamu timu hiyo yenye wakongwe wengi wakati itakapovaana na Fountain ambayo imeingiza zaidi ya wachezaji 20 wapya.

Baadhi wanaosubiriwa kuwika zaidi ni John Noble, Aron Lulambo, Patrick Lembo, Seleman Mwalimu na Shafik Batambuze.


Simba mpya KMC

Mashabiki Jumapili watakuwa kwenye Uwanja wa KMC uliopo Mwenge kuitazama Simba ambayo bado inatafuta muunganiko ikivaana na Tabora United kwenye mchezo wa kwanza wa ligi.

Simba ambayo ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya tatu kwenye ligi itaingia kwenye mchezo huu wa kwanza wa ligi ikiwa na sura kadhaa mpya, likiwemo benchi la ufundi chini ya Fadlu Davids.

Mastaa wapya wanaosubiriwa kwa hamu kwenye mchezo huu ni Joshua Mutale, Steven Mukwala, Charles Ahoua, Augustine Okejepha na kipa Moussa Camara.

Huku Tabora ikiwa na maingizo mapya wakiwemo Heritier Makambo, Yacouba Songne, Victor Sochima, Enyinnaya Kazie Godswill na Shedrack Asiegbu ambao wanatarajiwa kuisumbua safu ya ulinzi ya Simba.


Cecafa

Simba Queens itaingia uwanjani Jumapili kuvaana na FAD ya Djibout nchini Ethiopia ikiwa inaanza kasi ya kutafuta ubingwa huu ambao msimu uliopita ulichukuliwa na JKT Queens.

Ubingwa hapa utawafanya Simba Queens washiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Ligi ya Mabingwa Afrika

Pamoja na mechi za Ligi Kuu Bara, pia kesho Jumamosi wananchi Yanga wataingia uwanjani kucheza mchezo wa hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O ya Burundi, mechi itakayopigwa saa 10:00 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa Yanga mpya ambayo imesajili mastaa kadhaa wakubwa, akiwemo Clatous Chama kutoka Simba, Jean Baleke, Chadrack Boka na Prince Dube.

Mashabiki wanausubiri mchezo huu ili kuona kama Yanga ambayo msimu uliopita ilifanya vizuri na kuishia hatua ya robo fainali inaweza kusogea mbele zaidi ya hatua hiyo, ikiwa imefanya vizuri kwenye michezo yake ya maandalizi ya msimu na kuanza kwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuwachapa Azam FC mabao 4-1.

Hata hivyo, wanasubiri upinzani kwa Vital’O, ambayo haina historia kubwa kwenye michuano ya Ulaya, lakini ikiwa na faida ya kutazama mechi zote kubwa za Yanga zilizopigwa hapa nchini.

Baada ya mechi hiyo, Azam itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex kuivaa APR ya Rwanda kwenye mchezo mwingine wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, zikiwa ni timu ambazo zinafahamiana zaidi.

APR tayari imeshacheza michezo kadhaa hapa nyumbani baada ya kufika fainali ya Kombe la Kagame, lakini baada ya hapo ilirejea tena nchini kuvaana na Simba kwenye mchezo wa Simba Day na hivyo Azam watakuwa wameshaitazama na kujua inavaana na timu ya namna gani.

Hivyo kwa Azam ambayo ilikwenda Rwanda kufanya tamasha lao na kucheza mchezo wa kirafiki jambo ambalo limewapa pia upenyo APR na kufahamu inakwenda kucheza na timu gani kwenye mchezo utakaopigwa saa 12:00 jioni keshokutwa Jumapili.

Kwa upande wa JKU watakuwa ugenini Misri kukipiga dhidi ya Pyramids lakini wakisomeka kama wenyeji baada ya kuamua michezo yao yote ipigwe nchini humo.


Kombe la Shirikisho Afrika

Uhamiaji ya Zanzibar, Jumapili itakuwa uwanjani kuvaana na Tripoli ya Libya mechi itapigwa saa 9:00 nchini Libya, ukiwa ni mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika, wakati pia Bravos watakuwa nyumbani kukipiga na Coastal Union ikiwa ni michezo ya awali ya michuano hiyo.


Ulaya napo kwa moto

Leo Manchester United itakuwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Old Trafford saa 4:00 usiku, kuvaana na Fulham kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England.

United inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa na hasira ya kushindwa kutwaa Ngao ya Jamii mbele ya Machester City wikiendi iliyopita.

Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa ligi hiyo ambapo michezo mingine ya ligi hiyo inatarajiwa kupigwa kesho Jumamosi ambapo Arsenal ambayo msimu uliopita ilimaliza nafasi pili itavaana na Wolves ikiwa nyumbani, Liverpool ambayo haijafanya usajili wowote mkubwa itakipiga dhidi ya wageni Ipswich Town, Everton watacheza na Brighton, Newcastle itacheza na Southampton, Nottigham Forest dhidi ya Bournemouth huku West ikikipiga na Aston Villa nyumbani.

Jumapili zitapigwa mechi mbili, lakini kali kuliko zote ni ile ya Chelsea ambayo imefanya usajili wa kundi kubwa la wachezaji itakayovaana na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Manchester City saa 12: 30 jioni.


Serie A

Kesho Jumamosi kipute cha Ligi Kuu Italia kitaanza wakati ambapo mchezo wa mapema zaidi utakuwa kati ya mabingwa watetezi Inter Milan ambapo watavaana na Genoa, huku mechi nyingine ya saa 1:30 usiku, ikiwa kati ya Parma ambao wataikaribisha Fiorentina.

AC Milan watacheza dhidi ya Torino huku Empoli wakivaana na Monza, mechi za Jumapili ni Verona na Napoli, Bologna na Udinese, Gagliari dhidi ya Roma huku Lazio wakikipiga na Venezia.


La Liga

Hii ni Ligi Kuu ya Hispania ambayo ilianza rasmi jana, lakini leo kutakuwa na michezo miwili Celta Vigo watavaana na Alaves huku La Palmer wakiwa nyumbani kukipiga na Sevilla kuanza mwanzo mpya wa ligi hiyo ambayo ubingwa wake unashikiliwa na Real Madrid.