Yanga dah! yapigwa bao jioni sasa yageukia nje...

Monday December 27 2021
yangapic
By Faudhia Ramadhani
By Eliya Solomon

MABOSI wa Yanga walikuwa ameanza kupumua baada ya dili lao la kumnyakua kipa chipukizi mwenye kipaji kikubwa, Abdultwalib Mshery kutoka Mtibwa Sugar, likionekana kutiki, lakini ghafla mambo yamegeukia kutokana na vigogo wa Manungu kuchomoa kumuachia kipa huyo.

Yanga ilikuwa ikiamini Mshery ndiye kipa sahihi wa kuibeba timu yao wakati kipa namba moja, Diarra Djigui atakapoenda na timu yake ya taifa ya Mali kwenye Fainali za Afrika (Afcon) yanayoanza mwezi ujao na ilikuwa imefikia hatua nzuri kwenye dili hilo kabla ya kutibuka dakika za mwisho.

Kabla ya kumfuata Mshery kupitia wakala wake na mchezaji huyo kukaririwa kama mabosi wake watamruhusu yeye anaweza kucheza kokote, ingawa hakutaka kuzungumzia dili hilo kwa vile bado ana mkataba mrefu na timu hiyo ya Manungu, Yanga ilikuwa ikiwapigia hesabu makipa wa Ruvui Shooting, MOhammed Makaka na yule wa Mbeya City, Haruna Mandanda.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga na Mtibwa zinasema dili la Mshery limekufa na kwamba hawezi kutua Jangwani, licha ya awali Yanga kupewa sharti ya kuuvunja mkataba wake Manungu kwa kulipa Sh 20 Milioni kabla ya kukubaliana kimasilahi na kipa huyo kijana.

Yanga ilishamuandalia Mshery mkataba wa miaka miwili wenye donge nono, lakini kauli ya mmoja wa vigogo wa Mtibwa kwa kuiambia Yanga ‘Mshery hauzwi’ imewanyong’onyesha.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alipendekeza usajili wa Mshery kutokana na kuvutiwa na kiwango chake na aliwapa jina hilo mabosi wake.

Advertisement
Advertisement