Yanga, Singida FG mechi ya pointi muhimu

Dar es Salaam. Mwenendo na kiwango kisichoridhisha ambacho imekuwa ikikionyesha siku za hivi karibuni, ni mambo yanayoifanya Singida Fountain Gate kutoonekana kikwazo kikubwa kwa Yanga wakati timu hizo zitakapokutana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba leo kuanzia saa 10:00 jioni.

Safu ya ushambuliaji ya Singida Fountain Gate imeonekana kupoteza makali katika miezi ya hivi karibuni kama ilivyo ile ya ulinzi kutokana na makosa ya mara kwa mara ambayo zimekuwa zikifanya jambo ambalo limekuwa likichangia muendelezo wa kufanya vibaya katika mechi zake hivi sasa kulinganisha na ilivyoanza msimu.

Timu hiyo katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu, imeibuka na ushindi mara moja tu, huku ikitoka sare katika mechi tatu na imepoteza michezo sita, ikifunga mabao sita na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.

Hali ni tofauti kwa Yanga ambayo inaonekana haipo kileleni mwa msimamo wa Ligi kwa bahati mbaya kutokana na mfululizo wa matokeo mazuri ambayo imekuwa ikiyapata katika mechi za ligi lakini hata mashindano mengine.

Uthibitisho wa hilo unaonekana katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu ambazo Yanga imeibuka na ushindi mara nane, kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja, ikifumania nyavu mara 20 na nyavu zake zikitikiswa mara tano tu.

Mwenyeji Singida Fountain Gate imekuwa haina historia nzuri dhidi ya Yanga na endapo itapata ushindi leo, itakuwa angalau imefuta machozi ya unyonge iliyonayo dhidi ya vinara hao wa ligi kwani haijawahi kupata ushindi wala sare dhidi yao tangu ilipopanda Ligi Kuu.

Singida Fountain Gate imekutana na Yanga mara tatu katika Ligi ambapo imefungwa katika mechi hizo zote, ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane na yenyewe imefunga bao moja tu.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa wanaingia katika mechi hiyo wakiwa na lengo la ushindi tu.

 "Tunahitaji kufanya kila liwezekano kushinda mataji yote ambayo tumebakiza. Yanga inahitaji kushinda na mimi kama kocha naamini katika hatua kwenye kila mchezo na kesho (leo) tunahitaji ushindi ili kwenda mbele zaidi," alisema Gamondi.

Kocha msaidizi wa Singida FG, Ngawina Ngawina alisema kuwa wamejiandaa vyema kwa ajili ya mechi hiyo.

"Tunajua timu ya Yanga ina ubora tunaiheshimu tutakwenda na tahadhari kubwa lakini naamini mwenye maandalizi mazuri atapata matokeo. Wachezaji wote wako katika hali nzuri yeyote atakayepata nafasi atatufanyia kazi nzuri," alisema Ngawina.

Katika Uwanja wa Kassima Majaliwa huko Ruangwa, Lindi, Namungo FC itaikaribisha Azam FC katika mchezo ambao mbali na hesabu ya kuwania pointi tatu, kila timu itakuwa na hamu ya kulipa kisasi kwa mwenzake kutokana na kilichowahi kutokea nyuma baina yao.

Mwenyeji Namungo FC itakuwa na hamu ya kulipa kisasi cha kupoteza nyumbani mechi zake mbili zilizopita za Ligi dhidi ya Azam ambapo moja ilifungwa bao 1-0 na kabla ya hapo katika msimu wa 2021/2022 ilipoteza kwa mabao 2-1.

Azam FC yenyewe itakuwa na hamu ya kulipa kisasi baada ya kutopata ushindi hata sare dhidi ya Namungo FC katika mechi zake mbili zilizopita za Ligi Kuu, ya kwanza ikiwa ni ya mzunguko wa kwanza wa ligi msimu huu ilipochapwa mabao 3-1 na kabla ya hapo ilifungwa mabao 2-1 katika mechi ya mwisho baina yao msimu uliopita.

Mchezo huo baina ya Namungo FC na Azam FC utachezwa kuanzia saa 1:00 usiku ambapo timuu mwenyeji ikipata ushindi itafikisha pointi 26 wakati timu ngeni ikishinda itafikisha pointi 50 ambazo zitaiweka katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.