Yanga, TFF kuanza upyaaa!

Yanga, TFF kuanza upyaaa!

Muktasari:

  • KIKAO cha zaidi ya saa tatu kimezika rasmi mgogoro baina ya klabu ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pande hizo mbili zimekubaliana kuanza upyaa!

KIKAO cha zaidi ya saa tatu kimezika rasmi mgogoro baina ya klabu ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pande hizo mbili zimekubaliana kuanza upyaa!

Kikao hicho kilichofanyika Jumatatu baada ya serikali kuzitaka pande hizo mbili kukaa ili kumaliza tofauti zao kufuatia malalamiko ya Yanga dhidi ya TFF.

Yanga ilipeleka malalamiko hayo wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wiki iliyopita na Wizara kuwaita TFF pia kabla ya kuwataka wakutane Jumatatu iliyopita na kumaliza sintofahamu hiyo.

Baada ya kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya TFF, Karume jijini Dar es Salaam, pande zote ziligoma kuzungumza kilichojadiliwa, Yanga ikiongozwa na mwenyekiti wake, Dk Mshindo Msolla.

Jana mmoja wa viongozi wa klabu hiyo aliyeomba hifadhi ya jina kutokana na makubaliano ya kikao hicho, alisema TFF ilikiri baadhi ya mambo kutoyafanyia kazi kwa wakati ikiwamo suala la Bernard Morrison kwenda kamati ya nidhamu.

“Kingine walichokiri ni suala zima la kutukata pesa bila ya kutupa taarifa na wametuahidi jambo hilo halitajirudia tena, kwani walikuwa wanatuwekea pesa kwenye akaunti lakini unakuta wamekata kama sio Milioni tatu, basi mbili au yoyote wanayojisikia wao kukata,”.

“Tukihoji tunaambiwa tunadaiwa kuna wachezaji wanatudai, ila kwa kuwa wameomba tuyamalize na tugange yajayo hata sisi Yanga tumekubali kwani lazima maisha yaendelee,” alisema.

Alisema kikao hicho kilimalizika vizuri na kila upande ukatoka una amani na TFF imewaomba kusahau yaliyopia na wasonge mbele.

“Unafahamu mambo tuliyokuwa tukifanyiwa na TFF yalituumiza sana, hivyo kikao cha Jumatatu kimekuwa na matokeo chanya na wametueleza kama tunaona jambo haliendi sawa kuwe na mawasiliano,” alisema kigogo huyo wa Yanga.

Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo alipoulizwa juu ya kikao hicho alisema hafahamu lolote.

“Sijapewa taarifa zozote juu ya hilo, hivyo siwezi kulizungumzia, labda uulize ofisi ya katibu mkuu.

Katibu Mkuu, Wilfred Kidao alipotafutwa hakupatikana huku msaidizi wake, Mohammed Mkangara akisema hawezi kuzungumzia kikao hicho kwa kuwa yeye si msemaji wa shirikisho.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo alisema;

“Wenye kuzungumzia kilichojiri ni TFF na Yanga, sisi tunasubiri taarifa ya kikao chao, lengo la kuwakutanisha ilikuwa waelewane na kumaliza tofauti zao,”

Alisema bado hajaiona taarifa hiyo, ila serikali ilitaka ni pande hizo mbili kumaliza tofauti hasa kutoaminiana.