Yanga vs Simba; hii huwezi kuikuta sehemu nyingine

MWAKA 2012, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka Kusini mwa Jangwa la Sahara, Ashford Mamelodi aliniomba nimuandikie habari nzuri kuhusu mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga, baada ya kushuhudia utamaduni wa kipekee wa mashabiki kila mara alipobahatika kuzuru nchini.

Kwake Mamelodi, utamaduni wa mashabiki wa Simba na Yanga ni wa kipekee kwa kuwa, hauhusishi vurugu, ugomvi, fujo wala uhalifu, bali huchochea upinzani wa jadi wa kirafiki, umoja na ari ya ushindani ambayo ni muhimu katika michezo na zaidi amani ya nchi.

“Hii huwezi kuikuta sehemu nyingine yoyote duniani,” alisema Mamelodi baada ya kueleza alivyoona mashabiki waliovalia sare nyekundu na nyeupe wakitoka uwanjani, huku wakipiga gumzo pamoja na mashabiki waliiovalia sare za rangi ya njano na kijani.

“Hiki ni kitu cha pekee. Hebu fanya hivi. Andika habari moja kuhusu mechi hizi za Simba na Yanga, na hasa tabia za ushiriki wa mashabiki kabla na baada ya mechi ili tuwape Fifa waichapishe kwenye jarida lao. Natumaini hii habari itapendwa na wengi.”

Ni mambo ambayo nilikuwa nayaona kila wakati na kuyachukulia kuwa ya kawaida, kumbe yana thamani kubwa kwa wengine, na nilipokaa chini kufanya utafiti kabla ya kuandika ndipo nilipogundua kuwa utamaduni wa mashabiki hao wa klabu za Kariakoo si wa kawaida.

Mamelodi ambaye ni raia wa Botswana ana rekodi nzuri ya ushabiki wa mechi kubwa za eneo moja, zikianzia Afrika Kusini ambako Kaizer Chiefs wana upinzani mkubwa na Orlando Pirates, ambao kabla ya mwaka 2010 ulikuwa unaishia kwenye fujo.

Vurugu kubwa zaidi ni katika mechi za vigogo wa Cairo nchini Misri, ambako wababe wa soka Afrika, Al Ahly na vigogo wengine, Zamalek hupambana. Mara kadhaa mechi baina ya vigogo hao huahirishwa na vurugu zinapotokea mashabiki wengi hujeruhiwa. Wakati fulani mechi hizo huchezeshwa na waamuzi kutoka nje. Mechi nyingine za timu kutoka eneo moja (derby) zenye vurugu ni Galatasaray v Fenebahce (Uturuki); Boca Juniors v River Plate (Argentina); Palermo v Catania (Italia), Rangers v Celtic (Scotland); West Ham v Millwall (England) na Red Star v Partizan Belgrade za Serbia.

Lakini Simba na Yanga zinapokutana, pambano hilo huwa ni kama tamasha kwa wapenzi wa soka na michezo kote nchini, licha ya kutotanguliwa na shughuli za burudani kama ilivyo kwa mechi nyingine kubwa za barani Ulaya, hasa Ujerumani ambako kila mechi hunakshiwa na burudani.

Ukiacha usafiri unaoandaliwa na mashabiki wa timu, wengi wanaoenda kwa kutumia mabasi ya kawaida au gari ndogo binafsi kwenda uwanjani huenda pamoja bila ya kujali tofauti zao. Kwenye maeneo yaliyo karibu na Uwanja wa Benjamin Mkapa au kokote ambako wababe hao hukutana (Mwanza, Arusha au Zanzibar), baa hujaa mashabiki waliiovalia rangi za timu hizo na mijadala huwa ya sauti kubwa kuelezea matarajio ya matokeo.

Pikipiki nyingi huwa zimebeba watu waliovalia fulana za rangi ya timu hizo mbili. Na hii si wakati wa kwenda uwanjani tu, bali hata wakati wa kurudi nyumbani; hawafarakani baada ya timu moja kufungwa.

Hata hivyo, ni wachache wanaoendeleza utamaduni wa zamani wa kutimiza ahadi zao iwapo matokeo yanakwenda kinyume na walivyotamba. Wapo ambao zamani walikubali kunyolewa nywele zote kwa wembe baada ya timu yake kushindwa, wapo waliowapelekea zawadi wapinzani wao, wapo waliokubali kumwagiwa vumbi na vitimbi vingine vingi.

Pengine ni kutokana na maendeleo ya teknolojia na ustaarabu baadhi ya vitu hivyo havifanyiki katika dunia ya sasa.Ni nadra sana mashabiki wa klabu hizo zilizoigawa nchi mara mbili kupambana mwilini wakati wa mechi baina yao, lakini imetokea mara kadhaa mashabiki hao kuchapana wakati wa mechi dhidi ya timu nyingine. Shabiki moja wa Yanga alikutana na kipigo kutoka kwa watu walioaminika kuwa ni mashabiki wa Simba jijini Mwanza wakati timu yake ilipokwenda kucheza na Mbao.

Klabu hizo zimewahi kufungiwa kwa muda na serikali kutumia Uwanja wa Mkapa baada ya kufanyiana fujo wakati timu zao zikishiriki michuano ya klabu ya Afrika.

Vurugu hizo hutanguliwa na tabia ya kushangilia timu kutoka nje na hata kuipokea inapokuja Tanzania.

“Huwezi kuona kitu hicho popote duniani,” alisema Muingereza Joel Green, ambaye alishuhudia mashabiki wa Simba wakishangilia baada ya Yanga kufungwa mabao 2-0 na Atletico ya Burundi katika michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2012.

“Kwanza nilidhani ni mashabiki kutoka Burundi, lakini kama ni mashabiki wa Simba, inashangaza. Ni mashabiki wa aina gani hawa?” Lakini hiyo ndio burudani ya mashabiki hao. Kitendo kibaya zaidi ni kile cha mashabiki wa Yanga cha mwaka 1993 kuamua kuishangilia Stella Abidjan ya Ivory Coast katika mechi ambayo Tanzania ingeweza kutoa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa michuano ya klabu Afrika. Simba ililazimisha sare jijini Abidjan na hivyo ilitakiwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kuweza kutwaa Kombe la CAF. Lakini Boli Zozo alifunga bao la kwanza kipindi cha kwanza na aliporejea kipindi cha pili akafunga bao la pili na kuamsha shangwe kutoka Yanga, ambao baadaye walisema “uzalendo uliwashinda”.

Kutokuwa na uadui hakumaanishi kuwa mashabiki hao hawana adui. Adui wao wa kwanza kabisa ni wasimamizi wa mechi, yaani Shirikisho la Soka (TFF) au zamani Chama cha Soka (FAT). Mwaka 1994, mashabiki waliwahi kurusha vitu kuelekea jukwaa kuu, ambako alikuwepo Rais Ali Hassan Mwinyi.

Waliamini kuwa mwamuzi wa mchezo aliyepangwa na FAT wakati huo, alipewa maelekezo aipendelee Simba. Hasira zao zilivuka kikomo wakati Madaraka Seleman alipoonekana ameugusa mpira kwa mkono kabla ya kufunga bao. Hapo matusi na vurugu vililipuka hadi polisi walipoingilia kati. Yanga alilala 4-1.

Hali ilikuwa tofauti mwaka 2016 wakati mashabiki wa Simba walipohamishia hasira zao dhidi ya refa Martin Saanya baada ya kukataa goli lililofungwa na Ibrahim Ajibu na kukubali la Amis Tambwe aliyeonekana kama ameunawa mpira kabla ya kufunga. Mechi hiyo iliisha kwa sare.

Wakati wakongwe wenzao AFC Leopards, Gor Mahia (Kenya), Sports Club Villa na Express za Uganda si wababe tena katika soka la nchi hizo, lakini Simba na Yanga zinaendeleza ubabe na ndizo zenye ushindani mkubwa katika kinyang’anyiro cha ubingwa, zikiwa zimetwaa ubingwa kwa ujumla mara 50, zikiacha klabu za Mseto, Pan African, Mtibwa Sugar, Coastal Union, Tukuyu Stars na Azam pekee kuonja taji hilo. Yanga, ambayo kesho inaingia ikiwa bingwa mtetezi, imetwaa mara 28 wakati Simba, iliyopokonywa ubingwa mwaka jana, imetwaa mara 22. Rekodi hizo pekee zinatosha kuzifanya klabu hizo mbili kuwa na ukubwa usiomithilika katika soka la Tanzania na hivyo kukusanya mashabiki wengi pengine kuliko klabu nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki au sehemu kubwa ya Afrika.

“Ni kitu kizuri kwa soka la Tanzania,” alisema kocha wa taifa wakati huo nikiandika mara ya Fifa, Kim Poulsen nilipomuuliza kuhusu mashabiki wa klabu hizo. “Unajua mashabiki wanaweka presha kwa wachezaji, kwa hiyo wanafanya jitihada kubwa wakati wanapocheza Dar es Salaam.”

Kama kawaida, kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa utafurika mashabiki wakiwa na matarajio tofauti; Simba wakitaka kuondoa unyonge kwenye ligi kwa Yanga na kuendeleza mazuri ambayo kocha Juma Mgunda ameanza nayo ndani na nje ya nchi, huku Yanga ikipania kuwafuta machozi mashabiki wao baada ya kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Kelele za maofisa habari wa klabu hizo, usajili wa wachezaji wageni wanaotamba kama Fiston Mayele na Aziz Ki kwa Yanga na Moses Phiri na Augustine Okrah kwa Simba kunazidisha kiwewe kwa mashabiki na kuifanya mechi iwe na mvuto wa kipekee. Ngoja tusubiri dakika 90 tuone soka.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa TFF