Yanga wajazwa mkwanja, wawekwa kambini chini ya ulinzi

Wednesday July 21 2021
yanga pic
By Mwandishi Wetu

YANGA walitua jijini Dar es Salaam juzi wakiwa na bashasha ya aina yake baada ya kukuta akaunti zao zimetuna.

Kikosi hicho kilitokea Dodoma walikotoka suluhu na Dodoma Jiji kwenye mchezo wa kukamilisha msimu.

Lakini jana wakakumbana na sapraizi ya aina yake Dar baada ya kuambiwa kwamba mkwanja wao wa Sh500 milioni walioahidiwa kwa kuifunga Simba umeingizwa.

Jambo hilo lilifanya baadhi yao kufikia kwanza kwenye benki moja maarufu na kufanya miamala kadhaa kabla ya kuunganisha kambini Avic kujiandaa na mechi dhidi ya Simba Jumapili ijayo mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

Baada ya kuwasili wachezaji hao wakiwa na ulinzi mkali walifika moja kwa moja kwenye benki inayotumiwa na klabu hiyo na walijikuta wamenona wakiwa wameingiziwa mgawo wao na Bilionea wao, Ghalib Mohamed maarufu kama GSM ambao ni miongoni mwa wadhamini wa Yanga.

Mzuka wa mamilioni hayo utawaongezea ari na sasa wataishi na ahadi nyingine kubwa kutoka kwa Ghalib alipowaambia wiki moja iliyopita kwamba kama wakimuua tena Mnyama kuna mzigo mwingine mkubwa kushinda huo.

Advertisement

Asilimia kubwa ya wachezaji waliocheza mechi hiyo wamejikuta wakiambulia sio chini ya Sh19 milioni na hata wafanyakazi wa kambini nao wamepewa mkwanja kiasi chao.

Jana wachezaji hao walionekana wakitoka benki na ulinzi wa makomandoo ukiwa nje wakihakikisha hakuna anayepotea njia kutokana na kibarua cha Jumapili cha fainali ya Shirikisho. Baada ya shughuli hiyo mabasi mawili yalielekea kambini Avic tayari kwa kambi fupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea Kigoma.

Advertisement