Yanga yashtua

Saturday June 05 2021
YANGA PIC
By Clezencia Tryphone

MASHABIKI wa soka nchini wameanza kutambiana huko mitaani kuelekea pambano la watani, Simba na Yanga lililopangwa kufanyika Julai 3 baada ya awali kuahirishwa kitatanishi, lakini juzi wameshtusha baada ya kuzagaa kwa taarifa kwamba Jangwani wamepanga kuugomea mchezo huo.

Jambo hilo limewashtushwa wadau wengi, wakiwamo mabosi wa Bodi ya Ligi (TPLB) waliodai hawajui kitu kitakachosababisha mchezo huo usipigwe tena kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam

Awali, mtanange huo ulipangwa kupigwa Mei 8 na kuahirishwa baada ya kuwepo kwa agizo la TFF kusogeza mbele kwa saa mbili ambazo Yanga waliingia uwanjani na kuondoka na baadaye Simba waliingia na wao na kuondoka baada ya kutangazwa kuahirishwa kwa mchezo huo.

Hata hivyo, juzi kuna clip ilizagaa mtandaoni zikionyesha Mkuu wa Idara ya Habari Hassan Bumbuli akisema wazi wazi kuwa hawaitambui mechi hiyo na wanachokifahamu wao ni kwamba wamebakiza mechi nne tu kumaliza msimu.

“Sisi mpaka sasa tumebakiza michezo minne tu ambayo ni Ruvu Shooting, Dodoma Jiji, Mwadui na Ihefu mechi na Simba tushacheza Mei 8. Hizo ndizo mechi zetu za kwenye ratiba,” alikaririwa Bumbuli, hata hivyo hakuna kiongozi wa juu wa Yanga aliyepatikana kuthibitisha kama huo ni msimamo rasmi wa Yanga ama la, kwani simu za Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla na Kaimu Katibu Mkuu, Haji Mfikirwa zilikuwa zikiita bila kupokewa.

Hata hivyo, Mwanaspoti imepenyezewa taarifa kwamba uongozi huo wa Yanga umeshaandika barua ya kuukata mchezo huo kwa TPLB, ingawa Mwenyekiti wa Bodi, Steven Mnguto alipoulizwa jana alisema kwa kifupi, watashangaa kama Yanga haitapeleka timu uwanjani katika mechi iliyopangwa Julai 3, kwani walikuwapo katika kikao cha majadiliano na waliafiki kupangwa tarehe ya mchezo huo.

Advertisement

Mnguto alisema, Yanga kama wanaona kuna sintofahamu katika tarehe hiyo iliyopangwa waandike barua bodi ya Ligi ili waeleze shida nini ambayo inawafanya kutopeleka timu na sio kuongea tu katika mitandao. Hata hivyo Mwanaspoti linafahamu Yanga imeshaandika barua na Bodi walikuwa wakijipanga kuijibu.

“Sitaki kuliongelea sana jambo hilo, kwa sababu siku bado haijafika, siku ikifika halafu wakashindwa kuleta timu uwanjani ndio itajulikana itakuwaje kwa sababu soka lina kanuni zake. Ila ni kwamba baada ya mechi kuahirishwa kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu tulikutana na Wizara ya Michezo na kuongea na kuelewana sasa walitakiwa wakatae katika kikao chetu na waziri, kama wanaona walikubali bahati mbaya wamtafute tena waziri wamwambie,” alisema Mnguto.


WASIKIE WADAU

Video hiyo ya Bumbuli akisisitiza hawaitambui mechi ya Julai 3, imewafanya wadau mbalimbali kuwa na mtazamo tofauti ambapo nyota wa zamani wa kimataifa wa Yanga na Taifa Stars, Chambua Seklojo alisema anashindwa kuzungumza kwa kina kwa kutojua vizuri kinachotaka kuizuia Yanga wasicheze mchezo huo.

“Tukio la mchezo kutochezwa lilitokea katika mazingira ambayo hayakufuata taratibu na sijafuatilia zaidi kujua sababu hasa ni nini kama kanuni zinataka mechi ichezwe kuna umuhimu wa kupeleka timu, kama kanuni haipo wanaweza kutoipeleka ila nawashauri wafuate taratibu,” alisema Chambua.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Nchunga alisema hadi leo hajui kilichosababishwa mechi ya awali kuahirishwa, ila anadhani hiyo ndio sababu inayowafanya Yanga kusimamia msimamo wao huo wa sasa.

“Kuahirishwa mchezo kuna mambo mengi sana ratiba, muda, sababu za ahirisho iliyokuwa kwenye ratiba ndio shida iko hapo. Yanga wanaililia sababu haitakiwi kuwa siri, ndio maana inatokea hii kitu, pande zote zinatakiwa ziujue ukweli wa kilichotokea kwa mujibu wa kalenda haikutakiwa chombo chochote iwe serikali, TFF na Bodi ya ligi kuahirisha mchezo huo,” alisema Nchunga.

Advertisement