Yanga yatozwa faini, Barbara, Mangungu wamo

KLABU ya Yanga imetozwa faini ya Sh1 milioni  kwa kosa la kuingia uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kutumia mlango usiokuwa rasmi katika mchezo uliowakutanisha na Simba Desemba 11 mwaka jana.

Hatua hii inakuja baada ya kamati ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) katika kikao chake cha Desemba 30, 2020 kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi hayo.

Ofisa Mtendaji wa Simba, Barbara Gonzales ametozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kuishutumu Bodi ya Ligi kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwa ilimzuia yeye na familia yake kuingia uwanjani kutazama mchezo wa Simba na Yanga jambo ambalo halina ukweli wowote.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya ligi hiyo ilieleza kuwa Barbara hakukubaliana na maelekezo halali ya maafisa wa mchezo huo kuhusu utaratibu wa kuingia eneo la watu maalumu (VVIP) ndipo akaamua kuondoka na kupewa adhabu hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 46 (10) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa viongozi.

Naye mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu ametozwa faini ya Sh500,000 kwa kutoa matamshi yenye utata kupitia vyombo vya Habari kuhusu Bodi ya Ligi na TFF kuwa zimepanga kuipa klabu ya Yanga ubingwa na kumaliza msimu mara moja.

Adhabu hiyo kwa Mangungu ni kwa kuzingatia kanuni ya 46 (10) kuhusu udhibiti kwa viongozi.

Katika hatua nyingine kamati hiyo imezitaka klabu zote kuendelea kutekeleza masharti yote ya mikataba ya udhamini kwa mazingatio ya kanuni kwani jambo hilo ni muhimu sana kwa sababu ndio msingi wa kuendelea kuwepo kwa wadhamini ikivutia pia wadhamini wengine.

Aidha imezikumbusha klabu kuzingatia na kulipatia umuhimu suala la mikutano ya wanahabari ambayo mbali na kusaidia kutangaza wadhamini wa ligi imekuwa na faida nyingi ikiwemo kuimaraisha mahusiano mazuri na vyombo vya habari ili kuweza kuitangaza ligi yenyewe na kuisaidia katika kuziunganisha klabu na mashabiki wake.

Kamati hiyo imezimia kutoa adhabu kwa klabu yoyote ambayo  kocha wake na nahodha watashindwa kuhudhuria mkutano na wanahabari kuanzia Januari mosi mwaka huu.

Adhabu ya juu kwa kosa la kwanza kwa mujibu wa kanuni ya 17(56 & 60) ya Ligi Kuu ni faini ya Sh1 milioni na kwa makosa ya kujirudia ni Sh5 milioni.