Miaka 20 ya Premier Agencies katika kutoa huduma bora na kulipa kodi

Mkurugenzi Mkuu wa Premier Agencies, Robert Singu (kulia) akikabidhiwa cheti cha ushiriki wa tuzo za mlipa kodi bora wa mwaka zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kampuni hiyo ilishika nafasi ya tatu katika kipengele cha walipa kodi wadogo Mkoa wa kikodi wa Temeke.
Muktasari:
Kodi ni msingi wa maendeleo ya Taifa kwa sababu ndizo zinazotumika katika kutengeneza ustawi wa Taifa kwa kuboresha huduma za jamii na miundombinu.
Kodi ni msingi wa maendeleo ya Taifa kwa sababu ndizo zinazotumika katika kutengeneza ustawi wa Taifa kwa kuboresha huduma za jamii na miundombinu.
Kodi hizi hulipwa na watu binafsi kupitia shughuli zao ikiwemo ajira, kampuni, mashirika, taasisi wajasiriamali na wafanyabiashara ambao kwa jina moja wote hutambulika kama walipa kodi.
Walipa kodi ni kundi muhimu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa sababu kodi ndizo zinaiwezesha Serikali kutekeleza mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
Kwa kutambua umuhimu wa walipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza Novemba kuwa mwezi maalumu kwa ajili ya kutoa shukrani kwao.
Pamoja na mambo mengine mamlaka hiyo ililenga kurudisha shukrani kwa walipa kodi na wadau wa kodi wote nchini kwa juhudi na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Miongoni mwa mambo ambayo TRA wameyafanya ikiwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho hayo ni kuandaa mbio na matembezi ya shukrani kwa mlipakodi pamoja na tuzo ambazo walizotoa kwa walipa kodi bora katika makundi tofauti.
Moja ya washindi katika tuzo hizo ni kampuni ya Premier Agencies ambayo ilishika nafasi ya tatu katika kundi la walipa kodi wadogo Mkoa wa Kikodi wa Temeke.
Gazeti hili lilipata nafasi ya kufanya mahojiano na Mkurugenziwa Mkuu wa kampuni hiyo, Robert Singu ambaye alieleza siri ya mafanikio ya kutwaa tuzo hiyo pamoja na mikakati yao katika kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri katika ulipaji kodi.
Tueleze kuhusu Premier Agencies na shughuli inazofanya
Premier Agencies ni kampuni iliyoanzishwa mwaka 2002 ambayo inajishughulisha na uuzaji, usambazaji, ufungaji na matengenezo ya vifaa vya kampuni za mafuta na viwandani.
Lengo kubwa la kuanzishwa kwake ni kutoa huduma za matengenezo katika kampuni za mafuta. Pia ni wakandarasi wa daraja la kwanza katika sekta ya mafuta na Gesi (Specialized contractors in oil and gas class 1).
Kitu kilichosababisha kuanzisha kampuni hii ni fursa tuliyoiona katika sekta ya mafuta na shughuli za viwandani kwa sababu kabla sijafungua kampuni hii nilifanya kazi katika kampuni za mafuta kwa miaka mingi hivyo niliona fursa hii.
Siku za nyuma wakati nipo katika shughuli za mafuta nilikuwa naona kampuni hizo zikiagiza vifaa, kufunga na kufanya matengenezo zenyewe.

Mkurugenzi Mkuu wa Premier Agencies, Robert Singu akiwa na cheti cha ushiriki wa tuzo za mlipa kodi bora wa mwaka zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kampuni hiyo ilishika nafasi ya tatu katika kipengele cha walipa kodi wadogo Mkoa wa kikodi wa Temeke.
Baadaye kampuni hizo ziliamua kupeleka kazi hizo katika kampuni nyingine ili zenyewe ziendeleze biashara ya mafuta hapo ndipo nilipoona fursa hiyo kwa sababu kipindi hicho nilikuwa nafanya kazi katika idara ya matengenezo kwenye moja ya kampuni hizo.
Nini kinafanya Premier Agencies kuwa bora sokoni?
Premier Agencies in wakala wa mauzo aliyeidhinishwa wa kampumi mbalimbali kubwa za kimataifa (zilipo Marekani na Ulaya) zinozotengeneza vifaa/mashine mbalimbali mfano Dover fuelling solutions, pampu za vituo vya mafuta, Technip FMC, mita za mafuta na gesi.
Ukiwa wakala aliyeidhinishwa wa kampuni hizi kubwa unapata nafasi ya wafanyakazi wako kupewa mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna ya kutambua vifaa halisi na visivyo halisi, ufungaji, matengenezo nk. Hivyo hili limetufanya kuwa moja ya kampuni inayotoa huduma za kipekee na kuaminiwa zaidi.
Premier Agencies haiuzi bidhaa pekee bali pia inatoa huduma za ufungaji, matengenezo na huduma kwa mteja baada ya mauzo hivyo kuifanya kuwa ya kipekee katika soko.
Bidhaa zetu zina ubora wa aina moja kwa sababu zinazalishwa na kampuni moja ambayo viwango vya bidhaa zake viko sawa. Kitu kingine ni weledi ambao tunao katika kutoa huduma.
Ubora wa bidhaa na huduma za Premier Agencies ukoje?
Ubora wa bidhaa zetu ni wa hali ya juu kwa sababu zimethibitishwa na mamlaka zote za ndani pamoja na mashirika ya kimataifa kwa sababu kampuni ambazo tunafanya nazo kazi ni za hadhi ya kimataifa.
Bidhaa ambayo inauzwa na Premier Agencies Tanzania ukienda Marekani ama Uingereza utaikuta tena katika ubora ule ule kwa sababu viwango vya ubora wa bidhaa za kampuni tunazofanya nazo kazi viko sawa dunia nzima.
Tuzo ya TRA mliyoipata ina maana gani kwenu?
Kwanza tunawashukuru wote waliotupigia kura, tunawaambia kwamba tunathamini imani yao kwetu na tunawahakikishia tutailinda kwa kuendelea kuwapa huduma bora.
Aidha, TRA kututambua kwamba tunafuata taratibu za kodi imetupa moyo na hamasa ya kuendelea kufuata sheria za kodi nchini kwa sababu sisi tunafanya kazi na kampuni za kimataifa ambazo zinazingatia kufuata taratibu, sheria na kanuni zote ikiwemo za kodi ili ziweze kufanya biashara na wewe.
Hivyo tuzo hii imetuongezea kuaminika kwa washirika wetu lakini pia Serikali na wateja wetu kwa sababu imeonyesha ni namna gani tunatii sheria zilizowekwa na mamlaka husika. Tuzo hii na nyingine ambazo tumewahi kushinda ikiwemo zile za kampuni ndogo na za kati (Top 100) zimenifanya kuwa mwanachama wa Umoja wa Watendaji Wakuu Tanzania (CEOrt Tanzania) ambao unasimamia maadili ya utendaji kazi.
Ni uzoefu gani mmeupata kwa kushiriki tuzo hizi?
Kikubwa ni kukutana na mashirika na taasisi kubwa zinazofanya biashara nchini, kukaa meza moja na kubadilishana uzoefu ni jambo kubwa ambalo tumelipata kwa kushiriki tuzo hizi.
Mikakati yenu ni ipi katika kuendelea kufanya vizuri kwenye tuzo hizi mwakani?
Mkakati mkubwa ni kuendelea kuboresha mifumo yetu ya ndani hususani ile ya kidijitali ili kuhakikisha inaendelea kuwa bora jambo litakalorahisisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kokodi na hivyo kutufanya kuendelea tulipoishia mwaka huu.
Kingine ni kuendelea kuboresha utoaji wa huduma na bidhaa kwa wateja wetu. Tutahakikisha tulichofanya mwaka huu tunakifanya mara mbili au tatu hapo mwakani hivyo wateja na washirika wetu wakae mkao wa kula mambo mazuri yanakuja.