NASHCoP: Mapambano dhidi ya VVU, UKIMWI, magonjwa ya ngono na homa ya ini ni jumuishi na endelevu
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya UKIMWI (UNAIDS) kwa mwaka 2023 liliitangaza Tanzania kuwa ni nchi iliyofikia makubaliano ya kimataifa ya 95 Tatu kabla ya muda uliokubalika wa mwaka 2025.
Lakini ukweli ni kwamba bado Tanzania ina watu takribani milioni 1.5 wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Takwimu hizi zinaifanya nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi tano zenye changamoto kubwa ya kudhibiti ugonjwa huu barani Afrika.
Mwaka 1978, Tanzania, kwa mara ya kwanza iliungana na wadau wengine wa afya kupigia chapuo uboreshaji wa huduma za afya duniani kupitia Azimio la Alma Atta ambalo lilisisitiza uboreshaji wa huduma za afya ya msingi.
Tangu hapo, Tanzania imekuwa ikishiriki na kuridhia maazimio mbalimbali ya sekta ya afya ya Umoja wa Mataifa katika kuyafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu. Hivyo, 1983 mtu wa kwanza alipogundulika na maambukizi ya VVU na UKIMWI Mkoani Kagera katika Hospitali ya Ndolage,
Serikali iliunda tume ya kushughulikia masuala ya UKIMWI mwaka 1984 na kisha Wizara ya Afya kuanzisha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP), mwaka 1988, lengo likiwa kusimamia shughuli zote za udhibiti wa mlipuko wa UKIMWI nchini na kisha Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) mwaka 2001 kwa lengo la kuratibu sekta zote kutokana na suala la UKIMWI kuwa mtambuka.
Harakati za kudhibiti UKIMWI zimekuwa zikiendelea na ilipofika mwaka 2016, Shirika la Afya Duniani kupitia mkutano wake wa “World Health Assembly” lilitoa maazimio kadhaa, ikiwemo kutokomeza maambukizi ya homa ya ini hadi kufikia mwaka 2030 kwa kuweka malengo yafuatayo: -
Kupunguza maambukizi mapya ya homa ya ini aina B na C kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2030, kupunguza vifo vitokanavyo na homa ya ini aina B na C kwa asilimia 65 ifikapo mwaka 2030 na kuhakikisha asilimia 80 ya watu wenye maambukizi ya homa ya ini wanapata matibabu stahiki.
Kwa takwimu zilizotolewa Shirika la Afya la Dunia mwaka 2019 inakadiria kuwa kiwango cha maambukizi ya homa ya ini kuwa; watu milioni 296 wanaishi na maambukizi sugu ya Virusi vya homa ya ini aina B, watu milioni 58 wanaishi na maambukizi sugu ya Virusi vya homa ya ini aina C, watu milioni 1.5 wana maambukizi mapya ya Virusi vya homa ya ini aina B na watu milioni 1.5 wana maambukizi mapya ya Virusi vya homa ya ini aina C. Kupitia taarifa ya homa ya ini aina B ya WHO ya mwaka 2021 ilikadiriwa kuwa kiwango cha maambukizi sugu ya homa hiyo, 2019 ni asilimia 6.1.
Hali hii ilipelekea mapendekezo ya WHO ya kujumuisha afua za homa ya ini na magonjwa ya ngono katika afua za VVU na UKIMWI, jambo ambalo liliridhiwa na Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Afya kuanzisha mchakato wa kuunganisha afua hizi.
Mantiki ya kujumuisha huduma za udhibiti wa magonjwa ya ngono na Homa ya ini kwenye NACP Virusi vinavyosababisha homa ya ini aina ya B na C vinaambukizwa kwa njia zinazofanana na VVU kama; njia ya damu, ngono, kuchangia vitu vyenye ncha kali kwa kujidunga madawa ya kulevya na maambukizi kutoka kwa mama mjamzito mwenye maambukizi kwenda kwa mtoto.
Pili, ufanano na upatikanaji wa vipimo na dawa, VVU na virusi vya homa ya ini vinaweza kupimwa kwa njia ya haraka. Tatu, NACP ina mtandao madhubuti wa maabara wa vipimo vya uwingi wa virusi (HVL) na vipimo vingine nchi nzima hii itasaidia kutumia rasilimali zilizopo nchini na kuweza kupunguza gharama za kupambana na Homa ya ini kwa mgonjwa.
Matibabu ya virusi vinavyosababisha homa ya ini aina B vinatibiwa kwa kutumia ARVs aina ya Tenofovir. Mpango huu unakusudia kuona maambukizi mapya ya VVU yanapungua kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025 kutoka kiwango cha awali cha mwaka 2010 (110,000), maambukizi ya VVU na Virusi ya homa ya ini kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanapungua hadi chini ya asilimia 4 ifikapo mwaka 2025, vifo vinavyotokana na UKIMWI vinapungua kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2025 kutoka kiwango cha awali cha mwaka 2010 (64,000).
Pia, unyanyapaa unaohusiana na UKIMWI unapungua hadi chini ya asilimia 5 ifikapo mwaka 2025 kutoka kiwango cha awali cha mwaka 2013, ambacho kilikuwa asilimia 28 kwa unyanyapaa wa jamii na asilimia 20.5 kwa unyanyapaa binafsi.
Mafanikio yaliyopatikana katika jitihada za kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa ya ngono hadi 2024
Wizara ya Afya kupitia NASHCoP imekuwa ikiandaa na kutoa sera, mipango mikakati, miongozo, usimamizi wa ubora wa huduma za afya za UKIMWI, kutoa msaada wa kitalaamu na kujengea uwezo kwa sekta nyingine, kufanya mafunzo, kukusanya takwimu na kusambaza taarifa juu ya huduma za VVU na UKIMWI, kutoa, Habari, elimu na Mawasiliano ya kubadili tabia na usambazaji wa bidhaa za huduma za VVU na UKIMWI kama kondomu, vitendanishi, vifaa tiba na kuhakikisha upatikanaji wa ARVs hapa nchini wakati wote ambapo kazi hii amekasimishwa Bohari ya Dawa (MSD) ambayo ni idara ndani ya Wizara ya Afya.
Mafanikio hadi kufikia Desemba 2023
I. Kiwango cha ushamiri wa VVU kimepungua kutoka asilimia 7.0 mwaka 2002/2003 hadi asilimia 4.4 mwaka 2022/2023 kwa watu wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 45. Kati ya hao, asilimia 4.5 ni wa upande wa Tanzania Bara, na asilimia 0.4. ni kutoka Zanzibar;
II. Asilimia 83 ya kati ya wanaokisiwa kuishi na VVU wamepima na wanatambua hali zao, kati yao asilimia 98 wameanzishiwa dawa za kupunguza makali na asilimia 94 wamefikia kiwango cha ufubavu wa VVU mwilini;
III. Maambukizi mapya ya VVU kupungua kutoka 46,000 mwaka 2021 hadi 32,000 mwaka 2023;
IV. Vifo vitokanavyo na UKIMWI kupungua kutoka 29,000 mwaka 2021 hadi 22,000 kwa mwaka 2023;
V. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupungua kutoka asilimia 8.04 mwaka 2021 hadi 6.94 mwaka 2023;
VI. Afua za kuzuia maambukizi ya virusi vya homa ya ini aina ‘B’ kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zinatolewa katika vituo 102 vilivyoko katika mikoa minne kwa majaribio ili kupata takwimu za kufanyia maoteo na kusambaza huduma hizi katika vituo vyote nchini;
VII. Machi 2023 hadi Februari 2024 jumla ya vitepe vya kujipima 1,444,356 sawa na asilimia 43 ya malengo viligawiwa jumla ya wateja 1,277,928 sawa na asilimia 88 walirudisha majibu;
VIII. Hadi Februari 2024, idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya Tiba na Matunzo vimefikia 7,396 kutoka 7,072 mwaka 2022/23, sawa na asilimia 80 ya vituo 9,277 vinavyotoa huduma za afya;
IX. Kuanzishwa kwa mfumo wa usajili wa WAVIU kwa kutumia alama za vidole, hadi sasa vituo 2,447 kati ya 7,396 sawa na asilimia 33 vinatumia mfumo huo;
X. Hadi Desemba 2023 walengwa 65,592 walikuwa wamepatiwa huduma ya dawa kinga dhidi ya maambukizi ya VVU;
XI. Julai 2023 hadi Februari 2024, WAVIU wote wameweza kupata ARV kwa asilimia 100;
XII. Mashine za kupima wingi wa virusi vya UKIMWI na maambukizi yake kwa watoto zimeongezeka kutoka 169 hadi 173;
XIII. Upimaji wa wingi wa VVU umeongezeka kutoka asilimia 90 hadi 96 toka mwaka 2021 hadi 2023;
XIV. Kufikia Desemba 2023, jumla ya walengwa 171,687 walichunguzwa Homa ya ini (Hepatitis B) na wapatao 125,222 walichunguzwa Homa ya ini (Hepatitis C); na
XV. Wizara kwa kupitia NASHCoP imefunga Makasha ya kusambazia Kondomu 85,000 ikijumuisha maeneo ya kazi, maofisi na maeneo ya ujenzi.
Kwa kipindi cha Desemba 2021 hadi Desemba, 2023 kondomu 279,518,200 zilipokelewa, 155,340,900 zilisambazwa na kubakiwa na akiba ya 124,177,300.
Hitimisho
Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha inatambua mahitaji halisi ya huduma za afya zinazohusu VVU, UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini kulingana na mazingira halisi, na kuratibu njia au mifumo rahisi ya kufikisha huduma za afya kwa walengwa kwa weledi, ubora, usawa bila unyanyapaa na bila malipo.
Kwa taarifa zaidi Ushauri na Rufaa ya VVU, Magonjwa na Ngono na Homa ya Ini piga Namba 117 Bila Malipo Au tuandikie S.L.P 784, Kilimani Area, NASCoP Buildig, Simu: +255 (0) 262060148, Barua pepe: nashcop@ afya.go.tz Au tembelea tivuti: nacp.go.tz, instgram.com/nashcoptanzania; nacpfurahayangu; facebook; NASHCoP-Furaha Yangu