Singu: Ushirikiano, weledi, kuzingatia ubora ndiyo siri ya mafanikio ya Premier Agencies
Kiongozi bora katika kampuni ni nguzo muhimu ya mafanikio. Wanatoa mwongozo, msukumo na mwelekeo kwa wafanyakazi. Kupitia uongozi wao, kampuni hufanikiwa kufikia malengo yake na kuendeleza utamaduni wa kazi uliojengwa juu ya uaminifu, uwazi, na uvumilivu.
Kiongozi bora anajua kuweka malengo na kuvuta timu yake kuelekea kwenye maono ya kampuni. Anajenga mwelekeo wa pamoja na kuhamasisha wafanyakazi kufuata lengo hilo.
Pia, husisitiza mawasiliano ya wazi kati ya wafanyakazi. Wanajua umuhimu wa kusikiliza maoni ya wafanyakazi na kushirikisha habari muhimu kwa njia inayoeleweka.
Sifa hizi haziji hivihivi bali ni kutokana na misingi bora iliyojengwa katika safari ya kiongozi huyo. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Premier Agencies, Robert Singu ni kielelezo sahihi cha sifa hizi.
Singu ambaye kitaaluma ni mhandisi mitambo (mechanical engineer) alianza safari yake mara baada ya kumaliza chuo kikuu ambapo aliajiriwa kiwandani akiwa mhandisi miradi wa moja ya kiwanda cha kuzalisha sabuni na dawa za meno kilichopo Dar es Salaam.
Anasema alifanya kazi kiwandani hapo kwa muda wa miaka minne kisha akaamua kuingia katika tasnia ya mafuta alipoajiriwa na moja ya kampuni kubwa za mafuta nchini na kufanikiwa kufanya kazi miaka mitatu kabla ya kuhamia katika kampuni nyingine ambapo ndipo ndoto ya kuanzisha kampuni yake ilipoanzia.
“Nilipoingia katika tasnia ya mafuta nilikuwa katika upande wa mitambo ambao jukumu langu kubwa lilikuwa ufungaji wa mitambo mbalimbali pamoja na kuifanyia matengenezo. Jukumu hili lilinifanya kukutana na wazalishaji mbalimbali wa mitambo hiyo,” anasema Singu.
Anasema wakati anaendelea kufanya kazi hiyo alikua anasoma kozi ya masoko ambyo anaeleza kuwu ilikuwa na nguzo nne ambazo alifundishwa. Nguzo hizo ni; bidhaa (products), bei (price), matangazo (promotion) na eneo (place).
“Baada ya kufanya kazi katika kampuni ya mafuta kwa miaka kadhaa niliona fursa katika sekta ya usambazaji, ufungaji na ukarabati wa mitambo katika tasnia ya mafuta na gesi,” anasema Singu.
Anasema kutokana na fursa hiyo, mwaka 2002 alianzisha kampuni ya Premier Agencies kwa lengo la kushughulikia changamoto iliyokuwa inaikabili sekta ya mafuta hususani katika upatikanaji wa mitambo bora, huduma bora za ufungaji na matengenezo.
Anasema kampuni za mafuta zilikuwa zinaagiza vifaa, kufunga na kufanya matengenezo zenyewe. Baadaye ziliamua kupeleka kazi hizo katika kampuni nyingine ili zenyewe ziendeleze biashara ya mafuta hapo ndipo alipoona fursa hiyo
“Premier Agencies ilianza rasmi mwaka 2002 kwa madhumuni ya kutoa huduma katika sekta ya mafuta kwa kuuza na kusambaza mitambo, kufunga na kutoa huduma za matengenezo,” anasema Singu.
Anasema katika kozi yake ya masoko alibobea katika masuala ya biashara za kimataifa hivyo akaingia makubaliano ya kibiashara na baadhi ya wasambazaji wa mitambo wa kimataifa ambao aliwafahamu wakati ameajiriwa.
Anasema kutokana na makubaliano hayo, Premier Agencies ni wakala wa mauzo aliyeidhinishwa wa kampumi mbalimbali kubwa za kimataifa (zilipo Marekani na Ulaya) zinozotengeneza vifaa/mashine mbalimbali mfano Dover fuelling solutions, pampu za vituo vya mafuta, Technip FMC, mita za mafuta na gesi, GRACO BVBA watengezaji mitambo ya kusukuma vilainishi vya mitambo (lubrication equipment)
“Premier Agencies haiuzi bidhaa pekee bali pia inatoa huduma za ufungaji, matengenezo na huduma kwa mteja baada ya mauzo hivyo kuifanya kuwa ya kipekee katika soko,” anasema Singu.
Anasema bidhaa zao zina ubora wa aina moja kwa sababu zinazalishwa na kampuni ambazo viwango vya bidhaa zake viko sawa bila kujali inauzwa wapi. Kitu kingine ni weledi ambao wanao katika kutoa huduma.
“Ubora wa bidhaa zetu ni wa hali ya juu kwa sababu zimethibitishwa na mamlaka zote za ndani pamoja na mashirika ya kimataifa kwa sababu kampuni ambazo tunafanya nazo kazi ni za hadhi ya kimataifa na ndiyo maana jina la kampuni ni Premier Agencies ikiwa na tafsiri ya kuwa wakala wa bidhaa ambazo ni “Premier,” anasema Singu.
Bidhaa ambayo wanauza ukienda Marekani ama Uingereza utazikuta tena katika ubora uleule kwa sababu viwango vya ubora vya kampuni wanazofanya nazo kazi viko sawa dunia nzima.
Kuhusu aina ya uongozi wake katika kampuni, Singu anasema yeye ni kiongozi ambaye anapenda kujifunza na kushirikisha wafanyakazi katika kila jambo.
“Naamini zaidi katika kujifunza na ushirikishwaji. Katika uzoefu wangu wangu wa zaidi ya miaka 20 bado kuna vitu sivifahamu hivyo naendelea kujifunza kupitia kwa wafanyakazi pamoja na wadau mbalimbali ninaofanya nao kazi,” anasema Mkurugenzi huyo.
Singu anasema mabadiliko ya teknolojia pamoja na ugunduzi wa gesi kunafanya vitu mbalimbali kubadilika katika soko hivyo lazima awe anajifunza kila siku ili kwenda sambamba na mabadiliko hayo.
Kuendeleza rasilimali watu ni moja ya mambo muhimu katika maendeleo ya kampuni, Singu anasema wamekuwa na mkakati wa kuwaendeleza wafanyakazi wao kupitia kampuni za kimataifa wanazofanya nazo kazi.
“Ukiwa wakala aliyeidhinishwa wa kampuni hizi kubwa unapata nafasi ya wafanyakazi wako kupewa mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna ya kutambua vifaa halisi na visivyo halisi, ufungaji, matengenezo nk. Hivyo hili limetufanya kuwa moja ya kampuni inayotoa huduma za kipekee na kuaminiwa zaidi,” anasema Singu.
Anasema kampuni hiyo pia imeanzisha mkakati wa kupita vyuoni na kuchukua wanafunzi kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ya vitendo ambapo panapotokea hitaji la wafanyakazi, huwatumia walewale waliowapa mafunzo.
Kuhusu mikakati Singu anasema kwa sasa wanaanda mazingira ya kuingia katika sekta ya gesi ili kuunga mkono juhudi za Serikali na mipango ya kitaifa ya matumizi ya gesi hususani kipindi hiki ambacho nchi ina rasilimali gesi.
Anasema kuendelea kuboresha mifumo ya ndani hususani ile ya kidijitali ili kuhakikisha inaendelea kuwa bora jambo litakalorahisisha utekelezaji wa masuala mbalimbali. Kingine ni kuendelea kuboresha utoaji wa huduma na bidhaa kwa wateja.