Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na miaka zaidi ya 60 katika utoaji wa elimu bora

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima (wa tatu kulia, walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru wakati wa mahafali ya taasisi hiyo mwaka 2022.

Muktasari:

Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (Tengeru Institute of Community Development-TICD) awali ilijulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii (Community Development Training Institute- CDTI Tengeru).

Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (Tengeru Institute of Community Development-TICD) awali ilijulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii (Community Development Training Institute- CDTI Tengeru).

Taasisi hii ipo mkoani Arusha, wilaya ya Arumeru nje kidogo ya jiji la Arusha ikiwa ni kilometa 13 kutokea mjini Arusha, kando ya barabara ya Moshi-Arusha.

Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ni mojawapo ya taasisi kongwe za elimu za Serikali iliyoanzishwa mwaka 1961.

Wataalam wa maendeleo na afya, waliofuzu kutoka katika taasisi hii walitumika kuhamasisha na kutoa mafunzo ya maendeleo kwa wananchi.

CDTI-Tengeru kilipata fursa ya kutoa mafunzo kwa wataalam hao waliotambuliwa kwa jina maarufu Ma-bibi/bwana maendeleo na afya kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 1967, ambapo baada ya hapo, mafunzo hayo yalihamishiwa katika chuo cha Uongozi wa Maendeleo Mzumbe.

Moja ya majengo ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.

Mwaka 1981 CDTI-Tengeru kilianza rasmi kutoa mafunzo kwa ngazi ya cheti na 1983 kilianza kutoa mafunzo ya Stashahada ya Juu ya Maendeleo ya Jamii. Kabla ya hapo mafunzo hayo yalikuwa yanatolewa na Chuo cha Uongozi wa Maendeleo Mzumbe.

CDTI-Tengeru ilitambulika rasmi kama taasisi ya elimu ya juu mwaka 1994 baada ya mtaala wa mafunzo ya stashahada ya Juu ya Maendeleo ya Jamii kupitiwa na kupitishwa na mamlaka ya uzimamizi wa mafunzo kwa wakati huo.

Hata hivyo, taasisi iliidhinishwa kuwa na mamlaka kamili mwaka 2013 na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa sheria namba 1 ya mwaka 2013 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shughuli zinazofanywa na taasisi

Taasisi inafanya shughuli kuu tatu ambazo ni;

I. Kuendesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika nyanja ya Maendeleo ya Jamii, Upangaji na Usimamizi wa Miradi na Jinsia na Maendeleo.

II. Kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali yanayohusu Maendeleo, Miradi na Jinsia

III. Kutoa ushauri elekezi katika mambo yanayohusu Maendeleo, Miradi na Jinsia.

Programu za nafunzo na sifa za kujiunga

Cheti cha Awali (Basic Technician Certificate-NTA level 4) katika Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Maendeleo ya Jamii na Uendeshaji wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii

Sifa-ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne angalau masomo manne kwa kiwango cha alama “D” au zaidi.

• Cheti cha Msingi (Technician Certificate-NTA level 5) katika Maendeleo ya Jamii; Jinsia na Maendeleo ya Jamii na Uendeshaji wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii.

• Ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne angalau masomo manne kwa kiwango cha alama “D” au zaidi.

• Cheti cha Awali (NTA level 4) kutoka chuo chochote kinachotambuliwa na NACTE au

• Ufaulu wa mtihani wa kidato cha sita angalau somo moja katika kiwango cha alama E (Principal pass) na somo moja alama S (Subsidiary pass) au zaidi kwa waliomaliza kabla ya mwaka 2014 na baada ya mwaka 2015. Waliomaliza kidato cha sita mwaka 2014 na 2015 wawe na angalau alama C (Principal pass).

Stashahada (Diploma)-(NTA LEVEL 6) katika Maendeleo ya Jamii; Jinsia na Maendeleo ya Jamii; na Uendeshaji wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii.

• Ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne angalau masomo manne kwa kiwango cha alama “D” au zaidi.

• Cheti cha Msingi (NTA level 5) kutoka Chuo chochote kinachotambuliwa na NACTE.

I. Shahada ya kwanza ya Maendeleo ya Jamii (Bachelor of Community Development).

II. Shahada ya kwanza ya Uendeshaji wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii (Bachelor of Project Management for Community Development).

III. Shahada ya kwanza ya Jinsia na Maendeleo ya Jamii (Bachelor of Gender and Community Development).

Mafunzo yanayotolewa na TICD yanazingatia uwiano kati ya nadharia na vitendo. Huku mitaala inatekelezwa ikizingatia dhana tatu ambazo ni uanagenzi, ushirikishwaji jamii na ubunifu wa kidijitali.

Aidha, kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na umuhimu wa kuandaa wahitimu wenye fikra sahihi na uwezo wa kujiajiri, TICD itaongeza program sita za mafunzo kuanzia dirisha la Machi 2023. Program hizo ni:

I. Usimamizi wa Rasilimali Watu (Human Resource Management);

II. Ustawi wa Jamii (Social Work);

III. Uhasibu na Usimamizi wa Fedha (Accounting and Finance);

IV. Utawala na Usimamizi wa Serikali za Mitaa (Local Government Administration);

V. Utawala na Usimamizi wa Maendeleo (Public Administration and Management); na;

VI. Usimamizi wa Afya Mazingira (Environmental Health Management.

Sifa za Kujiunga kwa kila Shahada

Waombaji wa Kidato cha Sita wawe na ufaulu wa masomo angalau mawili yenye ufaulu wa alama kuanzia D jumla ya pointi nne. Waliomaliza Kidato cha Sita mwaka 2014 na 2015 wawe na angalau ufaulu wa masomo mawili alama C pointi nne.

Waombaji wa Stashahada (NTA level 6) katika fani za Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Maendeleo, Upangaji wa Miradi, Sheria, Utunzaji wa Kumbukumbu, Uchumi na Maendeleo, Ualimu, Utawala na Rasilimali watu wawe na wastani wa alama B au GPA ya 3.0 kutoka kwenye vyuo vinavyotambuliwa na NACTE au TCU

• Ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne angalau masomo manne kwa kiwango cha alama “D” au zaidi.

• Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii (Master Degree in Community Development)

• Shahada ya Uzamili ya Mipango, Usimamizi na Tathmini ya Miradi (Master Degree in Project Planning, Monitoring and Evaluation)

• Sifa za Kujiunga Shahada ya Uzamili

• Shahada ya kwanza (Degree)

• Stashahada ya Juu (Advanced Diploma) kutoka katika Chuo kinachotambuliwa na NACTVET au TCU.

Miundombinu ya kujifunzia

Taasisi ina mazingira rafiki na tulivu ya kufundishia na kujifunzia yanayomwezesha mwanafunzi kuwa mahiri katika nyanja ya Maendeleo ya Jamii, Upangaji na Uzimamizi wa Miradi na Jinsia na Maendeleo. Miundombinu hiyo ni kama ilivyochanganuliwa hapa chini:

Kumbi za mihadhara na madarasa

TICD inayo madarasa na kumbi za mihadhara za kutosha zenye kutoa nafasi nzuri kwa ajili ya kujifunzia na kufundishia. Kumbi za mihadhara zilizopo ndani ya Taasisi zinatumika kwa ajili ya kuendeshea mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na warsha na mihadhara mbalimbali.

Maabara ya Kompyuta

Taasisi ina maabara tatu za kompyuta zenye uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 180 kwa wakati mmoja. Maabara hizi zimefungwa kompyuta za kisasa zilizounganishwa na mtandao muda wote.

Hali kadhalika kompyuta za taasisi zimewezeshwa kupakuwa vitabu na machapisho vya nakala laini kutoka kwenye mifumo ya maktaba ya taasisi hata ikiwa hakuna mtandao (offline libray). Matumizi ya technolojia yanawezesha wanafunzi kuwa kwenye mazingira mazuri na rahisi ya kujisomea.

Hata hivyo taasisi inatoa nafasi kwa wanafunzi kujiunganishia mtandao kwa njia ya ‘’WIFI’’ ili watumiaji wengi wapate huduma ya mtandao kwa pamoja.

Maktaba

Maktaba kuu ya Taasisi ina vitabu na machapisho ya kutosha yaliyopo kwenye nakala ngumu na nakala laini. Maktaba hii ina uwezo wa kutoa huduma kwa watumiaji waliopo ndani na nje ya maktaba.

Watumiaji wa maktaba wanaweza kusoma vitabu vilivyopo kwenye maktaba kwa kutumia simu janja, kompyuta mpakato au kifaa chochote kinachoweza kuunganishwa na mtandao. Matumizi ya technolojia yamesaidia watumiaji wengi kutumia maktaba ya Taasisi wakati wote wa siku.

Malazi

Taasisi ina uwezo wa kutoa huduma ya malazi kwa takribani wanafunzi 1000 wanaosajiliwa kujiunga na taasisi. Aidha, huduma ya malazi (hosteli) inapatikana katika taasisi kwa bei nafuu. Huduma ya malazi inatolewa kipaumbele kwa wanafunzi wageni na wanafunzi wanaosoma cheti na diploma.

Masuala ya ubunifu wa kidijitali

Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ina kituo cha Huduma Tandaa na Ubunifu wa Kidijitali (JODIC) kilichoanzishwa mwaka 2019 kikiwa na lengo la kuwa na eneo la kuzalisha na kulea mawazo ya ubunifu hadi kufikia kutumiwa na jamii.

Kituo hiki kinahudumia wanafunzi waliosajiliwa kusoma kwenye Taasisi hii lakini pia wananchi wanaozunguka maeneo ya jirani na chuo katika wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha kwa ujumla.

Kituo cha Utafiti na Uhifadhi wa Machapisho yahusuyo wanawake (NWRDC)

Maktaba hii inayo machapisho na taarifa mbalimbali zinazohusu utafiti na u machapisho ya wanawake zilizokusanywa kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi. Maktaba hii inasaidia pia wanafunzi kujifunza na kujisomea kupitia machapisho na vitabu.