TADB, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuleta mapinduzi ya uchumi wa buluu

“Kikundi chetu cha Nguvu Kazi Group Mtandi kina wanachama kumi na tano (15) ni kikundi cha kijamii (Community Based Organization). Tumekua tukitumia mitumbwi ya kawaida ya mbao kwa muda mrefu. Mitumbwi hiyo hufikia wakati inatoboka au mbao kuoza, hivyo tunashindwa kuwa na uhakika wa kuvua dagaa. Hatukujua kuwa tunaweza kupati boti ya kisasa kabisa tena bila riba,” Bi. Desderia Kishesha katibu wa kikundi cha Nguvu Kazi Mtandi kilichopo Mwanza.


Tafiti zinaonesha kuwa ukosefu wa zana bora za kuvulia samaki ni moja ya changamoto kubwa inayokabili wavuvi nchini hasa wavuvi wadogo.

Sekta ya Uvuvi nchini inajumuisha shughuli za uvuvi wa samaki na na ukuzaji viumbe maji. Sekta hii imekuwa ikikua kwa kiwango cha wastani cha asilimia 1.5 kwa mwaka. Sekta ya Uvuvi ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula, lishe, ustawi wa kijamii na kiuchumi.

Aidha, sekta hii inachangia asilimia 1.7 ya pato la Taifa na hutoa ajira moja kwa moja kwa wavuvi 195,435 na wakuzaji viumbe maji 30,064.

Pamoja na hayo, takribani watu milioni 4.5 (asilimia 6.89 ya jumla idadi ya watu) nchini wanapata ajira zisizo rasmi kupitia shughuli mbalimbali zinazohusiana na minada ya samaki na mazao ya uvuvi.

Kwa kutambua umuhimu wa sekta hii adhimu kwa Watanzania, kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa, Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassan amedhaamiria kuwezesha sekta ya uvuvi nchini ili kuwezesha sekta hiyo kufikia malengo ya kuchangia asilimia 10 katika pato la Taifa (GDP). Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepewa jukumu la kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Kwa kuzingatia dhima na malengo ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) katika kuleta mapinduzi katika sekta ya Uvuvi nchini Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliichagua TADB kuwa benki mshirika katika kutekeleza mradi wa mikopo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji.


Ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Wizara ya Mifugo na Uvuvi na TADB walisaini makubaliano kutekeleza mradi maalumu wa mikopo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji wenye thamani ya Sh 33.4 bilioni kupitia makubaliano hayo, TADB inasimamia na kutoka mikopo katika sekta ya uvuvi kwa riba ya asilimia sifuri.

Malengo ya mikopo hii ni kutatua changamoto za ukosefu wa zana bora za uvuvi, ukosefu wa fedha katika kuendesha miradi ya ukuzaji viumbe maji na ukosefu wa mitaji miongoni mwa wanawake na vijana wanaojishughulisha na uvuvi na kilimo cha mwani.

Zana za kisasa za kuvua samaki kama vile boti, nyavu, injini n.k

TADB kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, katika awamu ya kwanza ya mradi imelenga kutoa jumla ya boti 160 zenye thamani ya Shilingi 11.4bn. Boti hizi za kisasa (fibre boats) zina ukubwa wa kati ya mita 5 hadi mita 14. Pamoja na boti hizi, wavuvi wanawezeshwa kupata vifaa vya utambuzi wa maeneo yenye samaki (fish finder) na vifaa vya kuonesha eneo walipo (GPS), nyavu bora jaketi okozi n.k.

Jumla ya wanufaika 3,361 watanufaika moja kwa moja na mikopo ya boti, kati yao wanawake ni 1,059 na wanaume ni 2,302.

“Boti hii imetusaidia tumeweza kutengeneza ajira kwa vijana wanachama wa kikundi chetu. Sasa tuna uhakika wa kuuza dagaa na kusambaza katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kwa uhakika zaidi,” alieleza Bi. Kishesha kwa tabasamu.


Ukuzaji Viumbe Maji (Aquaculture)

Umuhimu wa kutumia teknolojia na mifumo mbalimbali ya kiubunifu ili kuongeza uzalishaji samaki na viumbe maji haukwepeki katika kufikia malengo ya kukuza uchumi wa Buluu nchini.

Kwa kuzingatia hili, TADB kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi itawawezesha wakulima wa mwani kwenye mikoa ya Pwani ya Bahari ya Hindi na wafugaji wa samaki kwenye vizimba katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria kupata mikopo isiyokuwa na riba katika kukuza biashara zao.

Kupitia mradi huu, wakulima wa mwani 1,738 watanufaika na mikopo ya pembejeo za kilimo cha mwani, kati yao wanufaika 1576 ni wanawake na wanufaika 162 ni wanaume.

Aidha, mikopo ya ufugaji samaki kwenye vizimba itawanufaisha jumla ya wafugaji 1,929 ambapo wanufaika 575 ni wanawake na wanufaika 1,343 ni wanaume.


Wanawake na vijana katika sekta ya uvuvi

Ujumuishaji wa wanawawake na vijana katika miradi ya uvuvi ni jambo muhimu katika kuweza kuboresha mifumo ya chakula na kuongeza ustawi katika jamii.

Kwa kujumuisha wanawake katika kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi katika sekta hii kutachochea kuongeza kwa kipato cha kaya na kuboresha lishe ya familia.

Katika mradi huu shirikishi kati ya TADB na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wanawake wakulima wa mwani na vikundi vya wanawake wavuvi wamepatiwa boti za kisasa zitakazo wasaidia katika kuendeleza shughuli zao za uvuvi na kilimo cha mwani.

Aidha, mradi umefanikiwa kusaidia vijana kupata zana bora za uvuvi na ufugaji viumbe maji.

TADB inaamini katika ushirikiano wa kimkakati. Kwa pamoja TADB itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo za kiserikali, zisizo za kiserikali na wadau wa maendeleo katika kuleta maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi.