Uwekezaji wa Swissport katika usalama hauna mfano

Muktasari:

Tuliyoidhani ingekuwa safari ya masaa machache kuangalia namna kampuni ya Swissport ilivyowekeza katika usalama, imebadilika na kuwa darasa bila malipo la siku nzima kinyume na matarajio yetu.

Tuliyoidhani ingekuwa safari ya masaa machache kuangalia namna kampuni ya Swissport ilivyowekeza katika usalama, imebadilika na kuwa darasa bila malipo la siku nzima kinyume na matarajio yetu.

Darasa lilianza majira ya saa 5:10 asubuhi tulipowasili pale getini, walinzi wa Swissport walipotaka kufahamu utambulisho wetu na kutukagua.

Tulivutiwa na mandhari tulivu ya nje na ubunifu wa rangi nyekundu na nyeupe iliyonakshiwa vyema ndani ya jengo hilo la ofisi iliyotusogeza hadi kwa mtu wa dawati la mapokezi ambaye naye alituandikisha na kutupatia vitambulisho vingine vya kuingia ofisini.

Tukiwa ndani ya ofisi tumepumzika katika kochi la kifahari huku jasho lililokuwa likitiririka likipulizwa na viyoyozi vilivyokuwapo ofisini hapo, tukimsubiria mwenyeji wetu, tuliona alama mbalimbali na matangazo yanayohusu uzingatiaji kanuni za usalama muda wote ukiwa hapo ofisini.

Meneja Ubora na Uzingatiaji Usalama, Deogratius Haule alituchukua na kutupeleka ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo ya hapa na pale kabla ya kuanza kutembelea shughuli za kampuni hiyo. Haule Alidadavua jinsi walivyojikita kuziishi itifaki za usalama katika shughuli zote za kampuni. Bw. Haule alitueleza kuwa tungeweza kutembelea maghala ya mizigo, karakana ya magari na stesheni za uwanja wa ndege kuangalia usalama unavyozingatiwa.

Ndani ya maghala

Tukiwa tunaelekea kwenye maghala ya mizigo tukiwa tumevalia mavazi ya kujikinga dhidi ya majanga, tulisimama kwenye lango la kuingilia ili kukaguliwa kwa mara nyingine. Namna tulivyokaribishwa katika karakana ya kisasa zaidi, lenye vifaa mbalimbali vya kazi lilikuwa jambo la aina yake.

Kwenye maghala ya mizigo iliyoagizwa nchini, kuna njia ndogo zilizonakshiwa kwa rangi ya bluu kwa ajili ya watembea kwa miguu na maeneo mengine yenye nafasi kubwa yaliyotofautishwa kwa rangi ya kijivu, yakitenganishwa kwa mistari ya njano, mahsusi kwa ajili ya usalama.

Pia kuna vioo mbonyeo vya ukubwa wa kati vilivyoning’inizwa ukutani kuwawezesha wafanyakazi kuonana kwa urahisi ili kuepusha ajali za hapa na pale. Kwa kuongeza, kuna njia maalumu za forklifts. Kwa kuongezea, kuna njia za forklift za kisasa zijulikanazo “Very Narrow Aisle (VNA)” zilizotengwa kuwezesha zoezi la uhamishaji wa mizigo kutoka eneo moja hadi lingine ghalani.

Bw Linus Musavangi, kiongozi wa timu katika ghala alitupitisha katika vidokezo vya usalama kuanzia katika hifadhi ya bidhaa za jumla, bidhaa za thamani (kama vile dhahabu na vito), bidhaa hatarishi, kemikali, mionzi, bidhaa zinazohifadhiwa katika ubaridi, wanyama na mochwari.

Taratibu za kiusalama katika uhifadhi wa mizigo inayosafirishwa nje ya nchi haina tofauti sana na ile inayoingia nchini. Vile vile kuna mizani inayopima mizigo uzito ghafi kwa ajili ya usafirishaji, kifaa cha upimaji kwa mionzi (x-rays) kinachopima uwepo wa mizigo hatarishi kabla ya kuingizwa katika ndege na kuhatarisha usalama wa ndege na abiria.

Ndani ya karakana ya matengenezo

Hata katika karakana, bado ajenda kuu ni usalama kuanzia ufanyaji kazi katika eneo hilo hadi utunzaji wa vifaa mbalimbali. Yovine Shine, mkuu wa usimamizi wa karakana hiyo ya Swissport aliitueleza kuwa karakana hiyo inafanyia matengenezo vifaa vyote vinavyosaidia huduma za usafirishaji mizigo na abiria katika ndege.

Usalama huzingatiwa kupitia matengenezo na ukarabati wa mara kwa mara unaofanyika hapa kituoni. Taarifa za programu za udhibiti kwa vifaa vyote hufanywa kupitia mfumo uitwao (MAXIMO).

“Kila tunapokarabati vifaa hivi tunafuata moja kwa moja mwongozo wa watengenezaji kwa sababu unapofanya vinginevyo kifaa hakitafanya kazi kwa kiwango sawa cha ufanisi wake unaotarajiwa au kinaweza kuharibika hadi kuhatarisha usalama wa shughuli zinazoendelea,” alidokeza Mhandisi Shine.

Katika vituo vya ndege

Kama ilivyo katika maghala, kulikuwa na vifaa mbalimbali na shughuli zilizokuwa zikiendeshwa na watu. Wafanyakazi waliokuwa wakiendesha vyombo vya kubebea mizigo, kupakia mizigo ndani ya ndege walikuwa wakifanya zoezi hilo vizuri na kwa uangalifu mkubwa huku wakiwa wamevalia mavazi ya kujikinga dhidi ya majanga. Utembeaji wa vyombo vya moto ulio katika utaratibu maalumu, wafanyakazi, matumizi ya ishara za mikono, uwekwaji sahihi wa chokes na cone inayoonyesha maeneo ya miruko ya ndege, zimefafanuliwa zaidi ili kueleza itifaki za kiusalama katika eneo hilo.

Msimamizi Mkuu wa Kitengo cha Kutoa Huduma Ndani ya Ndege, Kupakia na Kupakua Mizigo wa kampuni hiyo, Salum Juma alisema kuwa wanayo timu ya wafanyakazi waliopatiwa mafunzo bora. Wakiwa kazini, hufuata taratibu za msingi za kiutendaji na mwongozo kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama kinavyotakiwa.

“Tunajivunia kuwa na utamaduni bora wa kuzingatia usalama katika kampuni jambo ambalo linahakikisha usalama wa hali ya juu katika shughuli zetu na tunapongezwa na wateja wetu na ndiyo maana tunaendelea kuwa kinara katika soko.”

Baada ya kujifunza mengi kupitia utaratibu huo katika stesheni hizo, Haule pia alitutambulisha kwa timu ya vijana mahiri wanaofanya kazi kubwa nyuma ya pazia kuhakikisha ndege ina uzito na usawa sahihi kabla ya kuondoka.

Mafunzo

Swissport ina programu ya mafunzo inayofuata kanuni za IGOM (IATA) na viwango vya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA). Alielezea program mbili kuu zinazotumiwa kwa ajili ya kufundisha wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Programu ya kwanza ni ya lazima ambayo inalenga usalama, afya, ubebaji wa bidhaa hatarishi, ulinzi wa anga, moto, binadamu na ulinzi wa taarifa. Programu ya pili imejikita katika kutoa mafunzo maalumu kulingana na majukumu ya mfanyakazi kama vile usimamizi wa upakiaji mizigo na abiria katika ndege na usafirishaji mizigo.

Kampuni hiyo inajivunia kuwa na kituo cha mafunzo chenye ithibati kutoka Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IATA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ili kutoa kozi za zenye ithibati kutoka katika taasisi hizi mbili kubwa kwa wadau wa nje.

“Hatumpi jukumu mfanyakazi yeyote kabla ya kuhudhuria mafunzo, hiyo ndiyo sera yetu,” anaongeza Omary ambaye pia alibainisha kuwa kampuni hiyo ina mfumo wa usimamizi wa mafunzo unaohifadhi taarifa zote za mafunzo yanayotolewa kwa wafanyakazi.

Mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji

Kufanya mazungumzo na Ofisa Mtendaji Mkuu katika kampuni hiyo, Bw. Mrisho Yassin, lilikuwa ni somo tosha namna gani utamaduni wa kuzingatia usalama unavyotiliwa mkazo. “Hapa Swissport, hakuna mjadala katika suala la usalama tunapowahudumia wateja wetu wa makampuni ya ndege. Tumejikita katika kutoa huduma bora lakini wakati huo huo kumlinda kila mmoja wetu,” alisema Bw Yassin.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa baadhi ya Mifumo ya Usimamizi wa Usalama (SMS) imekuwa ni sababu ya kampuni kuboresha utendaji katika masuala ya kiusalama. Shughuli za Swissport zinafanyika kwa mujibu wa Taratibu za Uendeshaji (SOPs) ili kuendana na matakwa ya viwango vya ISAGO.

Ili kuimarisha utendaji wake wa kiusalama, kampuni pia imewekeza katika vifaa vya kiitendaji, vifaa vya kisasa vya usaidizi kiwanjani, rasilimali watu, uongozi, mifumo ya kuripoti na sera zinazohusiana na usalama.

Pia anaeleza pia kampuni ina mfumo wa usimamizi wa usalama (SMT) ambao huu una kazi ya kufuatilia sera ya utekelezaji wa usalama katika kampuni. Wafanyakazi wanashauriwa kutoa taarifa kuhusiana na matukio mbalimbali ya kiusalama muda wowote. Ripoti hizo zinatumika kama mafunzo kwa ajili ya kuboresha usalama.

Alipoulizwa juu ya hatua zilizochukuliwa na kampuni wakati wa janga la Uviko 19, alisema kwamba zilikuwa nyakati ngumu zaidi kuwahi kutokea katika biashara yao, ikisababisha kuporomoka kwa mapato yaliyotokana na kushuka kwa miruko ya ndege ghafla huku mwenendo wa biashara ya usafirishaji mizigo ukibaki katika hali yake ya kawaida kutokana na kuwapo kwa mahitaji makubwa ya usafirishaji mizigo ndani na nje ya nchi. “Ilitubidi kuendana na mabadiliko ya ghafla kwa nyakati zile kwa kuchukua hatua za kupunguza gharama za uendeshaji na kupunguza wafanyakazi huku tukihakikisha waliopo hawaathiriwi na janga hilo,” Yassin alisema.

Matarajio ya Swissport, kulingana na Yassin, ni kuona kampuni hiyo ikiendelea kuzingatia kanuni za usalama bila kuchoka na kutanua wigo wao katika eneo la mazingira, nyanja ambayo haijaguswa sana na Swissport.

Siku inafungwa kwa tabasamu

Darasa letu lilikoma saa 10:45 jioni huku tukiwa wenye bashasha licha ya uchovu uliotokana na kuwa na siku ndefu. Tulijikuta tukifurahi wenyewe tulipokumbuka kuwa mpango wetu ule wa kutumia chini ya masaa mawili ofisini kwenda kinyume chake lakini tukiondoka na somo kubwa la namna ya kuthamini usalama katika kila kinachofanywa na binadamu. Pongezi kwa wakufunzi wetu, Haule na Yassin!

Kuhusu Swissport

Swissport ilianzishwa mwaka 1996. Leo, kampuni hii ndiyo inayoongoza duniani kote katika huduma za ndani za uwanja wa ndege na usafirishaji wa mizigo, kutegemea na mapato na idadi ya viwanja vya ndege wanavyovihudumia. Swissport International Ltd. (Swissport) ndiye mtoa huduma anayeongoza duniani wa huduma za uwanja wa ndege na ushughulikiaji wa mizigo inayosafirishwa kwa njia ya anga iliyoko Zurich, Uswisi. Kampuni hutoa huduma katika viwanja vya ndege kwa zaidi ya abiria milioni 82 na huhudumia tani milioni 4.1 za mizigo kwa mwaka kwa niaba ya baadhi ya makampuni 850 ya wateja katika sekta ya usafiri wa anga. Ikiwa na nguvu kazi ya zaidi ya wafanyikazi 45,000, Swissport inafanya kazi katika zaidi ya vituo 269 katika nchi 47 katika mabara 6